Si haki kuzitwisha mzigo nchi zinazoendelea kwenye suala la mabadiliko ya tabia nchi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,006
1,026
Na Fadhili Mpunji

VCG111320191371.jpg


Wakati dunia inatafakari mambo yaliyojadiliwa na makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi COP26 uliofanyika huko Glasgow Scotland, suala la uwajibikaji kwenye kukabiliana na tatizo hilo limekuwa gumzo tena, na China kwa kushirikiana na India zimejitokeza kuwa mstari wa mbele kupaza sauti ya nchi zinazoendelea, kuhusu mambo yanayoonekana kuwa si haki kwa nchi hizo.

Kwenye mkutano wa Glasgow pande zote zilijadili na kukubaliana kuwa, nishati ya visukuku na hasa makaa ya mawe inachangia sana kuongezeka kwa hewa ya ukaa na joto duniani na kupunguza matumizi ya makaa, ni moja ya njia zenye ufanisi za kukabiliana na kuongezeka kwa joto duniani, na hata mabadiliko ya tabia nchi. Bila shaka dunia inatambua kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea sasa duniani, ni matokeo ya matumizi ya muda mrefu ya nishati ya visukuku ambayo imetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi zilizoendelea.

Ni kweli kupunguza matumizi ya makaa ya mawe kunaweza kuwa njia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini pia tunatakiwa kuangalia hali halisi ya nchi zinazoendelea. Tunaweza kuona makaa ya mawe bado ni nishati muhimu kwa nchi zinazoendelea kwa kuwa bado ni nishati ya gharama ya chini kuliko nishati nyingine. Nchi nyingi zinazoendelea zinategemea nishati hiyo kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na hata uzalishaji wa umeme. Kwa hiyo kutaka nchi hizo ziache kutumia makaa ya mawe si jambo la busara. Kiuhalisia ni kwamba itachukua muda mrefu sana kabla ya kufikia lengo hilo.

Taarifa iliyokuwa inataka kutolewa baada ya mkutano huo ilikuwa na lugha ya kutia hofu kidogo. Nchi zilizoendelea zilitaka taarifa iseme matumizi ya makaa ya mawe yaondolewe kabisa, lakini China na India zilikuwa makini kwenye kuchagua matumizi ya maneno ya taarifa ya mwisho baada ya mkutano huo. China na India ziliona ni bora kutumia maneno “kupunguza polepole” badala ya “kuondoa kabisa” matumizi ya makaa ya mawe. Tofauti ya maneno haya ni kubwa, na inaendana na hali halisi ya nchi nyingi zinazoendelea, ambazo bado zinatumia makaa ya mawe kama nishati muhimu kwa maendeleo yake ya uchumi.

Kama leo matumizi ya makaa ya mawe yatapigwa marufuku duniani, kuna uwezekano mkubwa maendeleo kidogo yaliyopatikana katika nchi za Afrika yatakuwa matatani, na huenda nchi hizo zitarudi nyuma sana. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Zhao Lijian amesema badala ya nchi zilizoendelea kuziambia nchi zinazoendelea kuacha kutumia makaa ya mawe, zinatakiwa kukumbuka kuwa nchi zinazoendelea bado zina safari ndefu sana kabla ya kufikia kiwango cha nchi zilizoendelea na kupiga marufuku matumizi ya makaa ya mawe. Lakini amesema ni bora kama nchi zilizoendelea zikaonyesha mfano kwanza kwa kuacha kabisa matumizi ya makaa ya mawe, na zitoe fedha, teknolojia na kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea kufanikisha mpito kutoka matumizi ya makaa ya mawe hadi kwenye nishati safi.

Toka suala la mabadiliko ya tabia nchi lianze kujadiliwa na makubaliano mbalimbali yanayofikiwa, nchi zilizoendelea zimekuwa zinaongea zaidi kuliko kufanya utekelezaji. Ahadi ya kutenga fedha kwa ajili ya mfuko wa kuzoea mabadiliko ya tabia nchi imekuwa ya kusuasua, na ahadi ya kusafirisha teknolojia za matumizi ya nishati mbadala kwa nchi zinazoendelea bila haijatekelezwa. Kwa hiyo kuzuia kabisa matumizi ya makaa ya mawe kabla ya hayo kutekelezwa litakuwa tatizo kubwa zaidi kwa nchi zinaoendelea.
 
Unataka waendelee kuchichafua dunia, wenzake wanandaa makazi huko sayari nyingine...
 
Back
Top Bottom