Sifa za mwanamke wa shoka-Biblia Takatifu

Dahafrazeril

JF-Expert Member
Jul 28, 2015
1,500
2,055
Sabalkheri wanaJamii Forums?.

Kama kichwa cha mada kinavyojieleza, Ifuatayo ni orodha ya sifa za Wanawake waliopata kuishi kabla na hata baada ya Kristo. Ukizisoma sifa hizi utajifunza mengi, ukiona hujaelewa basi ujue una tatizo la msingi sana.

Uwe Mkristu, Mmuhamadi, Mhindu, Mbudha, Mjaini nk unapaswa kusoma na kujifunza pasipo ukomo. Wazungu wanasema Sky Is The limit. Achana na misimamamo mikali iso na Mantiki.

Thubutu kuhoji chochote, kusaka popote na basi uweze kujiponya na chochote- aidha upofu wa kiroho, kimwili na kiakili pia.

Kasumba, itikadi ama msimamo wa aidha kiorthodoksi, ki-islam, kipagani na kadhalika si fahari. Ni uduni na upeo wa kijitakia. Kujua kitu usichokijua si ujinga, na kama una nafasi fanya hivyo na si kukaa pembeni na kufurahia ujinga wa kutokujua.

Kama vile Walter Russel wa Marikani kaskazini, mwanamaono, mvumbuzi na msanii alivyopata kusema "Udunya ni maradhi ya kujitakia, kipaji ni kujifadhili". Kwa lugha yake akimaanisha "Mediocrity is self inflicted, genius is self bestowed".

Karibu, twende pamoja..


Loisi na Eunike
https://womenofchrist.wordpress.com/2011/05/10/loisi-na-eunike/

2 Timotheo 1:1-5

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu, kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ikikaa kwanza kwa bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.

Hii ni mistari pekee katika biblia ambayo imewatambua Eunike na Loisi kwa majina yao. Loisi ni bibi yake Timotheo na Eunike ni mama wa Timotheo, mistari mingine inawaelezea ila si kwa majina yao. Kwa muda mrefu Timotheo amekuwa msaidizi wa Paulo katika huduma yake. Paulo aliiona imani kubwa aliyonayo Timotheo na kutambua kuwa imetokana na malezi bora na mafundisho toka kwa mama yake na bibi yake. Aliwatambua wanawake hawa kama watu imara katika imani na katika malezi pia.

Matendo 16:1-3 Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke myahudi aliyeamini; lakini baba yake alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo alimtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni myunani.

Mama yake Timotheo, Eunike alikuwa ameolewa na mtu wa mataifa na kutokana na kumheshimu mume wake hakimtahiri mtoto wake kama imani yake inavyosema. Hapa inaonyesha jinsi gani alikuwa mnyenyekevu na mwenye hekima. Pia Eunike alitambua kuwa pamoja na kwamba mtoto wake hakutahiriwa kama ilivyo desturi ya wayahudi, bado yeye analo jukumu la kumfundisha kweli ya Mungu tangu akiwa na umri mdogo. Alifanya hivi huku alipata ushirikiano toka kwa mama yake Loisi na kwa pamoja walimjengea Timotheo msingi imara wa imani.

Matendo 16:2 Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio

Mistari hii inatuonyesha pia kuwa wanawake hawa hawakusimama peke yao bali walikuwa bega kwa bega na kanisa la Mungu. Timotheo hakupata mwongozo wa kiroho kutoka kwa baba yake maana hakuwa mwamini lakini mama yake alihakikisha anamuweka karibu kabisa na watumishi wa Mungu, waamini wa mahali pamoja ili waweze kuwa msaada kwake.

Tunajifunza kuwa wanawake wana wajibu mkubwa sana katika kuwafundisha watoto wetu misingi ya neno la Mungu na wokovu. Ni muhimu sana hasa pale ambapo mwenzi wako hajaokoka maana Mungu anakuangalia wewe kuweka misingi bora ya kiMungu ndani ya moyo wa mtoto wako. Usipofanya hivyo shetani atapanda pando lake ambalo itakuwa ni ngumu sana kuling’oa.


Miriamu: Nabii wa Israeli
https://womenofchrist.wordpress.com/2011/01/20/miriamu-nabii-wa-israeli/

Kutoka 2 na 15 na Hesabu 12 na 20

Miriam alikuwa ni dada wa Musa na Haruni na Jina la Miriam lina maana ya anayempenda Bwana.

Hesabu 26:59 Na jina la mke wa Amramu aliitwa Yokebedi, binti wa Lawi, ambaye alizaliwa kwake Lawi huko Misri; na huyo Yokebedi akamzalia Amramu Haruni, na Musa, na Miriamu umbu lao.

Tunasoma habari za Miriam kwanza pale alipomlinda mdogo wake Musa alipokuwa amewekwa kwenye kisafina kingoni mwa mto, na ndiye aliyeongea na binti wa farao kumuelezea kuwa kuna mtu anayeweza kumnyonyesha huyo mtoto. Uwezo mkubwa wa kufikiri na kushawishi wa Miriamu ulimwezesha Musa kulelewa na kunyonyeshwa na mama yake mzazi hadi alipoacha kunyonya.

Miriam alishirikiana na Musa katika harakati za kuwatoa wana wa israeli utumwani Misri.

Mika 6:4 Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako.

Tunasoma pia kuwa Miriamu alikuwa ni nabii katika Israeli.

Kutoka 15:20a Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake haruni, akatwaa tari mkononi mwake;

Utumishi wake ulianzia pale alipohakikisha usalama wa Musa ambaye baadaye alikuja kuwa nabii mkubwa katika israeli. Miriamu pia alikuwa muimbaji na aliwaongoza wana wa Israeli kuimba wimbo wa sifa baada ya kuvuka kwa salama bahari ya shamu na Mungu kuliteketeza jeshi la Misri.

Kutokana na Miriamu kishi na Musa alipokuwa mtoto, kukaa naye muda mrefu na kuwa mkubwa kwake, kwa kiasi fulani alisahau utumishi wa kaka yake na kuona kuwa yeye anastahili kuwa sawa naye kiutumishi. Wakati Musa alipomuoa mwanamke wa Kushi na kusema kuwa Mungu amesema naye, Miriamu hakukubaliana naye. Kwanza alimsema kwa sababu ya kuoa mke wa Kushi na pili kwa sababu alisema Mungu amesema naye na kwanini aseme naye tu na sio yeye Miriamu. Alisahau kuwa Musa ndiye aliyekuwa ameitwa na Mungu kwa ajili ya taifa la Israeli.

Hesabu 12:1-2 Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke mkushi. Wakasema, Je! ni kweli Bwana amenena na Musa tu? hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao.

Wivu ulimpata Miriamu juu ya utumishi wa kaka yake na kusahau kuwa yeye pia ni mtumishi katika nafasi yake. Unapojisahau wewe ni nani na kudharau huduma uliyopewa na Mungu ni rahisi sana wivu kukupata juu ya huduma za watu wengine.

Vile vile Miriamu sababu anamfahamu Musa kwa undani zaidi basi kwa kuangalia udhaifu wake wa kibinadamu akadhani kuwa Mungu hawezi kumtumia bila kuwatumia na wao pia. Mara nyingi tumewanyooshea watumishi wa Mungu vidole kutokana na kuwa tunaangalia udhaifu wao na kusahau kuwa Mungu anaangalia zaidi ya sisi binadamu tunavyoangalia. Mheshimu mtumishi yeyote wa Mungu hata kama ni mdogo kwako au wewe ndiye uliyemshuhudia kuokoka. Tusiwaseme vibaya watumishi wa Mungu kwa lolote wanalolifanya maana hatujui maagano yao na Mungu.

Miriamu alimshirikisha kaka yake Haruni katika kumteta Musa na Mungu aliwasikia. Mungu alikasirika kwa tendo hili na akamwagiza Musa kuwa wote watoke nje ya hema ili akazungumze nao. Kutokana na ushawishi wake kwa Haruni katika kumteta Musa, Miriamu aliadhibiwa na Mungu pale pale. Musa alipoona Miriamu amepata ukoma akamlilia Mungu kwa ajili ya rehema kwa Miriamu, Mungu alisikia maombi yake lakini hakumponya pale pale, aliacha kwanza kwa muda wa siku saba ili iwe fundisho kwa miriamu na watu wote wakiwemo sisi tunaosoma habari hii siku ya leo.

Kama mtumishi wa Mungu, pale watu wanapokunenea vibaya usiweke kinyongo wala kulipiza kisasi, mwachie Mungu yeye ndiye mpiganaji wako na usiache kuomba rehema kwa ajili yao ili Mungu aweze kuwaponya. Hakika tumejifunza mengi kupitia maisha ya Miriamu.

Hesabu 12: 4-15 (Tafadhali ukiwa na nia soma mistari hii)

Elisabeti
https://womenofchrist.wordpress.com/2010/09/22/wanawake-wa-biblia-elisabeti/

Habari ya Elisabeti inapatikana katika kitabu cha Luka 1:5-80. Elisabeti alikuwa ni mwanamke anayemcha Mungu. Biblia inamzingumzia elisabeti na mume wake kama inavyoonyesha hapa:

Luka 1:6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

Alikuwa ni mwananke mwenye haki na akizifuata amri zote za Mungu. Pamoja na kuwa alikuwa mkamilifu mbele za Mungu bado hakuwa na mtoto. Watu wengi wanapoona Mungu anakawia kujibu maombi yao wanajiona kama wanadhambi au wamemkosea Mungu ndio maana hawajapata majibu ya maombi yao. Elisabeti alikuwa tasa si kwa sababu amemkosea Mungu, bali ilikuwa ni sababu ya mpango wa Mungu katika maisha yake.

Kujitoa kwa Elisabeti na mume wake kwa Mungu kulikuwa kwa kudhamiria toka moyoni, sababu ya upendo wao kwa Mungu na sio kitu kingine chochote. Hawakuacha kumtumikia na kumfuata Mungu sababu hawajapata watoto kama watu wengi wanavyoacha kumtumikia Mungu pale wanapopata matatizo katika maisha yao na kuona kama Mungu amewaacha.

Mungu alikuwa amewaandalia nafasi kubwa katika mpango wake wa ukombozi wa mwanadamu, kati yao alitakiwa kuzaliwa Yohana mbatizaji aliyakuja kumbatiza Yesu. Muda wa Yohana kuzaliwa ilikuwa bado ndio maana hawakupata mtoto mapema, kama elisabeti angekata tama na kumwacha Mungu basi asingeweza kuipata nafasi na heshima kubwa ambayo Mungu alikuwa amemwandalia.

Je ni jambo gani limekusumbua kwa muda mrefu na umeomba sana bila kuona matokeo yoyote? Inawezekana umefikia hatua ya kukata tamaa na kuona kama Mungu amekuacha, yumkini umefikiria kutafuta njia yako mwenyewe ya kukabiliana na tatizo hilo. Leo nakutia moyo, endelea kumngoja Bwana, usikate tamaa maana Mungu anampango kamili wa maisha yako na kuna jambo kumbwa anakuandaa kulifanya. Kwa sababu Mungu alikuwa amemfundisha Elisabeti uvumilivu na kumtumaini yeye ilimsaidia sana wakati anamlea mtoto wake, pale alipokuwa anashinda nyikani akihubiri na kubatiza Elisabeti hakuwa na hofu maana anauhakika kuwa ni mpango sahihi wa Mungu.

Isaya 40:31 bali wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.


Ruthi na Naomi
https://womenofchrist.wordpress.com/2010/04/13/ruthi-na-naomi/

1. Ruthi alimpenda na kumjali mama mkwe wake

Naomi alipomwambia arudi kwao baada ya mume wake kufariki alikataa na kuchagua kuambatana naye.

Ruthi 1:16-17 Lakini Ruthi akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia nami nitafia hapo na papo hapo nitazikwa.BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine cho chote kitanitenga nawe isipokuwa kifo

Alimuheshimu mama mkwe wake na kumchukulia kama mama yake mzazi.

2. Ruthi alimhudumia mama mkwe wake

Kwa upendo Ruthi alichukua jukumu la kumlea mama mkwe wake. Alienda kutafuta chakula kwa ajili yake na mama mkwe wake.

Ruthi 2:2 Ruthi Mmoabi akamwambia Naomi, “Nitakwenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.”

Upendo wake ulimpatia Ruthi sifa njema katika mji ule na jambo hilo likamfanya akapata mume mwema. Unavyomtendea mama mkwe wako hudhihirika katika jamii inayowazunguka.

Ruthi 2:11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wake alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu

3. Ruthi alikuwa tayari kushauriwa na kufundishwa

Utayari wake wa kufundishwa na kushauriwa ulimpelekea kupata baraka za Mungu. Kitabu cha Ruth 3 kinaonyesha jinsi alivyokuwa msikivu kwa naomi. Hakuwa mkaidi wala mwenye kiburi bali alitulia chini ya uongozi na uelekezi wa mama mkwe wake.

4. Ruthi alimbariki mama mkwe wake

Baada ya Ruthi kuolewa na kupata mtoto hakumzuilia naomi kuwa naye bali alimwacha amlee na kuwa naye. Naomi alipata faraja sana kuwa na mtoto wa Ruthi na wanawake wote wa mji walimpongeza na kumbariki. Ruthi alifanyika baraka katika maisha ya Naomi.

Ruthi 4:15-16 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe BWANA, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote! Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye aliyemzaa.’’ Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake

Sababu ya wema, utii na kuwa tayari kufundishwa na mama mkwe wake, Ruthi alibarikiwa na kitabu cha biblia kikaandikwa kwa kumbukumbu yake na kubwa zaidi uzao wake ukabarikiwa na masihi Yesu Kristo akazaliwa katika vizazi vyake.

Ruthi 4: 18-22

18, Hivi ndivyo vizazi vya Peresi:
Peresi alimzaa Hesroni,
19, Hesroni akamzaa Ramu,
Ramu akamzaa Aminadabu,
20, Aminadabu akamzaa Nashoni,
Nashoni akamzaa Salmoni;
21, Salmoni akamzaa Boazi,
Boazi akamzaa Obedi;
22, Obedi akamzaa Yese
na Yese akamzaa Daudi.

Dorcas
https://womenofchrist.wordpress.com/2010/02/10/wanawake-wa-biblia-dorcas/
Matendo 9: 36-42

Huko Jopa kulikuwa na mwanafunzi mwanamke aliyeitwa Tabita au kwa lugha ya Kigiriki, Dorkasi, yaani paa. Huyu mama alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37Hata hivyo aliugua akafa. Wakamwosha na kumlaza katika chumba cha ghorofani. 38Kwa kuwa Jopa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kuwa Petro yuko Lida, waliwatuma wenzao wawili wakamwambie, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.” 39Kwa hiyo Petro akaharakisha akaenda nao Jopa. Alipowasili wakampeleka hadi kwenye chumba alipokuwa amelazwa marehemu Dorkasi. Wajane wengi walikuwa wamemzunguka marehemu wakilia na kuonyesha mavazi ambayo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa hai. 40Petro akawatoa wote nje, kisha akapiga magoti akaomba; akaugeukia ule mwili akasema, “Tabita, Amka!” Dorkasi akafumbua macho na alipomwona Petro, akaketi. 41Petro akamshika mkono akamsaidia kusimama. Ndipo alipowaita wale waamini na wajane aka wakabidhi Dorkasi akiwa hai. 42Habari hizi zilienea sehemu zote za Jopa. Na watu wengi wakamwamini Bwana.

Biblia inamwelezea Dorkas kama mwanamke mkarimu sana ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Yesu. Tunaambiwa kuwa katika maisha yake alikuwa mtu mwenye kutenda mema na kuwasaidia maskini, hapa hatujaambiwa kuwa yeye alikuwa ni tajiri wa Moyo wake wa upendo kwa wengine na uanafunzi wake mwema kwa Yesu ulimfanya kuwa na huruma kuwaona watu wanakosa nguo za kuvaa na ndipo akaamua kuwashonea watu hao nguo wengi wao wakiwa ni wajane. Aliifanya huduma hii kwa moyo wa upendo sana ndio maana pale alipougua na kufa wajane wengi walimzunguka na nguo zao wakilia na waliposikia petro yupo karibu walimwita ili aweze kumuombea apate uzima maana walikuwa bado wanamwitaji sana.

Dorkas aliitambua huduma ambayo Mungu alikuwa amempa na alimtumikia Mungu kwa uwezo wake wote katika huduma yake na kuwagusa watu kwa kiasi kikubwa sana. Haijalishi ni huduma gani Mungu ameiweka ndani yako, yakupasa kuifanyia kazi na kumtumikia Mungu kwa uwezo wako wote. Huduma sio lazima uwe mchungaji, mwinjilisti au mwimbaji, waweza kuwa mkarimu wa wageni na wasio na makazi, kuwaangalia wajane na yatima, kuwategemeza watumishi wa Bwana, kuiangalia nyumba ya Bwana n.k. Pia haikupasi kuwatangazia watu wewe unafanya nini bali watu waone kile unachokifanya na wamtukuze Mungu kwa hilo.

1Timotheo 4:14 Usiache kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee wa kanisa walipokuwekea mikono

Matendo yetu na yaonyeshe tu watumishi wa Mungu, ili kwa neema ya Mungu tuweze kuongezewa siku za kuishi kuendelea kuifanya kazi ya Mungu.


Sara
https://womenofchrist.wordpress.com/2009/12/07/wanawake-wa-biblia-sara/
Mwanzo 12-16

Mungu aliwaahidi Abraham na Sara uzao kama nyota za angani, Mwanzo 15:1-7 . Wote walipokea ahadi hii kwa furaha wakimtazamia Mungu kuitimiliza. Pamoja na kwamba Sara aliiamini ahadi ya Mungu ya kuwapatia motto, alipoona kama Mungu anachelewa alipata hofu na kuamua kuchukua hatua yake mwenyewe. Kwanza alianza na kumlaumu Mungu kwamba amemfunga asizae na kusahau ahadi ambayo waliipokea.

Mwanzo 16:2a Sarai akamwambia Abramu, basi sasa Bwana amenifunga tumbo nisizae,.

Akaanza kudhani kuwa ahadi ambayo Bwana aliwapa ni ahadi ya Abramu mumewe pekee na si yeye hivyo akamwambia mumewe apate mtoto na mjakazi wake. Alisahau kwamba yeye na mumewe ni kitu kimoja na ahadi ni kwao na sio kwa mjakazi wake. Aliamua kumsaidia Mungu kutimiliza ahadi yake kwa kuona kama anachelewa.

Mwanzo 16:2 Sarai akamwambia Abramu, basi sasa Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu, labda nitapata uzao kwa yeye. Abram akaisikiliza sauti ya Sarai.

Jambo hili lilikuja kuleta majuto makubwa kwa Sara maana mjakazi wake alipopata ujauzito alipata kiburi na kumdharau Sara. Na matokeo ya kosa hili yanandelea hadi leo. Mwanamke anaushawishi mkubwa sana kwa mumewe na ni vyema sana kumuomba Mungu mara zote ili atuwezeshe kuwa na busara na hekima maana kama Sara hakumwambia Abramu kuzaa na mjakazi wake Abramu asingefanya hivyo.

Tunaona pia uaminifu wa Mungu kwa ahadi yake, pamoja na kwamba Sara alikata tamaa na kujipa majibu mwenyewe Mungu bado aliitimiza ahadi yake ya kumpa mtoto ambaye atakuwa mrithi.


Abigaili
https://womenofchrist.wordpress.com/2009/11/09/wanawake-wa-biblia-abigaili/

1 Samweli 25:2-3 , 25

2-3, Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na mali huko Karmeli, yeye alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. 3Jina la mtu huyo aliitwa Nabali na jina la mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe ambaye alikuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake.

25, Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake, jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye.

Busara na ujasiri wa Abigail uliiokoa familia yake na maangamizi toka kwa Daudi na watu wake. Ukisoma kitabu chote cha 1 Samweli utaipata habari hii kwa upana. Abigaili alikuwa ni mwanamke mwenye akili njema na mzuri wa sura pia bali mumuwe Nabali alikuwa ni mpumbavu. Kwa akili na hekima aliyokuwa nayo aliweza kuituliza hasira ya mfalme Daudi alipotaka kuwaangamiza kutokana na makosa ya mumewe Nabali.

Katika habari hii ya Abigaili tunaona sifa kuu tatu alizokuwa nazo. Kwanza alikuwa ni mtu mnyenyekevu maana alipopata taarifa ya jinsi mume wake alivyomjibu Daudi na ambavyo hasira ya Daudi imewaka , mara moja alichukua punda na kumfuata Daudi na kuomba msamaha kwa niaba ya mume wake ambaye wakati huo alikuwa akila na kunywa bila kujali chochote. Hakwenda kulumbana na mumewe bali aliamua kunyenyekea na kulichukua kosa la mume wake kama lake na kisha kutafuta suluhisho.

Vilevile alikuwa ni mwanamke mkarimu. Alipoenda kumlaki Daudi hakwenda mikono mitupu bali alibeba chakula cha kuwatosha wote waliokuwa pamoja naye maana aliambiwa kuwa vijana wa Daudi walienda kuomba chakula kwa mumuwe wakanyimwa hivyo kwa moyo wake wa ukarimu aliamua kuwalisha japokuwa walikuwa wamedhamiria kuwaangamiza. Sifa nyingine aliyokuwa nayo ni Upatanishi. Aliweza kuzuia hasira ya Daudi juu ya Nabali mume wake na kisha kumweleza Nabali yaliyotokea kwa upole kesho yake baada ya ulevi kumtoka. Asingekuwa na sifa hii angeweza kumwendea Nabali pale tu aliposikia Daudi anakuja na matokeo yake angesababisha maafa maana kwa upumbavu wake Nabali angeamua kupambana na Daudi.

Abigaili ni mfano mzuri sana wa jinsi mwanamke anayemjua Mungu anavyopaswa kuenenda. Maisha yetu ni lazima yajae unyenyekevu, ukarimu na upatanishi ili tuweze kuziponya ndoa zetu, familia, kanisa na jamii kwa ujumla. Pia Abigaili anatufundisha kuchukuliana, pamoja na kuwa mumewe alikuwa mpumbavu yeye alijifunza kuchukuliana naye na hivyo wakafanikiwa kujenga maisha yao.


I dedicate this message to all Women in this Forum. Mungu akubariki sana.
 
Back
Top Bottom