Siagi ya karanga kutoka Kenya yapigwa marufuku Afrika Mashariki

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,499
9,279
Picha

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimepiga marufuku uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa za siagi, zilizotengenezwa kwa karanga kutoka Kenya.

Zimepigwa marufuku kutokana na bidhaa hiyo, kubainika kuwa na vimelea hatarishi kwa afya za walaji.

Kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), bidhaa hizo zimezuiwa kuingia Tanzania kutoka Kenya ili kulinda afya za Watanzania, kutokana na uchunguzi uliofanywa na Shirika la Viwango la Kenya (KBS) kubaini zina sumu kuvu, inayoweza kusababisha ugonjwa wa saratani kwa binadamu.
Nchi za Rwanda na Uganda, pia zimepiga marufuku bidhaa hizo kuingizwa na kutumiwa katika nchi hizo kutokana na athari zake.

Bidhaa za siagi zilizopigwa marufuku na KBS baada ya kubainika kuwa na athari katika afya za binadamu ni Truenutz iliyokuwa ikizalishwa na Truenutz Kenya, Fressy iliyokuwa ikizalishwa na Fressy Food Company Limited, Supa Meal iliyokuwa ikizalishwa na Supacosm Products Limited.

Nyingine zilizozuiwa kuingia sokoni ni Nuteez iliyokuwa ikizalishwa na Jetlak Foods Limited, Sue’s Naturals iliyokuwa ikizalishwa na Nature’s Way Health, Zesta iliyokuwa ikizalishwa na Trufoods Limited na Nutty.

Ofisa Habari wa TBS, Roida Andusamile, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa kutokana na athari ya bidhaa hiyo, TBS iliamua kuwatuma maofisa wake kuisaka madukani na kuzuia siingie tena nchini.

“Tuna maofisa wetu mbao wapo mitaani kuhakikisha bidhaa liyoingia madukani haitumiki nchini, wengine wapo katika harakati za upimaji wa bidhaa hiyo ili kujiridhisha kuhusu sumu kuvu na kiwango cha sumu hiyo,” alisema.

Andusamile alisema siagi iliyozuiliwa kuuzwa na kusambazwa nchini ni ile inayotoka Kenya, lakini wananchi wanaruhusiwa kuendelea kutumia siagi inayozalishwa hapa nchini, kwa sababu ni salama na imekuwa ikipimwa mara kwa mara tangu kiwandani mpaka kuingia sokoni.

“Siagi inayozalishwa Tanzania haina shida kwa sababu maofisa wetu wanaipima tangu ikiwa kiwandani wakati wa utengenezaji wake hadi ikiwa sokoni,” alisema Andusamile.

Baada ya KBS kugundua kuwa kuna sumu kuvu, inayoweza kusababisha saratani, shirika hilo lilipiga marufuku uzalishaji na usambazaji wa siagi hiyo iliyokuwa ikiuzwa karibu katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Katika taarifa yake iliyotolewa mwezi uliopita, KBS ilisitisha uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa hiyo, hadi pale itakapojiridhisha kuwa athari zilizopo katika bidhaa hiyo zimeondolewa.

Kufuatia taarifa ya KBS kuwa bidhaa hiyo ina sumu, inayoweza kusababisha vimelea vya saratani, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda (RFDA) nayo ilitangaza kusitisha uingizwaji na usambazwaji wa bidhaa hiyo nchini humo.

Kwa mujibu wa RFDA, serikali ya Rwanda inaendelea na utafiti ili kujua aina hasa ya sumu na kiwango kilichopo katika bidhaa hiyo. Mamlaka hiyo pia iliutangazia umma kuhusu usitishaji wa bidhaa hiyo na kuwataka wananchi kutoitumia.

“Kuna uthibitisho uliooneshwa katika taarifa ya KBS kuhusu bidhaa saba za siagi zilizo chini ya viwango, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda inawataka wananchi kusitisha mara moja utumiaji wa bidhaa hiyo mpaka uchunguzi utakapofanyika,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RFDA, Dk Charles Karangwa.

Hali hiyo pia ilifanya Shirika la Viwango la Uganda (UBS), kuchukua hatua kama zilizochukuliwa na Tanzania, Kenya na Rwanda na kuzuia uingizaji na usambazaji wa siagi hiyo katika soko la Uganda.
 
Kwa Tanzania ya viwanda ya sasa kwenye miji mingi kuna wajasiriamali wadogo wadogo wengi sana wanaotengeneza hizo peanut butter hadi majumbani na kuzijaza kwenye vikopo vya plastic na kuziuza madukani hadi na majirani. Je usalama wake kwa walaji ukoje?
 
Back
Top Bottom