Siasa, Mpira vs Bongo Fleva

Chilojnr

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
302
1,306
SISI TULIWAAMBIA, MKATUPUUZIA

Unakumbuka kipindi kile ulipokuwa unabishana na watu mtaani kwako kuhusu Diamond na Ali Kiba nani mkali? Sijui nani ana tuzo nyingi? Sijui nani amefanya hivi na vile? Unakumbuka ama unataka nikukumbushe?

Unakumbuka kipindi kile ulipokuwa ukikaa chumbani kwako na kusema kuna mwamba wa Hip Hop katoa ngoma kali kishenzi, acha niisikilize, halafu nafungulia sauti mpaka mwisho, ngoma ina mdundo kupita kawaida.

Basi achana na hayo manake naona kama nakuvuruga! Unakumbuka kipindi kile ulipokuwa unasikia tuzo za msanii bora ukampigie kura kwenye tovuti maalumu na kukimbilia huko haraka sana ili msanii wako achukue tuzo? Unakumbuka ama sasa hivi unajiona umekua na huwezi kufanya vile tena?

Nikwambie tu kwamba kile ulichokuwa ukikifanya hakikuwa utoto, ujinga ama kitu kibaya, moyo wako ulitawaliwa na mapenzi makubwa ya muziki na wasanii wa Bongo, ulikuwa unawapenda na ulipenda kuwasapoti kwa nguvu kubwa, yaani ni kama nilivyokuwa nikifanya mimi ile zamani.

Ushajiuliza kwa sababu gani sasa hivi hufanyi? Ushajiuliza kwa sababu gani sasa hivi hata ukimsikia msanii katoa ngoma kali, tena video hujisikii hata kwenda kuicheki Youtube? Usisingizie bando bhana! Na wala usisingizie muda, najua una muda mwingi na pia bando unalo la kutosha, ila kuna kitu tu kinakufanya hutaki kwenda, hicho kitu kimesababishwa na wanamuziki wenyewe. Endelea kwenda nami chini, nakuahidi sitokuchosha kwa hizi floo tamu.

Unaonaje tukiwalaumu WCB? Tuseme wao ndiyo wanakwenda kulimaliza kabisa soko la muziki Bongo ama? Au basi tufanye tusiilaumu hiyo lebo, unaonaje tukiwalaumu wasanii wengine kwa kutokujitangaza sana kama WCB? Wale wasanii wavivu ambao baada ya kutoa ngoma na kusikika mitaa minne, wameridhika bila kugundua kuna mitaa zaidi ya milioni mia tano duniani.

Muziki umefifia sana! Umekosa sapoti kutoka kwa mashabiki nikiwemo mimi. Kuna ngoma zimetoka wiki hii lakini huwezi kuamini hata sijazisikia, na sina muda wa kuzisikia, unajua kwa sababu gani? Wanamuziki wameyaondoa mapenzi ya ngoma zao mioyoni mwetu.

Kuna wasanii kabla ya yote, yaani namaanisha kutoa ngoma, kwanza linatengenezwa bonge moja la kiki! Yaani hiyo kiki ikitoka tu, ndani ya wiki hiyohiyo inaachiwa ngoma moja matata sana, kwa sababu kiki imetangulia, basi unajikuta ukienda kutazama hiyo ngoma.

Kwa miaka ya nyuma, yaani nyuma ya 2021 wanamuziki walifanikiwa sana kwa kuwa ‘sisi wanyonge’ tuliendekeza sana umbeya kuliko mambo mengine. Yaani tukisikia mwanamuziki fulani yupo na fulani, wenyewe tunaona rahaaaa, tunafurahi sana lakini si kwa sasa.

Kuna kiki kadhaa zilitoka hapo nyuma, watu wakaziua kama hazipo vile, zikatengenezwa nyingine na nyingine halafu watu wakazipotezea, unajua kwa sababu gani? Jibu ni moja tu, kwa sasa sisi Watanzania hatutaki kuendeshwa na kiki, tunataka kazi ziongee zaidi.

Kama huwezi kufanya muziki bila kiki! Muziki huo una mwisho wake, utaweka kiki hii, kiki ile lakini mwisho wa siku watu watakupotezea na kuendelea na mambo yake, si mnajionea jamani ama mnyonge mie nadanganya?

WCB walikuja kwa kasi sana, wakatengeneza himaya yao, kwa kweli iliwabeba sana, ikatufanya tuwasahau wengine, yaani ukiingia mitandaoni na sehemu nyingine, ni wao tu. Of course walifanikiwa kwa kile walichokihitaji, ila nikutonye tu washikaji wamechangia sana kuufanya muziki wa Bongo Fleva kudrop kwa sasa. Unajua kwa nini? Kwanza usinimaindi, weka mahasira yako pembeni twende sawa, hayo mapovu yahifadhi, najua una nguo nyingi chafu, na sabuni huna.

Vichwa vyetu vilituambia hakuna wanamuziki kama WCB, tukasema ukiwa lebo nyingine video yako haitoweza kuangaliwa na watu wengi kama wewe si WCB, yaani ili uvume, usikike ni lazima kwanza tuanze na hawa WCB, na kila aliyeingia, kwa kweli akatusua! Washikaji nawapa Big Up! Wamepambana sana.

Sasa bwana! Si unajua binadamu anachoka. Wewe si unapenda sana kula baga, unaonaje tukikupa baga ule kila siku, yaani mwaka mzima uwe unakula baga tu, utachoka, si ndiyo? Sasa ndiyo ilivyotokea kwa WCB.

Leo tunamsikia Diamond, kesho Rayvann, kesho mwingine, mwisho ikafika hatua tukachoka, ndiyo! Sisi ni binadamu na huwa tunachoka, sasa tunahitaji kupewa kitu kipya, kwa watu wapya lakini hakuna, mwisho wa siku sasa tunakimbilia kwa wasanii wachanga wa nje, ndiyo, ni kwa sababu hakuna jipya linaloendelea nchini.

Kuwasikiliza wasanii haohao kila siku inaboa! Kusikiliza aina ya muziki huohuo nayo inaboa. Tunatamani waje wengine, watuchangamshe kidogo, ila hawawezi, na hawawezi kwa sababu tayari kuna mizizi ya lebo fulani imekwishawekwa ardhini, huwezi kuing’oa kirahisi, japo tukiamua kuing’oa, itang’oka tu.

Mwangalie msanii kama Zuchu, amekuja kwa kasi, akavuma sana, unajua kwa sababu gani? Ni mtu mpya, tuliamini alikuwa na kitu kipya, hivyo tukamsapoti kwa lengo la kusikia upya wake, tena kubwa zaidi alikuwa ndani ya lebo pendwa ya WCB.

Leo Watanzania hatuna muhemko na muziki kwa sababu utawasikia wasanii walewale wa siku zote, wakiimba aina ya muziki ule ule. Yaani kama wimbo wa kwanza alililia kuachwa, wa leo analilia kusalitiwa, yaani kilio kile kile ila utofauti ni chanzo cha kilio chake.

Wakati wasanii wakijiuliza tatizo ni nini hasa! Mara ghafla bin vuu, mpira ukaibuka kwa kasi ya kishada, Wabongo sasa tukawa bize kufuatilia mpira, MO Dewji na GSM wakatuchanganya kabisa. Tukasahau kama kuna ngoma mpya zilikuwa zinatolewa.

Hatujakaa sawa, rais wetu, John Pombe Magufuli akafariki dunia, watu wakachanganyikiwa, akili zetu zikavurugwa, muziki ukapigwa kapuni kabisa. Ngoma za mazishi zikatolewa, watu hawakutaka kuzielewa, mwisho wa siku wakasema yule Kepteni Komba alikuwa noma sana kwa nyimbo za mazishi, unajua kauli hii ilimaanisha nini? JIONGEZE.

Ndani ya msiba huohuo (yaani kipindi cha mazishi) Simba alikuwa akicheza mechi za kimataifa, napo likatufanya tuwe bize kwa mambo ya siasa na mpira, muziki ukasahaulika kabisa.

Wakati tukisema basi msiba ukiisha tutarudi kwa kasi kwenye muziki, mara jamaa anayeitwa Kigogo naye akavuma kwa kasi, akatufanya kuwa bize, wakati tunajifariji acha mazishi yaishe, hatujakaa sawa CAG naye kaibuka na ripoti zake, wanamuziki wakasema ngoja tutoe ngoma mpya tuone mambo yakoje, watu hawataki kabisa kuelewa, wanazungumzia siasa na mpira tu.

Muziki umepoteza mvuto na sababu kubwa ni kwamba tumechoka kusikia wasanii walewale wakiimba kitu kilekile na ndiyo maana ngoma mpya ikitolewa, mtu anakwambia hiyo itakuwa inahusu kitu fulani tu, na kweli ipo hivyo.

Siasa imeshika sana maisha yetu, kila kitu kinapelekwa na siasa, wakati Watanzania tumevurugwa na ripoti ya CAG halafu muda huohuo unatoa ngoma yako, huwezi kupita kwenye kichaka hiki aiseee.

Wanaoua muziki wa Bongo ni wanamuziki wenyewe, wasimtafute mchawi ni nani. Kipindi cha nyuma tulisema Bongo Muvi imeuliwa na waigizaji wenyewe, kila kitu kilichokuja kwa kasi na kufa, wahusika ndiyo wamekiua wao wenyewe.

Kama unaona watu hawapendi kusoma vitabu basi jua waandishi ndiyo wameua mioyo ya watu kwenye usomaji wa vitabu, baadaye ukiona watu wanaachana na mpira na kufanya mambo mengine, basi jua ni wachezaji ama viongozi wa mpira ndiyo haohao walioua mpira wao.

Leo nashangaa tu ngoma mpya zinatoka, hakuna hata bodaboda inayozipiga, ngoma mpya zinatolewa, hakuna gumzo lolote lile mitaani, yaani watu wanachukulia poa kabisa.

Bongo Fleva inatakiwa kuwekewa gesi na kushtua mapigo yake ya moyo, ipo mahututi na inatakiwa kupona haraka sana. Itapona kwa namna gani? Mimi sijui, ila wanamuziki wenyewe wanajua, na inawezekana kwenye kujua huko wanaogopa kufanya kwa kuhisi kuna wengine wataneemeka zaidi yao.

Kiki hazina maana kwa sasa! Muziki wa hapa Bongo hauwezi kufufuliwa kwa kiki. Ni lazima wasanii wabadilike na waangalie njia mbadala, kama hawa wakongwe wameshindwa, wasisite kuwapa nafasi hata vijana wapya wakaja kulete vitu vipya kama ilivyokuwa kwa singeli.

Watanzania tunataka kuwasikia watu wapya, wakipewa nafasi na kufanya kile tunachotaka kukisikia. Leo mtu ukimpa simu anakuuliza hii ina Kigogo humu? Hii nitamuona CAG? Kadiri muda unavyozidi kwenda mbele, Wabongo wanautupa muziki wetu, wanakimbilia kwenye siasa, mpira na wakichoka sanaaaaa, wanajiburudisha na series za Kikorea ama Uturuki kutoka Azam.

Ukiwauliza muziki vipi? Wanakujibu sifuatilii muziki wa kiki! Wanamuziki kazi kwetu. Twende tukanyoe kwa kinyozi ama tumtafute msusi akatusuke?

Yuleyule, Mnyonge namba 56.
 
Bandiko refu lakini msumari ndio huu hapa. Kiukweli wasanii wa Tanzania kuanzia mziki mpaka filamu hawana idea mpya yoyote

"Muziki umepoteza mvuto na sababu kubwa ni kwamba tumechoka kusikia wasanii walewale wakiimba kitu kilekile na ndiyo maana ngoma mpya ikitolewa, mtu anakwambia hiyo itakuwa inahusu kitu fulani tu, na kweli ipo hivyo."
 
Bandiko refu lakini msumari ndio huu hapa. Kiukweli wasanii wa Tanzania kuanzia mziki mpaka filamu hawana idea mpya yoyote

"Muziki umepoteza mvuto na sababu kubwa ni kwamba tumechoka kusikia wasanii walewale wakiimba kitu kilekile na ndiyo maana ngoma mpya ikitolewa, mtu anakwambia hiyo itakuwa inahusu kitu fulani tu, na kweli ipo hivyo."
Noma sana. Wanatakiwa kufanya jambo.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom