Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Ina Maana Gani Kwako Kama Mwananchi?

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,372
8,108
Data-Protection-Act-2018.jpg


Hatimaye Tanzania imepata Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, sheria ambayo imekuwa ikipigiwa chapuo na wanaharakati wengi wa masuala ya haki za binadamu waliokuwa wanataka sheria hiyo iwepo ili taarifa binafsi za watu ziweze kuwa salama.

Mnamo Januari 31, 2023, Spika wa Bunge Tulia Ackson aliwaambia wabunge kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameusaini Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuwa sheria na hivyo sheria hiyo kuanza kutumika.

Lakini uwepo wa sheria hii una maana gani kwa mwananchi wa kawaida pamoja na taifa kwa ujumla?

Kufahamu hili na mengineyo kuhusu sheria hiyo, The Chanzo ilifanya mahojiano maalum na wakili Benedict Ishabakaki, ambaye ni mmoja kati ya watu waliondaa sheria ya mfano wa ulinzi wa taarifa binafsi kama sehemu ya harakati za kutaka Serikali ianzishe sheria hiyo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo yaliyofanyika Februari 1, 2023, na hapa Ishabakaki anaeleza hatua hiyo inamaanisha nini:

Benedict Ishabakaki: Kama mlivyosikia kwenye taarifa za Bunge hivi jana [Januari 31, 2023], Mheshimiwa Spika Dk Tulia [Ackson] ametoa ripoti kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania [Samia Suluhu Hassan] ameshasaini Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, sheria Namba 11 ya mwaka 2020 imesainiwa Disemba na amesema kwamba sheria imeshaanza kutumika.

Ni kweli sheria imesainiwa na hivi sasa tunasema imeanza kutumika. Lakini kwa mtu tu wa kawaida ajue kwamba hii sheria Namba 11 imeanzisha vitu vitatu. Imeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Kwa hiyo, kuna tume maalum ambayo imeanzishwa kama vile mmesikia baadhi ya tume mbalimbali.

Lakini pia [sheria hii] imeanzisha bodi ya haya mambo ya masuala ya taarifa binafsi na ulinzi na faragha ya watu. Lakini pia imesema lazima kutakuwa kuna mkurugenzi wa hiyo tume ambaye ataajiriwa ambaye ndiye atakuwa anafanya kazi za kila siku kwa siku.

Kwa hiyo, tunaona Mheshimiwa Rais kweli amesaini hiyo sheria, lakini bado hatujajua bodi kama imechaguliwa na pia hatujaona kama hiyo tume imeshaundwa kwa sababu kumbuka hiki ni chombo kipya na lazima kiwezeshwe.

Kwa hiyo, naweza nikasema sheria imeanza kazi lakini utekelezaji wake hatuwezi kusema kwamba tunaweza tukauona moja kwa moja kwa sababu mpaka hivi vyombo vitatu viweze kuundwa.

Yaani, bodi tujue ni kina nani kwa sababu kuna baadhi ya wajumbe wa bodi wanachaguliwa na Mheshimiwa Rais. Lakini pia mkurugenzi wa hiyo tume ambaye pia naye anateuliwa ama anaajiriwa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, sheria imeanza lakini bado kuna hivi vyombo ambavyo havijaundwa.

The Chanzo: Je, ni kwa namna gani sheria hii inafanya kazi?

Benedict Ishabakaki: Sasa kwa pamoja ni kwamba, pindi ambapo sasa bodi itaundwa na hii tume itaundwa na mkurugenzi atajiriwa, huyu mkurugenzi atakuwa na sekretarieti, au watumishi, ambao kazi yao ukisoma hii sheria imelazimisha wakusanya taarifa wote – hapa tunazungumzia makampuni ya simu, tunazungumzia mahospitali, tunazungumzia vyuo vikuu, labda maofisi kama ya kwetu – lazima wasajiliwe na hii tume.

Kwamba lazima uende ujisalimishe kwamba mimi ni mmoja wa wakusanya taarifa za watu ili uweze kusajiliwa. Lakini pia baada ya hapo sheria imetoa majukumu mbalimbali. Kwa mfano tu, ili iweze kwa mwananchi ambaye anaweza kuangalia, tumezoea kwamba kuna makampuni ambayo yanakuwa yanakusanya taarifa za watu, tuseme majina au jinsia ama tabia fulani, kisha anakuwa anazitoa kwa ajili ya tunasema kwa Kiingereza tunasema commercialization of data yaani kufanya kama biashara.

Kwa sheria hii sasa imenyima kutoa taarifa za Mtanzania yoyote nje ya nchi bila aidha ya ridhaa ya tume ama bila ya ridhaa ya mtu husika.

Kwa hiyo, hiki kilikuwa kilio cha wananchi na kilikuwa kilio pia cha wadau wengi. Kwamba nchi yetu imekuwa haina sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi. Na sasa hivi tayari sheria imekuja.

Kwa hiyo, nadhani ni wito tu kwa makampuni na wadau wengine sasa kujua kwamba taarifa yoyote ambayo unaikusanya ya mwananchi iwe ni jina, iwe ni namba ya simu ama ni kitu chochote ambacho kinahusiana na taarifa ya yule mtu lazima, ujue kwamba kuna sheria ambayo inamlinda endapo utatumia ile taarifa ndivyo sivyo, ama endapo utashindwa kutekeleza matakwa ya kisheria ambayo yapo kwenye ile sheria.

The Chanzo: Ni hatua gani sasa zinazozoweza kuchukuliwa endapo haki ya ulinzi wa taarifa binafsi itavunjwa?

Benedict Ishabakaki: Ukiangalia sheria jinsi ilivyo na kwa sababu tayari imeshatekelezwa, na bila shaka ukisoma sheria inasema kwamba itaanza kutumika pale ambapo kutakuwa kuna tunasema Gazeti la Serikali na tayari kuna Gazeti la Serikali ambalo lishachapisha hiyo sheria ikiwa na maana imeshaanza kutumika.

Kwa hiyo, ni kwamba mwananchi wa kawaida ambaye ataona kwamba haki zake, taarifa zake, labda zimefichuliwa ndivyo sivyo, ama kuna kampuni ilichukua taarifa kwa lengo fulani lakini imetumia kwa lengo lingine ambavyo sheria pia inanyima sasa, sasa hivi anaweza akachukua hatua za kisheria.

Baadhi ya hatua za kisheria jinsi ilivyo kwenye sheria hii ni, namba moja, unaweza ukatoa malalamiko kwenye tume, bahati mbaya, kama nilivyokwambia, bado tume hatujaijua ni akina nani.

Lakini pia unaweza ikawa ni jinai, Mwendesha Mashtaka wa Serikali yeye mwenyewe akaamua kufungua kosa la jinai endapo labda ataona kwamba kuna kampuni fulani imechukua taarifa za nchi au taarifa za wananchi imetoa nje ya mipaka ya nchi bila ridhaa ya tume au bila ridhaa ya mtoa taarifa.

Lakini pia [mwananchi] anaweza akaja kwa wanasheria, au akaenda kwa wanasheria wowote walipo, akaomba ushauri wa kisheria na akaweza kwenda mahakamani kushtaki kama taarifa zake zimekuwa zimevunjwa, ama haki yake imevunjwa.

The Chanzo: Kuna uhusiano gani kati ya sheria hii na kuongezeka kwa wawekezaji nchini?

Benedict Ishabakaki: Kwa hiyo, tuseme kwamba sasa hivi nchi hii ni salama kwa watu ambao taarifa zao zinachukuliwa. Lakini pia wawekezaji sasa nadhani wanaelewa kwamba sasa hivi sheria imeshakuja, kwa hiyo tutegemee pia wawekezaji kwa wingi kuja kwenye nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji.

Kimsingi, kwa sisi ambao tunafanya hizi kazi, na tuna wateja wengi wa kimataifa, moja ya maswali ambayo tunaulizwa wanasheria ni je, nchi yenu ina sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi?

Moja ni kwa sababu wawekezaji wanatoka katika mataifa tuseme ya Ulaya yanawalazimisha wao kuwa na viwango vya ubora ambavyo vinaendana na mikataba ya kimataifa ya kwao ya masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Lakini pili, kwa hiyo, ni kwamba ni viwango vya ubora vya kimataifa kwamba lazima kuwe na misingi na nyanja mbalimbali ambazo kampuni itafuata katika kuhakikisha kwamba inafanya biashara kwenye nchi fulani.

Kwa hiyo, ukiangalia, kwa mfano, nchi za Ulaya zinakuwa zinafungwa, kuna mikakati maalum ambayo unawekewa kwamba ukichukua taarifa ya mtu fulani itumie kwa ajili ya ile maana lakini pia jinsi ya kuzitoa hizo taarifa baada ya matumizi na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo, hili ni swali la kwanza ambalo wawekezaji wengi ambao wanataka kuja Tanzania huwa wanauliza je, nchi yenu ina sheria kama hiyo?

Lakini cha pili uhusiano ni kwamba, kama mnavyojua makampuni mengi siyo kampuni inaweza kuja kufanya kazi tu Tanzania. Inaweza ikawa na kampuni mama Kenya, inaweza ikawa na kampuni kaka Afrika Kusini au Marekani.

Sasa ile sheria ya nchi zao na ukiangalia viwango vya ubora wa sheria nyingi za kimataifa au za mataifa mengine ni kwamba unaruhusiwa kutoa taarifa kuzipeleka kwa nchi nyingine yenye sheria.

Kwa hiyo, tuseme kama unataka kuchukua taarifa za Tanzania za watu Tanzania kuzipeleka Kenya. Ukisoma moja ya vigezo ambavyo vipo kwenye sheria yetu sisi ni kwamba hizo taarifa zinapoenda kwenye hiyo nchi hiyo nchi lazima iwe na sheria [ya ulinzi wa taarifa binafsi].

Kwa hiyo, dhani kama una wawekezaji wanatoka Kenya, ama Afrika Kusini, wanaona ni ugumu sana kutoa taarifa zao kutoka kule kwa sababu unajua sasa hivi dunia imeenda kwenye tunasema big data, ni uchumi wa data, yaani taarifa nyingi nyingi sana wanazifanyia algorithm halafu wanafanya artificial intelligence.

Kwa hiyo, unakuta nchi, namaanisha yule mwekezaji ataogopa kuleta zile taarifa Tanzania kwa sababu ile nchi ya Tanzania haina sheria. Na ukisoma viwango vya ubora wa kimataifa inasema peleka taarifa pale ambapo hiyo nchi nayo inakuwa tayari lazima iwe na sheria.

Kwa hiyo, hicho pia ndiyo maana kimekuwa kilio cha wawekezaji wengi, au kilio cha watu wengi, kwamba tunataka Tanzania iwe na sheria ili waweze kufanya biashara yao kwenye au mazingira ambayo yaliyo salama.

Lakini sababu ya tatu ni kwamba wawekezaji wengi pia wanatafuta tunasema, yaani Kiswahili nashindwa kupata Kiswahili kizuri lakini tunasema uhakika wa biashara.

Siyo kwamba leo umekuja umechukua taarifa za watu tuseme labda unafanya kampuni ya kubashiri, umechukua taarifa za watu umezitumia vibaya kisha mtu anakuja kukushtaki labda kwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao au anakuja kukushtaki kwa sheria ya EPOCA, tunaita Electronic Postal Communication Act.

Yaani, [wawekezaji] wanataka kitu ambacho kwamba anajua kabisa kwamba ninaenda kuwekeza Tanzania na hizi data ambazo nitazichukua nitazitumia hivi kutokana na sheria inasema hivi.

Kwa hiyo, anakuwa kabisa ameenda kuwekeza kwenye nchi ambayo ina mazingira ambayo yanatabirika, unajua kabisa kwamba nikifanya hichi hichi ndiyo hichi. Kwa hiyo, hizo ndiyo sababu kuu tatu ambazo naona kwamba wawekezaji wanapenda kuja au kwenda kwenye nchi ambayo pia na yenyewe ina sheria kama hiyo.

Na kama mnavyojua sasa hivi karibu dunia nzima tupo kwenye uchumi wa dijitali na tunapozungumzia uchumi wa dijitali tunazungumzia taarifa, ama tunazungumzia data, na lazima tuwe na sheria ambazo inadhibiti hizo data, ama hizo taarifa.

Bila shaka kutokana na mabadiliko mengi ambayo yanakuja ya sheria pamoja na sheria hii tutegemee tutapata, bila shaka, wawekezaji wengi haswa kwenye wawekezaji ambao wanafanya mambo ya teknolojia.

Lakini pia na wawekezaji wengi ambao wanafuata ile miiko [au] viwango vya kimataifa ambayo inawalazimisha wao kuhakikisha kwamba wanatunza taarifa za watu na wanatunza usiri wa watu na faragha ya watu.

The Chanzo: Wewe kama miongoni mwa wadau walioshiriki kutengeneza muswada mbadala wa sheria hiyo, je, kile kilichopo kwenye sheria ndicho ambacho wadau mlipendekeza?

Benedict Ishabakaki: Kwa kifupi nimeshiriki kwenye mchakato wa, tuseme, wa kutengeneza mswada mbadala. Tulipewa hii kazi na watu wa asasi za kiraia bila shaka ikiwemo Jamii Forums, kwenye kutunga huu mswada. Siyo huu wa Serikali, ule mswada mbadala.

Ninaweza nikasema bila shaka kwa asilimia fulani Serikali tuishukuru imechukua maoni tuliyotoa japo kuna maoni mengine ambayo ni ya muhimu sana na ikipelekea hata tu leo mwenyewe kama mmemsikia Mheshimiwa Rais wa nchi anazungumzia kuhusu mfumo wa jinai au mfumo wa haki kwa Tanzania.

Mfano tu nikwambie baadhi ya vipengele ambavyo vimeachwa na sisi tulitegemea vingeweza kuingia ni vipengele ambavyo vinahusu na masuala ya jinai.

Tulikuwa tumezungumzia, tumechukua mfano mzuri wa sheria ya Afrika Kusini ambayo yenyewe inasema ukimtuhumu mtu na kosa fulani ambalo unahisi kwamba lazima utaenda kuchukua taarifa, kuna njia fulani ambayo inaundwa kwenye ile sheria ambayo itamlamzimu yule Askari wa Jeshi la Polisi apate ridhaa ya Mahakama kwenda kuchukua ile taarifa.

Kwa hapa nchini kwetu bado haijawa hivyo. Nadhani ndiyo maana unaona bado watu wanalalamikia mfumo wanalalamikia Jeshi la Polisi.

Lakini wangefuata ile sheria ya mfano ambayo tulikuwa tumeipendekeza ni kwamba utaenda mahakamani utaapa kiapo na utasema kwa nini unataka ile taarifa na utapewa kibali na Mahakama ndiyo unaweza ukaenda kuchukua.

Hiyo, itaondoa malalamiko kwamba afisa fulani wa polisi ameenda amechukua taarifa zangu labda kwenye kampuni ya simu bila ya kuwa na kibali. Hiyo tunaona kwenye sheria bado haijawepo.

Lakini pia sisi muswada tulikuwa tumesema angalau uwe na neno faragha kama nilivyowaambia mfano Kenya sheria yao inaitwa Data Protection and Privacy, yaani Sheria ya Ulinzi wa Taarifa na Faragha.

Baadhi ya nchi nyingi pia zimetumia neno sheria ya ulinzi wa taarifa na faragha, sisi tumetumia tu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi. Tulikuwa tumependekeza kwamba kuwe na neno faragha kwa sababu Ibara ya 16 [ya Katiba] inalinda usiri na faragha ya mtu.

Lakini pia kwa nchini kwetu Tanzania kama mmekumbuka miaka miwili iliyopita au mitano nyuma kulikuwa kuna sauti zinavuja, kuna watu wanalalamikia kwamba wanahisi mawasiliano yao yanakuwa yanaingiliwa.

Kwa hiyo, tulitegemea kwamba, tulikuwa tumeweka vifungu ambavyo vingeweza kuwa na ulinzi mzuri zaidi haswa mtu awe na amani kwamba ninavyoongea na simu na mtu mwingine ajue simu yake iko salama ama maongezi yake yako salama siyo leo na kesho utaona tena maongezi yake yanasambaa kwenye magroup ya WhatsApp.

Lakini bila shaka sheria siyo mbaya ni nzuri kwa kuanzia lakini nadhani labda kama hii tume ya Mama [Rais Samia] ambayo imeundwa kama itaenda kuangalia kwa kwenye mfumo jinai na kama na sisi bila shaka ni wadau tutaenda kutoa maoni tunaweza tukaangalia haya maoni.

Kwa sababu tatizo kubwa sana kwa hapa Tanzania limekuja kwa sisi ambao tunafanya hizi kazi za za makosa ya kimtandao na data unakuta tuseme kama umefanya kosa atakuja askari atachukua simu yako kukurudishia inaweza ikawa isiwepo au ikarudishwa baada ya miaka miwili.

Au akaja ofisini kwako umefanya kosa la kompyuta sheria inamtakia yeye akija ajikite kwenye lile kosa na siyo kuja kuchukua kompyuta isababishe wewe ushindwe kufanya kazi kabisa.

Na kama mmekumbuka Mheshimiwa Rais amesema angalau kuwe na mfumo ambao ukitoka kwenye ofisi, namaanisha mtu akiwa anahojiwa polisi, moja kwa moja ofisi ya DPP iwe inajua na hilo hilo kosa liende mahakamani.

Kwenye makosa, bahati nzuri nimebahatika kufanya kazi nyingi sana za sheria kwenye masuala ya kimtandao na hili suala la data. Unakuta mtu amekamatwa kwa kosa labda la kukashfu kitu fulani kwenye mtandao lakini akienda kufanyiwa upelelezi wakakuta labda simu yake ina mambo mengine wanaachana na lile kosa ambalo mtu alikuwa ametumiwa nalo la mara ya kwanza, wanabadilisha kesi, inakuja kesi nyingine na hicho ndiyo kitu ambacho Mheshimiwa Rais amesema tukiepuke.

Ikiwa na maana kwamba tungekuwa tuna sheria ile sheria ya mfano ambayo au ule mswada mbadala wa kwetu ungekuwa umechukuliwa kwa ukamilifu au moja kwa moja inategemea matatizo yangeweza kupungua.

Lakini mwisho wa siku kama ninavyozidi kusema siyo tu kuwa na sheria nzuri ama siyo tu kuwa na sheria nzuri au Katiba nzuri, mwisho wa siku ni watendaji.

Kwa hiyo, nadhani sheria hii imepita ni sawa lakini watendaji tuwafundishe labda maadili, au wafundishwe pia teknolojia waweze kujua pia kwamba unavyoenda kufanya uchunguzi kwa mtu ukichukua kompyuta atashindwa kuzalisha na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo, ni zaidi ya uadilifu, ni zaidi ya utendaji kazi ulio na unajua, ubunifu na vitu kama hivyo na siyo tuache ule ukiritimba wa zamani ya kufanya kazi.

Kimsingi ina athari kwa sababu unapoweka kwenye sheria, unajua hii ni sheria ambayo na nishukuru Bunge bila shaka na Serikali, Bunge kwa sababu wakati tulipendekeza kwamba hii sheria inabidi iwe inakuja kuwa juu ya sheria nyingine zote tunapohusiana na masuala ya taarifa binafsi na usiri na hiyo ndiyo imekuwa hivyo.

Sasa tatizo linakuja inapokuja kwenye suala la uchunguzi. Kama nilivyosema, ukiwa na mfumo wa jinai ambao haupo haupo sawa, itapelekea sasa leo hii badala wewe kuchunguzwa kuhusu kufanya jinai fulani,watu wataenda kuchunguza mahusiano yako na ndo maana umeona kuna malalamiko itatokea kuhusu uko kwenye mahusiano na mke wako lakini mke wako labda ameenda kwenye kampuni ya simu fulani amepata taarifa fulani.

Au upo kwenye hospitali fulani ambayo matibabu yako ni usiri lakini mtu fulani mwingine usikie anaanza kutangaza majibu yako. Ni kwa sababu kama tunakuwa hatuna mfumo wa uchunguzi ambao umetajwa kwenye sheria ina maana tunaachia Jeshi la Polisi, au vyombo vya ulinzi na usalama, mwanya mkubwa wa kutumia taarifa zetu wanavyotaka.

Lakini kungekuwa kuna mfumo ambao wanatumia taarifa lakini kunakuwa kuna mtu wa tatu ambaye anaangalia hii taarifa unayoenda kuichukua ni kwa ajili gani unachunguza nini? Nadhani ingepelekea tuwe na mfumo wa jinai ambao kidogo iko vizuri. Kwa hiyo, sheria hii bado ina mapungufu kwenye hilo suala la uchunguzi.

The Chanzo: Unadhani Watanzania wana uelewa kuhusiana na hii sheria?

Benedict Ishabakaki: Mimi kama mdau ninaweza nikasema kifupi sioni uelewa, ungeniambia nipime uelewa kwa sababu siyo tu wananchi hata sisi wanasheria wenyewe binafsi nimebahatika kuingia ndani zaidi na kusoma sana hizi sheria kwa sababu tulikuwa ni kazi ambayo tunafanya kama kampuni yetu ya sheria na pia ni eneo ambalo tunalifanyia kazi.

Lakini ni eneo ambao hata wanasheria wenyewe pia bado hawajawa na uelewa nao nadhani unaweza ukachukua ushahidi tu kwenye sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015 (Cybercrime Act) umeona malalamiko mengi ambayo yalikuwepo mpaka ikaenda bungeni pia ikarekebishwa kidogo.

Kwa hiyo, uelewa wa wananchi kuhusu makosa ya kimtandao ni mdogo sana lakini sasa unawaletea pia sheria nyingine ambayo ni ya masuala ya taarifa binafsi na ulinzi wa taarifa binafsi bado pia ni uelewa ni mdogo.

Kwa hiyo, moja ya kazi bila shaka ya tume kama itaundwa na Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba inatoa elimu kwa watu kujua taarifa binafsi ni nini, zinachukuliwa wakati gani, matumizi ya mtandao na vitu kama hivyo.

Kwa sababu, nikuambie tu pia kwamba kwenye sheria yenyewe imeanzisha wajibu, siyo haki tu, pia wewe una wajibu kama mwananchi. Siyo leo hii umepiga picha zako za uchi, umeweka kwenye mtandao, kesho unasema taarifa zangu zimetumika ndivyo sivyo.

Kwa hiyo, una wajibu pia kuhakikisha una password kwenye chombo chako unachotumia, kuhakikisha ni maudhui gani au ni taarifa gani ambazo unaziweka mtandaoni, kuhakikisha matumizi ya tovuti unazoingia je, unasoma vigezo na masharti na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo, tume imepewa kazi ya kuhakikisha kwamba wananchi wana uelewa wa hii sheria, wananchi wana uelewa na masuala ya taarifa. Na niseme tu siyo tume tu hata sisi wenyewe mawakili, nyie kama waandishi wa habari.

Kwa sababu unakuta ni teknolojia inakuja kwa kasi sana na Serikali pia imeshaingia kwenye masuala ya Serikali mtandao kwenye masuala ya kimfumo wa kidijitali, lakini uelewa unakuwa ni mdogo.

Na kumbuka sasa hivi kwenye maisha ya sasa hivi kwenye simu yako ndiyo kila kitu, ndiyo ina password yako, ina M-Pesa yako, ina Tigo-Pesa yako. Kwa hiyo, nadhani ingekuwa ni mimi ungeniuliza ningesema tuwajengee wananchi uwezo zaidi ili waweze kutambua hizi haki zao.

Lakini pia wajue kwamba wana wajibu kuhakikisha kwamba ni maudhui gani ambayo wanakuwa wanaweka kwenye mitandao.

Wito wangu kwa wananchi ni kuangalia matumizi sahihi ya mtandao kwa sababu ukiangalia asilimia, bila shaka taarifa binafsi siyo tu kwenye mtandao, tunazungumzia hata nje ya mtandao, yaani mfano kama nimekuja ofisini kwako, nikaandikisha kwenye daftari la wageni, au labda umeenda kwenye hoteli ukajiandikisha kwenye daftari la wageni, ile tayari ni taarifa binafsi.

Lakini kwa dunia ya sasa na kwa nchi yetu kama Tanzania taarifa binafsi ambayo tunazungumzia nyingi zinakuwa ni mtandaoni. Kwa hiyo, niwasihi tu wananchi kwamba wawe makini sana na matumizi ya mtandao.

Na bahati mbaya sana hili ninaomba iwe pia kwenye rekodi ni kwamba sisi kwenye muswada mbadala tulikuwa tumepitisha kitu kinaitwa yaani haki ya kusahaulika mtandaoni.

Lakini ni bahati mbaya kidogo sheria hii haijawa na hicho kipengele, sijakiona binafsi labda kama kimewekwa, lakini sijakiona. Bahati mbaya ni kwamba leo hii, mfano Benedict wa leo hii nimeposti picha fulani nikiwa chuo kikuu ama ndiyo naanza kazi ukumbuke baada ya miaka 30 ambapo labda nimekuja kuwa kwenye nafasi fulani ya juu au una kitu fulani ukumbuke ile picha haitakaa iweze kutoka mtandaoni.

Kwa hiyo, kama ulikuwa unapiga picha za zisizo na heshima, za utupu ni muda wa kujirekebisha kwa sababu bahati mbaya sana sheria yetu ya taarifa na ulinzi haijatoa haki yako ya wewe kwenda kumwambia mtoa huduma afute ile taarifa.

Kwa hiyo, haki ya kusahaulika bado. Wenzetu Ulaya unaweza ukaenda mahakamani, baadhi ya nchi nadhani kama Sweden, unaweza ukaenda mahakamani ukasema kwamba mimi taarifa hizi ni za zamani nilikuwa mtoto naomba uziondoe mtandaoni, inaitwa haki ya kusahaulika. Sisi bado hatuna hiyo.

Kwa hiyo, ni wananchi tu waangalie ni taarifa gani unazoeka kwenye mtandao, zina manufaa kwako lakini pia uwaze mbeleni na vitu kama hivyo.



THE CHANZO
 
Lakini pia [sheria hii] imeanzisha bodi ya haya mambo ya masuala ya taarifa binafsi na ulinzi na faragha ya watu. Lakini pia imesema lazima kutakuwa kuna mkurugenzi wa hiyo tume ambaye ataajiriwa ambaye ndiye atakuwa anafanya kazi za kila siku kwa siku.
Huyo anaweza kuwa kama wale wa NEMC, PCCB, LATRA nk malalamiko ya wananchi yanaingilia sikio la huku na kutokea sikio la pili
 
Back
Top Bottom