Siku 11 baada ya kuteuliwa: Kamishna Jenerali Kasike afanya mabadiliko katika Jeshi la Magereza

Kunguru Mjanja

JF-Expert Member
Aug 22, 2012
2,036
3,927
Siku 11 baada ya Phaustine Kasike kuteuliwa kuwa kamishna jenerali wa Magereza, kiongozi huyo amefanya mabadiliko ya wakuu wa magereza nchini.

Kasike aliteuliwa Julai 13 na Rais John Magufuli baada ya Juma Malewa kustaafu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisa habari wa jeshi hilo, Lucas Mboje imetaja mabadiliko ya vituo vya kazi kwa baadhi ya wakuu wa jeshi hilo.

“Mabadiliko hayo yanalenga kuboresha utendaji kazi ndani ya Jeshi la Magereza ili kuongeza ufanisi,” imesema taarifa ya Mboje.

Akihojiwa na Shirika la Utangazaji la TBC hivi karibuni, waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliwataka wasaidizi wake kupitia sheria vizuri na kumpelekea mpango mzuri wa utekelezaji wa agizo la Rais, la kuwatumia wafungwa kufanya kazi za kilimo na ufugaji pamoja na kujitafutia chakula wao wenyewe.

Katika mabadiliko hayo aliyekuwa mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Julius Sang’udi amehamishwa na kuwa mkuu wa kitengo cha huduma za wafungwa makao makuu ya Magereza.

Nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida, Salum Hessein.

Pia, aliyekuwa mkuu wa Gereza la Mtego wa Simba, Msekwa Omary ameteuliwa kuwa kaimu mkuu wa Magereza Singida na nafasi yake inakaimiwa na mrakibu wa Magereza, Muta Tibalinda.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga amekuwa mkuu wa kitengo cha viwanda vya Jeshi la Magereza makao makuu na nafasi yake imekaimishwa kwa aliyekuwa mnadhimu wa Magereza Tanga, Emmanel Lwinga.

Wengine ni aliyekuwa boharia mkuu wa Magereza, Afwilile Mwakijungu aliyehamishiwa makao makuu ya Magereza kuwa mdhibiti mkuu wa Shirika la Magereza na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Goleha Masunzu.

Aliyekuwa ofisa mwandamizi sehemu ya utawala wa Magereza Mwanza, Benezeth Bisibe anakuwa kaimu mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara.

Naibu Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri, Joel Matani ameteuliwa rasmi kuwa mkuu wa chuo hicho.

Nafasi yake inachukuliwa na Wilington Kahumuza aliyekuwa naibu mkuu wa chuo hicho ambaye nafasi yake imechukuliwa na Ahmad Seleman.

Wakati huohuo, kamishna jenerali wa Magereza, Kasike amemteua mrakibu wa Magereza (SP), Amina Kavirondo kuwa msemaji mkuu wa Jeshi la Magereza.

Chanzo: Mwananchi
 
Hayo mabadiliko yawe na Tija na pia kwa walioteuliwa watambue haki za binadam na kuziheshim
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom