Shule 20 mkoa wa Pwani zakabidhiwa kompyuta mpakato 100

esther mashiker

JF-Expert Member
May 29, 2018
616
552
1087713

Shule 20 za mkoa wa Pwani zimekabidhiwa kompyuta mpakato 100 kupitia mradi wa Umoja wa Mataifa (UN) unaohamasisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kufundisha.

Mradi huo unaoitwa Global e-Schools and Communities Initiative (gesci) unatekelezwa katika shule 40 za mikoa ya Pwani na Morogoro ukilenga kumaliza matumizi ya chaki katika kufundisha.

Akikabidhi kompyuta hizo baada ya walimu na wajumbe wa bosi za shule za sekondari kumaliza mafunzo ya Tehama mjini hapa, ofisa elimu mkoa wa Pwani, Alhaj Abdul Maulid amesema shule zilizopewa vifaa hivyo ni zile zilizoanza kufundisha kwa kutumia teknolojia hiyo tangu mradi huo ulipoanza mwaka 2016.

“Hii ni fursa adhimu kwa shule zetu za mkoa wa Pwani na tumeona mafanikio makubwa kwa sababu uelewa wa watoto darasani umeongezeka tangu teknolojia hii ilipoanza kutumika kufundishia,” amesema. Awali, mratibu wa mradi huo mkoani Pwani, Bahati Juma alisema mbali na kompyuta hizo, kila shule iliyo kwenye mradi huo imepatiwa projecta kurahisisha ufundishaji.

Amesema zipo shule zimeongeza kompyuta baada ya kubaini matokeo chanya ya matumizi ya teknolojia hiyo. “Kuna shule hazikuwa na umeme lakini baada ya kuwapelekea mradi wametafuta namna nyingine ya kupata umeme na wameanza matumizi ya teknolojia hii jambo linalopaswa kuigwa na shule nyingine,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mandela Chalinze, Rose Umila alisema matumizi ya Tehama yameongeza uelewa na ufaulu wa wanafunzi wake tofauti na wakati walimu wanatumia chaki kufundishia. “Somo la sayansi halifundishwi kinadharia, ukianza kufundisha unamuonyesha mtoto namna moyo unavyofanya kazi anaelewa zaidi na hivyo hawezi kufeli kabisa, tumeamua kutumia teknolojia hii na karibu kila mwalimu ana kompyuta mpakato yake,” amesema.
 
Back
Top Bottom