Shirika la PRIDE mbona hatuwaelewi, hisa za Serikali zilipoteaje?

Mende Mzoefu

New Member
Apr 28, 2016
4
3
Kwakweli Taarifa za Mkaguzi wa Serikali zimetatiza. Kwa mwenendo huu wasio na mioyo ya subira na shukurani wasije wakageuza na kuanza kusema kuwa nanili ni shirika ambalo mkaguzi wa serikali anadai kuwa serikali ilikua na hisa zake humo alafu zikatokomea, linalo toa mikopo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo kwa masharti nafuu ingawa wakati mwingine hupiga kalenda tarehe zake za utoaji wa mikopo (hapa tuwakaribishe wataalamu wa baraza la kiswahili watusaidia kufupisha hii kaulimbiu maana imekua ndefu mno)

================

Shirika la PRIDE limeongelewa sana kwenye Vyombo vya Habari vya hapa Njini.

Hili ni Shirika lisilopenda “Misifa” ya kujitangaza tangaza kwenye vyombo vya Habari mara kwa mara kwahiyo lilipo chomozea wengine tukataka kujua kunani huko tena! Lakini Swala kubwa zaidi ni kuhusu utata wa umiliki wa Sirika hilo kutokana na kile ambacho Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu wa Serikali kudai kuwa Hisa zilizokua zinamilikiwa na Serikali kuhamishwa "kinyemela" kutoka Serikalini kumilikishwa Mmiliki ambaye hakutajwa. Msajili wa Hazina naye akajibu kwamba Shirika hilo halikuwa la Serikali hivyo taarifa ya Mkaguzi haikuwa sahihi. Haya ni Mambo ya Kisheria na hapa kuna Mamlaka mbili zinatoa Matamko yanayo kinzana.

Nani mwenye ukweli nani "kachemka". Ingawa kwa sisi ambao hatuna Taaluma ya Sheria tunajiuliza kuwa kweli Taasisi Nyeti kama Ofisi ya Mkaguzi wa Serikali inaweza ikashindwa kupata Tafsiri Sahihi ya umiliki wa Hisa katika Mashirika hadi kufikia hatua ya kutoa Taarifa “fyongo” kwa Miaka miwili mfululizo….kweli!….kweli! Kana kwamba hiyo haikutosha, jambo hilo lilihojiwa na Wabunge mwaka jana. Ningekua Mie ndio mmiliki “Halali” wa Shirika hili na nina Uhakika kuwa Sikuhamisha Hisa za Serikali kinyemela, Walai tena ningeiburuza Serikali Mahakamani kwa kunisema vibaya.

Lakini Taarifa ya Mkaguzi ilienda mbali zaidi na kuongelea mambo mengine kuhusu Shirika Hilo. Mosi ilidaiwa kuwa Shirika halijawahi kukaguliwa na Taasisi yake. Wahusika wakafafanua kuwa Ukaguzi huwa unafanywa na Wakaguzi Binafsi. Pili taarifa nyingine ikadai kuwa Sirika hilo kwa sasa limelemewa na Mzigo Mzito wa Madeni kutoka taasisi za Fedha hapa nchini hivyo kuathiriwa kiutendaji. Sijui tuseme pole kwa Wahusika ama tuwashangae. Shirika lilikopa fedha kutokana na Mipango yake Mizuri ya Maendeleo lakini linakuja kushindwa kulipa. Why…Kwanini?

Mbona Shirika hili linaonekana kuwa na mtandao mzuri wa Matawi na biashara nzuri tu, kwanini lishindwe kulipa Madeni? Kama Sirika lilikopa Fedha kutokana na Mahitaji yake, likakopa na Fedha ZOTE za Mkopo zikaingia kwenye Uendeshaji Why….kwanini likwame kulipa madeni? Chjiii, Hivi kumbe Mtalaamu wa kukopesha anaweza kushindwa kurejesha fedha alizokopa nayeye! - Ndio yale yale ya fundi vyatu anaye vaa vyatu ambavyo vidole vinachungulia inje utafikiri Sendoz kumbe vyatu.

Kiukweli hivi sasa Shirika linaonekana kuchechemea tena kweli kweli. Hivi sasa kuna Ucheleweshaji wa Malipo ya Mishahara kwa Wafanyakazi. Zamani Mishahara ilikua haiwezi kulipwa zaidi ya Tarehe 25 ya Mwezi husika lakini sasa hivi mishahara inaweza kutoka ata Tarehe Mbili ya Mwezi. Sambamba na hilo kuna mdau mmoja anaye hisiwa kuwa ni Mtumishi huko alililamikia mabadiliko katika taratibu za Upatikanaji wa Mikopo ya Watumishi hivi sasa, jambo linaloweza husishwa na Ukwasi wa Shirika kwani zamani jambo hili lilikua rahisi kama kusinzia.

Upande wa Wateja, maombi yao ya Mikopo yanapigwa danadana kiasi kwamba badala ya kupatikana kwa Mkopo baada ya siku saba hivi sasa upatikanaji wa Mikopo ni Maajaliwa ya Mnyazi Mungu kwani inaweza kupita Mwezi bila Mkopo kutolewa. Hapo ndipo lilipofika Shirika hili ambalo lilikua linajivunia kuwa "Kinara" wa Asasi Zitoazo Mikopo kwa Wafanya Biashara ndogo ndogo - Africa mashariki na Kati. Zamani walikua wanasema kuwa PRIDE NI SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LINALO TOA MIKOPO YENYE MASHART NAFUU KWA WAFANYABIASHARA NDOGO NDOGO.

Kwa mwenendo huu wasio na mioyo ya Subira na Shukurani wasije wakageuza na kuanza kusema kuwa Nanili ni SHIRIKA AMBALO MKAGUZI WA SERIKALI ANADAI KUWA SERIKALI ILIKUA NA HISA ZAKE HUMO ALAFU ZIKATOKOMEA, LINALO TOA MIKOPO KWA WAFANYABIASHARA NDOGO NDOGO KWA MASHARTI NAFUU INGAWA WAKATI MWINGINE HUPIGA KALENDA TAREHE ZAKE ZA UTOAJI WA MIKOPO (Hapa tuwakaribishe Wataalamu wa Baraza la Kiswahili watusaidia kufupisha hii Kaulimbiu maana imekua ndefu mno)

Shirika hili lilikua la kutolea Mifano kwakweli. Lilisifika sana na waliokuwepo miaka ya 1994 – 2002 hivi, wanalimwagia sifa kuwa Watu walikua wanalilia kupata nafasi ya kujiunga ili kupata Huduma ya mikopo. Pale tawi la Tanga Wamama walikua wanakimbia mbio na watoto mgongoni kuwahi muda maana walikua wkichelewa wanatozwa adhabu au kufutwa kabisa. Viongozi Mbalimbali wa Kitaifa walikua wakitolea Mifano Shirika hili kwenye Hotuba zao. Mabenki yenyewe yalikua yanaligwaya kwakua mshindani wao katika sekta ya Fedha hasa katika utoaji wa huduma ya Mikopo.

Hivi sasa mambo hayako vile tena. Shirika ni sawa na “Wapo lakini hawavumi”. Wafanyakazi wake hawana uchangamfu tena maana hawajui ya kesho yatakuweje. Wengine muda mwingi wapo kwenye viunga vya kuuzia magazeti wakitizama hasa kurasa za Matangazo. Kakika Masomo ya Biashara kuna kitu kinaitwa Business Life Cycle, ule mstari unachorwa unapanda hadi kileleni alafu unaanza kushuka kwa nyuzi kali – Binafsi naogopa kufikiria kwamba tayari shirika hili linachukua huo muanguko wa nyuzi kali kuelekea chini mithiri ya wale wapiga mbizi wa kwenye michezo ya kuogelea ya Olimpiki. Kwanini naogopa Shirika hili lisichukue huo muanguko wa kibiashara?
  1. Ni kwa sababu ya Sifa kubwa iliyojizolea Shirika hili. Ni vema likaendele kuwepo na kuwa mfano wa Mashirika yaliyo simamiwa na kuendelezwa na Wabongo wenyewe.

  2. Shirika lina wafanyakazi wengi ambao wanatunza Familia – Wake/waume, Watoto, wazazi na ndugu kiasi kwamba lingeangukia pua Waathirika kiuchumi watakua wengi - yaani ni Maelfu kwa idadi.

  3. Wateja hawatapata Mahali pengine pakupata Huduma Bora yenye Masharti Nafuu kama walivyokua wanapata kutoka Shirika hili.

  4. Likiangukia pua kuna Uwezekano wa kushindwa kulipa Akiba za Wateja wake. Ikifikia huko kitakua kitu kibaya kwani Suala hilo litaichafua Serikali maana tafsiri itakua kwamba Serikali imeshindwa kulinda Maslahi ya Watanzania. Zaidi ya hapo, Jambo hil lita athiri imani ya Watu kwa asasi za Kifedha. Tuombe sana sala lisifikie huko kwani ata wasimamizi wakuu watatakiwa kutueleza kulikoni.
Lakini Swali la Msingi hapa ni - Je Shirika hili limefikaje huko. Au ndio yale ya Wakunga ya kusema kuwa Ngoma ikivuma sana Vuuuh vuuuh vuuuuuh! Mwisho wake ni kupasuka na Mphuuuuuum! Yawezekana moja au nyingine ya Mamboyafuatayo kuwa Sababu.
  1. Mabadiliko au Ushindani katika biashara ya Ukopeshaji. Ongezeko la Taasisi za Fedha Nchini,
Nyingine, badala ya kuwa tu na Masharti nafuu, zenyewe zina Huduma na Masharti “Amazing”, ….kama tunavyopenda kusema sisi vijana wa siku hizi.
  1. Mipango mibaya ya kimkakati inaweza kusababisha Shirika likafika mahala pabaya. Kwa mfano kupanuka bila mpangilio kunaweza kusababisha Shirika likashindwa kujimudu katika Mahitaji na Matumizi.

  2. Kupitwa na Wakati kutokana na kutumia Taratibu na kanuni zile zile huku ubunifu ukiwekwa kando huku Wenye nalo wakiendelea kulewa Sifa za kuwa Kinara katika sekta hii.

  3. Wateja kuota Sugu ya ukorofi wa kutorejesha Marejesho ambapo hutumia mbinu za kisasa kufanya udanganyifu wa kujipatia mikopo na kushindwa kuirejesha.

  4. Wizi na ubadhirifu mdogo mdogo wa Wafanyakazi Matawini. Hawa wakiamua wanaweza kushirikiana na Wateja kutengeza Mikopo Hewa ambayo hailipiki. Pia wanaweza kuchota
Fedha kiujanjaujanja na kutokomea nazo gisani.

Huenda hili nalo linaweza kuwa limechangia kwani tumeshaona sawadi nono ikitangazwa

kwenye vyombo vya habari na Shirika kutolewa kwa watu watakao mkamatisha Chalii mmoja

ambaye alikua muajiriwa wa Shirika hili bahati mbaya Shetani akampata akaona ajilipe

Fedha na kutokomea nazo kizani. Kutokana na Sawadi yenyewe ilivyokua imenona, bila shaka

Chalii alikwapua “Mkwanja wenye akili.”

Watanzania katika hili embu tushikamane ili kuhakikisha kuwa anakamatwa ili arudishe Fedha

za Shirika walau ata zikatumike kutoa mikopo kwa Wateja au ata kupunguza hayo madeni

aliyoyasungumsia mkagusi wa Serikali.
  1. Ufujaji Mkubwa wa Menejimenti ya Shirika ambapo Wasimamizi wakuu wanaweza wakaamua kujigawia Fedha za Shirika kama vile Chakula cha Misaada kinavyo gawiwa kwenye maeneo ya njaa. Kuna njia nyingi ya kufanya hivyo na zinajulikana. Kwa Mashirika Mengine Wakubwa wanaweza wakajikopesha Mamikopo makubwa alafu yasiingizwe kwenye orodha ya Madeni ya ndani. Wakubwa wanaweza wakawa wanajiandikia na kujipitishia malipo ya kufa mtu mara kwa mara. Tungekua na uwezo wa kuona Maisha wanayoishi hawa wakubwa tungeweza kusema zaidi juu ya hili lakini kwakua hatujui vizuri Maisha yao na mali wanazo miliki hadi hapa hatuwezi kuwaongelea kwa mabaya.

  2. Sirika kuishi zaidi ya Uwezo wake ambapo unakuta linakua na Gharama za uendeshaji kubwa kulingana na kipato. Hilo linaweza kusababishwa na kukodi Mijengo ya Ofisi yenye Gharama kubwa. Safari za gharama zisizo na tija, Mishahara minono kwa baadhi ya watu ni kama vile anavyosema Mheshimiwa Raisi kuwa kuna watu wengine Mishahara yao inawafanya Waishi kama kwenye Upepo wakati ndani ya Taasisi hizo hizo wapo wenye vijimishahara viduchu vinavyo wafanya waishi kama Ahera.

  3. Inawezekana ni ule ukweli kwamba Sirika halipati mawazo mapya kutokana na kuwa na baadhi ya Wafanyakazi walioshika nyadhifa zao tangu enzi na enzi hivyo kuwasababisha kufanya kazi kwa mazoea. Ushindani wa sasa unahitaji ubunifu mkubwa na “utundu” Fulani ambao unaiwezesha Biashara kuhimili mikiki mikiki ya Ushindani wa soko.

  4. Ushirikishaji na Mawasiliano hafifu. Kuna Mashirika mengine yalifeli mitihani kutokana na Menejimenti kuona kama wanaweza kila kitu. Wanachokiwaza wenyewe ndio sahihi bila kuwa na Mikutano ya kujadili na kupanga mikakati na Watu walio jirani na wateja. Kwa njia hiyo ni lazima anguko lije kwani hawa wanaohenyeka na wateja huko hawajioni tena kuwa ni sehemu ya Uongozi wa Shirika. Inafika sehemu hawawi tena upande wa Menejimenti, wanakua kivyao vyao tu na hawajali matokeo ya utendaji wao.
Hatuwezi kujua nini hasa kinalisibu Shirika hili. Bila shaka hali yake haijafikia hatua mbaya ya kushindikana kurekebishika. Wahusika wakubwa wachukue hatua za haraka ili kulinusuru na kulirejesha katika Mstari na kuwezesha Maelfu ya Wateja na Wafanyakazi wake kuendelea kufaidi matunda mema.

Mimi nina amini kuwa PRAID inaweza ikazaliwa upya na kurudi kwenye Chati za Moja bora tena hasa kwakua yenyewe ina Mtaji mkubwa wa Mabilioni ya Fedha yaliyoko Mikononi mwa Wateja wake zikiwa kama madeni ya mikopo. Mabilioni yale yakikusanywa kwa bidii ndipo mikakati mizuri iwekwe kwa nidhamu na utaalamu, hakika mambo yatakuwa mwerere tena. Zaidi ya hapo, Sirika lina Wafanyakazi wazuri na Wateja watiifu, kwanini isishindikane Bwana?

Hivi nilikua nawaza tu au nimeandika kabisa?
 

Attachments

  • YA PRAIDI..docx
    22.8 KB · Views: 97
Naomba uangalie tafsiri ya neno ukwasi kama umelitumia sahihi
 
Back
Top Bottom