Siasa ya Tanzania: Ujamaa na Kujitegema? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Siasa ya Tanzania: Ujamaa na Kujitegema?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Bakari Maligwa, Sep 2, 2012.

 1. Bakari Maligwa

  Bakari Maligwa Member

  #1
  Sep 2, 2012
  Joined: Aug 18, 2010
  Messages: 65
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mwanzo; baada ya uhuru na kama ilivyosadifu TANU (chama cha ukombozi wa Mwafrika), Tanzania ilifuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwenye makrabasha ya siasa ya TANU na baadaye CCM hata kabla ya kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 iliandikwa kwamba: "UJAMAA NA KUTITEGEMEA NDIO NJIA PEKEE YA KUJENGA JAMII YA WATU WALIO SAWA NA HURU."

  Miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika na miaka takriban 48 ya muungano wa Tanganyika na Zanaibar (Tanzania) tumekuwa tukisomesha na hata kuimbishwa juu ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ujamaa wa kiafrika kwa mujibu wa mawazo ya Mwalimu Julius K. Nyerere (1922 hadi 1999) na hata Katiba ja JMT ya 1977 iliandikwa kwa misingi hiyo (tazama Ibara ya 3[1] ya katiba ya JMT ya 1977). Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa; Tanzania imekuwa inafuata siasa isiyoelezeka kwenye utendaji achilia mbali nadharia ya siasa yenyewe.

  Mwalimu (J. K. Nyerere) alitamani sana ujamaa na kujitegema uwe ndio njia ya kujenga jamii, uchumi na siasa! Watu wa Tanzania waliandaliwa kuchukua nafasi yao kama wamiliki wakuu wa uchumi wa nchi na waendeshaji wa shuhuli zote za maendeleo ya nchi na watu wake. Azimio la Arusha la 1967 ndilo lililokuja na sera za kuufanya uchumi wa Tanzania umilikiwe na umma kupitia mikono ya serikali ya watu kama ilivyo kwenye Ibara ya 8 ya Katiba ya JMT ya 1977.

  Tanzania imebadilisha mwelekeo; tangu lilipopitishwa lile linaloitwa Azimio la Zanzibar (Maamuzi ya Zanzibar) nchi imekuwa haifuati tena siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Chama kinachotawala siasa na uchumi; yaani CCM, kimebinafsisha siasa na uchumi umefanywa mali ya watu wachache wenye fedha na wachuuzi wa haki na uhuru wa wananchi wanyonge wasiyokuwa na hali wala mali. Ardhi kubwa na yenye uzalishaji mkubwa wa chakula (mashamba ya kilimo), madini na gesi wamepewa wawekezaji ambao kwa sehemu kubwa wananyonya na kubakisha asilimia 4 hadi 5 ya mrabaha [!] kama sehemu ya mapato kiduchu...wananchi wanaendelea kutaabika kwenye nchi yao huku wageni wakipewa usaidizi wa uvunaji wa rasilimali ya nchi!

  Ujamaa na kujitegemea umebaki nadharia ya kuwahadaa wananchi huku kila tone la utajiri likivunwa na wanyonyaji wa ndani (wazungu weusi na mawakala wa mabwanyenye) na wanyonyaji na mabepari wa nje wanaotumia mitaji yao katika kufanikisha unyonyaji unaosimamiwa na sheria mbovu zilizotungwa katika kulinda maslahi ya wawekezaji. Sipati picha; hivi, ni wapi siasa yetu inapochukua akili na falsafa zake wakati tukielekea kwenye mfumo mpya na uandikaji wa katiba mpya? Sijui; hata kama, wanaochangia maoni ya katiba mpya kama wanalijua hil ![?]...nasema sijui!

  Mwisho, waungwana na wananchi wenzangu; je, tumekaa chini kutaakari hatma ya siasa yetu? Au, tunadhani kwamba mfumo wa siasa za "vurumai" yaani, vyama vingi vya siasa ndio siasa yetu? Sidhani kama ni sahihi kudhani kwamba Tanzania ni nchi ya siasa ya vyama vingi[?] Nadhani tuna wajibu wa kutafuta jinsi tutakavyoielezea na kuitafsiri siasa ya nchi yetu. Nadhani tusipofanya hivyo tunaweza kujikuta katika hamkani na au sintofahamu ya kuwa na mfumo wa siasa isiyozingatia utashi wa maisha ya wananchi wengi wa Tanzania katika kipindi cha miaka 50 au zaidi ijayo! Natahadharisha juu ya kutokea kwa vurugu za maoni ya kisiasa kama hatua za makusudi za kuiainisha siasa ya nchi kama falsafa na mtazamo wa uendeshaji wa siasa utakaowekea misingi itakayofuatwa na wananchi wote kwa jinsi katiba itakavyopendekeza. Siasa ni mwendo murua wa uendeshaji wa shughuli za wananchi kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kwa hivyo basi; Tanzania inahitaji tafsiri sahihi ya siasa yake ya ndani na ya nje ili tusipotee kwenye songombingo na sintofahamu za kisiasa zinazoanza kuchukua nafasi ya ubinafsi wa kimakundi na hata kimtazamo wa tofauti ya falsafa.

  TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA; KUJENGA NI KAZI KUBOMOA KAZI RAHISI! MUNGU IBARIKI TANZANIA; MUNGU TUBARIKI WATANZANIA, NA WAPE HEKIMA WANANCHI WA TANZANIA WACHANGIE KWA HEKIMA NA BUSARA ILIYO KUU KWENYE UANDIKAJI WA KATIBA MPYA NA KAMWE WASISAHAU KUAINISHA VEMA NA KWA MAKINI SIASA YA NCHI YETU. TANZANIA INAHITAJI SIASA SAFI KATIKA UJENZI WA JAMII ILIYO HURU, INAYOZINGATIA USAWA NA UADILIFU WA MAISHA YA KIJAMII, KISIASA NA KIUCHUMI.
   
Loading...