'Shetani' Mtanashati na Amri Kuu 10

Habibu B. Anga

JF-Expert Member
May 7, 2013
6,557
25,671
Sasa, unaweza kupata nakala za Kitabu changu cha "NYUMA YA ULIMWENGU WA SIRI NA UJASUSI".
kitabu kina kurasa 442 na ndani yake kuna makala 17.
Bei ya kitabu hiki ni Tsh 50,000/-

Pia waweza kupata kitabu changu cha "OPARESHENI ZA KIJASUSI ZILIZOFANIKIWA ZAIDI"
Kitabu hiki kina kurasa 214 na ndani yake nimechambua Oparesheni 6 tofauti.
Bei ya kitabu hiki ni Tsh 15,000/-

Wasiliana nami kwa namba 0759 181 457

Niko naandika makala fulani hivi taratibu taratibu kutokana na pilika za hapa na pale siku si nyingi nitaiweka hapa. Wakati tunasubiri makala hiyo ikamilike nimeona nishee nanyi kwa kifupi sana kisa kimoja ambacho binafsi kinanivutia sana..

Ni kisa kinachomuhusu moja ya 'wapigaji' (tapeli) mashuhuri zaidi na aliyekuwa na mbinu mwanana kiasi cha kwamba namuweka katika kundi la "Wapigaji Daraja la Kwanza". Huyu alikuwa ni mahiri kiasi kwamba alifanikiwa kuuza mara mbili mnara maarufu wa Eiffel ulipo jijini Paris kwa wafanya biashara wakubwa maarufu. Umahiri wake katika 'upigaji' uliwahi kutishia hata 'afya' wa mfumo wa kibenki na uchumi wa marekani.

Jina lake halisi imekuwa ni gumu kujulikana kwani kipindi cha uhai wake aliwahi kutumia zaidi ya majina 47 tofauti.. Pia alikuwa na hati za kusafiria za zaidi ya nchi 17 tofauti.
Maisha yake yaligubikwa na mlolongo wa uongo kiasi kwamba ni ngumu hata kujua asili yake na familia yake aliyotokea.
Lakini jina rasmi lililokubalika kumuita ili angalau kujua ni nani anayeongelewa lilikuwa ni Victor Lustig.

a4f6f8ff08a171edc6fac90579fe9b3b.jpg

Victor Lustig

'Genesis'

Victor Lustig inaaminika na wengi kuwa alizaliwa Austria-Hungary (Czech Republic ya sasa) na akiwa katika umri wa makumi alihamia nchini Marekani.

Akiwa bado kijana Lustig alijiingiza katika 'mishe mishe' za mitaani za halali na haramu. Rafiki zake wanasema kwamba mwanzoni kabisa Lustig alijifunza michezo ya karata na akawa mahiri kiasi kwamba unaweza kudhani hakuna duniani mtu mwingine mwenye uwezo wa kuchezea karata kumshinda Lustig.

Lustig alimudu kwa umahiri kila aina ya 'card trick' (palming, slipping cards, dealing from the bottom n.k.). Kitu pekee ambacho labda kilimshinda ilikuwa ni kuzifanya karata ziongee, na kwa kuwa hilo haliwezekani basi yafaa kusema Lustig alikuwa ni 'master' wa michezo ya karata.

Kipindi hiki ilikuwa inakaribia miaka ya 1950 na ndio vitaa kuu ya pili ilikuwa inaishia, na uchumi wa marekani ulikuwa unakua kwa kasi kubwa sana na watu wa kipato cha kati na cha juu walikuwa wanaongezeka kwa kasi sana. Lustig akaiona fursa ya 'malisho' mapya ya maisha yake ya uhalifu na akaamua kujiingiza rasmi katika 'upigaji'.

Kama nilivyoeleza katika makala mbali mbali kuwa wahalifu wengi wa Daraja la kwanza huwa wanakuwa na falsafa wanayoiamini na kuwaongoza. Kwa mfano Pablo alijiongoza kwa Sera ya 'Plata O Plomo'.

Lustig kwa upande wake pia alikuwa na falsafa aliyoiamini na kuifuata na kumfanya kuwa pengine ndiye 'mpigaji' mashuhuri zaidi katika historia ya ulimwengu..

Katika vitabu vya dini Mwenyezi Mungu aliwapa wanadamu amri kuu 10 za kuwaongoza kuishi maisha matakatifu, lakini yeye Lustig alijiwekea amri kuu 10 za kumuongoza kufanikisha Utapeli.

Amri hizo alizojiwekea zilikuwa ni hizi;

1. Kuwa msikilizaji makini (hii ndio sifa inayofanikisha utapeli, sio kuongea sana.

2. Usijionyeshe Umeboreka (never look bored)

3. Muache unayeongea naye aonyeshe mlengo wake wa kisiasa kisha kubaliana nae.

4. Muache unayeongea naye adhihirishe imani yake ya dini, kisha jifanye una imani sawa naye.

5. Gusia maongezi ya kimpenzi, lakini usiingie ndani sana isipokuwa tu pale unayeongea naye akionyesha kupendelea maongezi hayo.

6. Kamwe usigusie mazungumzo ya magonjwa au ugonjwa isipokuwa tu kama kuna ulazima wa kuzungumzia.

7. Kamwe usilazimishe kutaka kujua mambo binafsi ya unayeongea naye (kuwa mvumilivu kadiri unavyoongea naye ataropoka mwenyewe)

8. Usijisifu au kujikweza - acha umuhimu wako ujidhihirishe wenyewe.

9. Usiwe na muonekano rough (mchafu/hovyo hovyo)

10. Usilewe.

Hizi ndizo amri kuu 10 za Bw. Lustig alizozifuata na kumuongoza katika maisha yake na kumfanya kuwa 'mpigaji' mashuhuri zaidi katika historia..

Mashine ya kuprint noti na Kuuza mnara wa Eiffel.

Moja ya matukio ya kukumbukwa zaidi yaliyofanywa na Lustig ilikuwa ni kuwauzia watu Mashine ya kuprint noti za dola ya Marekani.

Waliouziwa hawakuwa wajinga kiasi kama unavyoweza kuhisi bali Lustig alikuwa anatumia akili ya ziada ambayo mtu aliyekuwa anatapeliwa abadani asingeweza kutia shaka kwa muda huo.

Kama tunavyofahamu kuwa kuna meli za starehe ambazo watu hupanda pale wanapokuwa mapumziko kwa ajili ya kuvinjari tu (Cruise Ships). Lustig alipendelea zaidi meli za starehe zilizokuwa zinasafiri kutoka New York mpaka Jijini Paris ufaransa. Abiria wa meli hizi walikuwa ni watu wenye kujiweza kwa kipato na hii ilimvutia zaidi Lustig.

Lustig alikuwa akishakupanda katika meli, alitumia masaa kadhaa kufanya upembuzi wa abiria gani amtapeli. Akishakupata mtu wa kumtapeli kwa kutumia uwezo wake wa hali ya juu wa kujieleza na kumteka mtu kwa maongezi alikuwa anamuita Chemba na kumuonyesha kiboksi kidogo cha saizi ya kati ambacho kwa ndani kinakuwa na mfumo complex na kina vitufe vya kubonyeza kwa juu. Kiboksi hiki alikitengeneza kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba kinadanganya macho na mtu kuamini kuwa kuna sayansi ya hali ya juu imetumika kukitengeneza.

Kisha Lustig alikuwa anampa mtu maelezo kuhusu kiboksi hicho kuwa kina mfumo maalumu pamoja ya madini ya 'Radium' ambapo kina uwezo wa kucopy noti za dola 100 za marekani kwa usahihi wa 100%.

Ili kuthibitisha hilo Lustig aliweka vipande kadhaa vya karatasi zenye rangi nyeusi ndani ya kiboksi hicho na kusubiri kwa muda kadhaa ambapo kiboksi hicho kinaprint fedha halali kabisa noti ya dola 100 ya marekani.

Kisha Lustig anamueleza zaidi kuwa kiboksi hicho kina uwezo wa kuprint noti moja ya dola 100 kwa kila masaa 6. Kutokana na mtu kuhisi kuwa atapata faida kubwa akiwa na kiboksi hicho chenye uwezo wa kumpatia dola 100 kwa kila masaa 6 pasipo kuvuja jasho hivyo walikuwa wakinunua kwa moyo mkunjufu kabisa na Lustig aliwauzia kiboksi hiki kwa dola elfu thelathini za marekani kwa kiboksi kimoja.

Kumbuka hapa wako ndani ya meli inayosafiri kuelekea Paris, Ufaransa kwahiyo huyu mtu akishanunua kiboksi baada ya masaa sita kiboksi kile kitaprint noti ya dola 100, baada ya masaa sita mengine kitaprint noti nyingine ya dola mia.. Lakini baada ya hapo kitaanza kuprint karatasi za kawaida nyeusi na hapa ndipo mtu hushituka kuwa amekwisha tapeliwa lakini kwa muda huu meli inakuwa imeshafika Paris na Lustig ameshashuka kwenye Meli na kutokomea.

efa8a23754df1ada8d957bd178cd859b.jpg

Eiffel Tower: mnara uliouzwa mara mbili na Lustig kwa wafanyabiashara mashuhuri jijini Paris.

Kuna siku Lustig alikuwa Paris, akiwa ameshashuka kwenye meli baada ya kumuuzia mtu mashine ya kuprint hela. Katika mizunguko yake akakutana na habari kwenye gazeti ambayo ilimsisimua. Habari hii ilikuwa inahusu taarifa ya serikali ikizungumzia kuhusu ni jinsi gani ilivyokuwa inaingia gharama kubwa kutunza mnara wa Eiffel.

Makala hii lengo lake hasa ilikuwa ni serikali wanajitetea baada ya raia kulalamika kuwa serikali hawako makini kuutunza mnara huo kwani umekuwa mkuu kuu na haupendezi tena. Katika makala hiyo serikali ilijitetea kuwa hata kuupaka rangi mnara huo ni gharama kubwa mno kwahiyo wananchi wawe wapole tu.

Taa ikawaka kichwani kwa Lustig.. Akang'amua hii ilikuwa ni fursa adhimu kwake kujitajirisha.

Lustig akaandaa vitambulisho na nyaraka za kugushi za serikali ya ufarasa ambazo zilimtambulisha yeye kama Naibu Mkurugenzi katika Wizara ya Mawasiliano akishugulikia masula ya Posta na Telegram. Kisha akaenda katika hoteli de Crillon ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ndio hoteli ya hadhi ya juu kabisa katika mji wa Paris na akakodi chumba na ukumbi kwa wageni wenye hadhi (executives).

Baada ya hapo akawasiliana na wafanya biashara wakubwa sita wenye makampuni makubwa zaidi ya biashara ya vyuma chakavu na akawaalika hotelini kwa mazungumzo maalumu.

Bila kusita wafanyaniashara hao wakawasili hotelini na moja kwa moja mazungumzo na Lustig yakaanza. Lustig akajitambulisha na kuwaeleza kuwa kikao hicho ni cha siri na serikali imewateua wao kwa ajili ya zoezi maalumu. Akawaeleza kuwa kama wanavyoona kwenye vyombo vya habari gharama za kutunza mnara wa Eiffel imekuwa kubwa kiasi kwamba serikali imeshindwa na hivyo suluhisho pekee ni kuubomoa. Hivyo basi serikali inataka kuwapa mmoja wapo kati yao deal ya kuubomoa mnara huo na kuchukua vyuma vitakavyo patikana.

Lakini akawasisitiza kuwa suala hilo ni aibu kwa serikali ndio maana hawakutaka hata kutangaza tenda hadharani hivyo anaomba ishu hii anayoongea nao iwe ni siri kubwa kwani serikali haitaki hilo suala lifahamike mpaka pale itakapofikia siku chache kabla ya kuubomoa. Akawaeleza kuwa tenda hiyo atapewa yule ambaye ataweka dau kubwa kuliko wenzake (highest bidder).

Baada ya mazungumzo hayo Lustig akawachukua kwa kutumia gari ya kifahari ya Limousine aliyokuwa ameikodi na kuwapeleka mpaka kwenye mnara wa Eiffel kwa ajili ya kuukagua pamoja na kupeana maelekezo zaidi.

Baada ya kufika kwenye mnara wakiwa bado wanapeana maelekezo, Lustig pia akatumia mwanya huu kuwasoma wafanyabiashara hao ili kujua yupi mwenye shauku zaidi ya dili hiyo na yupi itakuwa raisi kwake kumtapeli. Baada ya kuwachunguza kwa kina karata yake ikaangukia kwa mfanyabiashata aliyeitwa Andre Poisson.

Baada ya kumaliza zoezi hili kesho yake wafanyabiashara hao wote waliwasilisha bids zao na kwa kuwa Lustig tayari alikuwa amemlenga Andre Poisson hivyo aliwasiliana naye huyu pekee kumtaarifu kuwa serikali imempitisha na kumpa hiyo deal.

Akamualika tena pale Hotelini kwake kwa ajili ya mazungumzo zaidi na kusaini mkataba wa hiyo deal. Wakiwa hapo hotelini watu wawili tu, Lustig pia akampa ombi maalumu bwana Andre Poisson kuwa amejitahidi sana kumpigia debe mpaka amepewa hiyo dili hivyo akamuomba 'asimsahau'.

Baada ya kusaini mkataba, Bw. Andre Poisson akalipia gharama ya kupewa hivyo vyuma (Eiffel Tower) pia akampa na asante Lustig. Yaani kwa maneno mengine akalipia gharama za kununua Eiffel Tower pia akatoa na rushwa kwa ajili ya kusaidiwa kununua mnara huo.

Baada ya kusaini na makabidhiano ya pesa kila mtu akaondoka na njia yake. Wiki kadhaa baadae ndipo ambapo Andre Poisson akang'amua kuwa ametapeliwa baada ya kutomuona tena Lustig na kukosa mawasilino naye.

Baada ya kugundua ametapeliwa Andre alijisikia aibu kubwa kiasi kwamba mpaka akashindwa kwenda polisi kwa kuhofia kuchekwa na jamii kwa kufanywa mjinga kiasi hicho kununua mnara wa serikali ambao ndio kama kitambulisho cha jiji la Paris. Ingelikuwa hapa Tanzania tungesema ni sawa sawa na mtu akuuzie ile sanamu ya askari pale posta. Ilikuwa ni aibu kubwa.

Mtikisiko wa mfumo wa Kibenki Marekani..

Baada ya pilika pilika za huku na huko na kukoswa koswa kukamatwa nchini Ufaransa kwani aliuza tena kwa mara ya pili Eiffel Tower na bwana huyu aliyemuuzia Mara ya pili alipogundua ametapeliwa hakukaa kimya kama Andre yeye akaenda polisi hivyo ikamlazimu Lustig akimbie Ufaransa kuhofia kukamatwa.

Baada ya kurudi marekani Lustig akaanza tena kuhangaika ili apate channel nyingine ya kujiingizia pesa kwa njia haramu.

Moja ya matukio aliyoyanya ilikuwa ni kumtapeli 'Baba wa wahuni' (Gangster's Godfather) wa kipindi hicho aliyeitwa Al Capone. Lustig alimfuata Capone na kumuomba amuazime dola elfu hamsini akafanyie 'dili'.. Capone akampa hiyo hela. Lustig akaenda kuiweka hiyo fedha benki bila kuifanyia chochote kwa muda wa miezi miwili kisha akaitoa na kumrudishia Capone akimlalamikia kuwa biashara aliyoifanya imefeli.

Capone akafurahishwa sana na 'uaminifu' wa Lustig kwamba licha ya kupata hasara kwenye biashara yake lakini amejitahidi kumrudishia fedha yake yote. Kuonyesha furaha yake na kumpoza Lustig kwa biashara kufeli akampatia dola elfu tano pasipo kujua kuwa hili ndio lilikuwa lengo hasa la Lustig toka siku alipokuja kumuomba hela.

Tukio lingine lilikuwa ni pale ambapo Lustig alimuuzia Sheriff kutoka Texas 'mashine ya kuprint hela'. Miezi kadhaa baadae Sheriff akafanikiwa kumkamata Lustig. Lustig akamuambia Sheriff kuwa kama atakubali wayamalize wenyewe bila kwenda kwenye vyombo vya sheria yeye yuko tayari kumlipa hela yake mara mbili zaidi. Sheriff akakubali na Lustig akamlipa hela yake mara mbili.

Kesho yake Sheriff alipopeleka hela benki kuzihifadhi akaambiwa kuwa zile pesa ni bandia.

Baada purukushani za huku na kule za kutafuta chaneli nyingine ya 'biashara' hatimaye Lustig akawakusanya mkemia aliyeitwa Tim Shaw, pamoja mtu maarufu wa kugushi aliyeitwa William Watts na wakaunda matandao hatari wa kutengeneza noti za kugushi za dola za marekani.

Noti zao feki zilitengenezwa kwa umahiri wa hali ya juu kiasi ambacho hata tellers katika benki walishindwa kuzitofautisha na zile halisi.

'Biashara' hii ilimfanya Lustig kuwa milionea kwa haraka sana na akaishi maisha ya anasa. Na biashara hii ndio iliyomfanya asakamwe na serikali wakimuwinda kila kona wamkamate kwani noti zake bandia zilizagaa kiasi kwamba baadhi ya nchi zilianza kukataa kupokea dola kutoka marekani wakihofia kuwa zinaweza kuwa feki.

Taarifa za idara ya Huduma za Siri (Secret Service) ambayo iliundwa kipindi hicho kwa lengo kuu la kupambana na kutokomeza fedha bandia (walikuja kubadilishiwa majukumu miaka ya baadae na kupewa jukumu la kulinda viongozi wakuu wa nchi) taarifa hizo zinasema kwamba tatizo la fedha bandia za Bw. Lustig lilikuwa kubwa kiasi ambacho ilifikia hatua ilikuwa kana kwamba kuna 'serikali' nyingine ndani ya Marekani iliyokuwa inashindana na Serikali halali katika kuchapa noti za fedha. Hivyo basi kumkamata Lustig ikawa ni kipaumbele namba moja cha Secret Service.

Lustig alikuwa na hawara aliyeitwa Billy May, na Lustig alifanya kosa la kuanzisha mahusiano ya siri na msaidizi wa ndani wa Billy May aliyeiitwa Marie. Kutoka na uchungu wa kusalitiwa, mwanamama Billy May aliwasiliana na polisi na kuwaeleza Lustig alipo na hii ikafanikisha kukamatwa kwake.

Baada ya kukamatwa Lustig alipelekwa katika gereza lililopo Manhattan na akakaa hapo kwa wiki kadhaa kabla ya kuwatoroka kwa njia ambayo hwakutarajia.

Lustig alitumia mashuka katika selo yake kutengeneza kamba ndefu. Kisha akakata vyuma vya dirisha la selo yake (haijulikani alikataje) na akatumia kamba kushukia chini upande wa nje ya gereza. Kutokana na gereza kuwa karibu na barabara, Lustig alikuwa anashuka ukutani taratibu huku akizuga kusafisha vioo ili asitiliwe shaka ma wapita njia kwanini yuko juu ya ukuta.

Alishuka kwa mtindo huu taratibu taratibu huku akisimama kila mara kufuta vioo mpaka alipofika chini kisha akatokomea kusikojulikana.

Askari magereza walipokuja kukagua selo yake wakakuta amewaachia kipande cha karatasi chenye Ujumbe aliouandika kutoka katika kitabu cha Les Miserables. Ujumbe huo ulisema;

"Aliruhusu apelekwe katika ahadi; Jean Valjean alikuwa na ahadi. Hata kwa mfungwa, naam tena mahsusi kwa mfungwa. Inaweza kumpa mfungwa kujiamini na kumuongoza katika njia ya haki. Sheria haikuandikwa na Mungu na binadamu aweza kukosea."

Baada ya kutoroka ulianzishwa msako mkali na miezi michache baadae alikamatwa tena na safari hii bila kuchelewa alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kutokana na rekodi yake ya kutoroka akaamuliwa akatumikie kifungo katika gereza la Alcatraz. Gereza hili lilikuwa linaogopwa haswa kipindi hicho, lilikwa kama Guantanamo kutokana na mateso yake.

Gereza lilikuwa kisiwani, hivyo limezungukwa na maji pande zote hivyo hata mfungwa angesema atoroke asingeweza kuogelea mpaka kukutana na nchi kavu.

Lustig alifariki miaka michache baadae kutokana na baridi kali lililopitiliza katika gereza la Alcatraz ambalo lilimsababishia pneumonia kali.

Baada ya kifo chake, mchunguzi na mwanahistoria mashuhuri Tomas Andel alifanya kazi kubwa ya kwenda kupeleleza na kutafuta nyaraka katika nchi ya Austria-Hungary pamoja na nchi nyingine za jirani na baada ya uchunguzi wake wa muda mrefu akatoa sentesi moja tu ya kuhitimisha: hakuna mahali popote duniani kwenye nyaraka hata chembe inayothibitisha au kuonyesha kuwa Lustig alizaliwa hapo.

Badala ya majibu uchunguzi wa kufukua historia ya aisili ya Lustig unatoa maswali zaidi! Ina maana hakuzaliwa?? Kama alizaliwa je alizaliwa wapi??

Lakini ukweli wote ambao hakutaka kumwambia mtu yeyote alikufa nao yeye mwenyewe Victor Lustig, 'mpigaji' wa Daraja la Kwanza kuwahi kutokea katika historia.



Jiunge na Group langu la WhatsApp kusoma simulizi mpya kila siku. Kuna malipo ya 5,000/- kwa mwezi. Wasiliana nami 0759 181 457


The Bold.
 
The bold Unasema hiki ni kisa kidogo ulichoona bora ushee nasisi wakati ukiendelea kuandika story??????
My God,
leo nimeamini Dogo kwako ni kubwa kwa mwenzako,
lemme tell you that, Hii ni moja kati ya story nzuri zaidi ulizowahi kuandika,
Inaanza
D.B Cooper. Inafuata ya Osama, then inaweza kufata hii...
Big up,
congrats,
all the best
-stunter-
 
Nimetoa macho nimejitahidi kusoma nikajua kwa jinsi ninavyosoma kwa uelewa na haraka,nitakimaliza kukisoma hiki kisa,kumbe mh!,hata robo sijafika.
The bold, kwa usawa huu mtu akijitera si' wa kuacha, ni kupiga tu.
 
The bold tunashukuru kwa simulizi zako, za kusisimua. Wengi tunakusoma kimya kimya. Unajua unasimulia kipekee kabisa, mtu huchoki kusoma, ni kama JF yote iwe nisimulizi zako tu.
Jamaa sura yake tu inaonyesha ilikuwa ya kipigaji, sura ya kazi. Nimecheka sana alipowauzia watu wawili Eiffel Tower, umeifanya jumamosi iwe murua. Tunasubiria simulizi zaidi. Ubarikiwe...
 
duh! jamaa anatisha hawa ndo wanaweza hata kukuuzia nyumba yako mwenyewe!
hiki ni kipaji cha aina yake bila shaka jamaa alikuwa anauwezo wa kucheza na sura yake hasa macho... macho yanauwezo wakudanganya sana kwa mtu anaejua kujiset vyema,mtu unakutana na mtu unaemtapeli ana kwa ana na unamdanganya bila hata kukushtukia duh!
alikuwa anajua nini anafanya.
 
The bold Unasema hiki ni kisa kidogo ulichoona bora ushee nasisi wakati ukiendelea kuandika story??????
My God,
leo nimeamini Dogo kwako ni kubwa kwa mwenzako,
lemme tell you that, Hii ni moja kati ya story nzuri zaidi ulizowahi kuandika,
Inaanza
D.B Cooper. Inafuata ya Osama, then inaweza kufata hii...
Big up,
congrats,
all the best
-stunter-
Cooper mie mpaka leo huwa nairudia.
Afu najiuliza, alipotelea wapi?
 
I salute you The bold......jamaa mpk kumuuzia mtu mnara sio jambo Dogo, watu wa aina hiyo ni kama wanazaliwa na kitu cha ziada kichwani, mtu kama huyo hata akiwa na kiasi gani cha fedha kwenye account hatoacha upigaji kwa vyovyote vile.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom