Sheria ya uchaguzi ni lazima ifanyiwe marekebisho-Tendwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Sheria ya uchaguzi ni lazima ifanyiwe marekebisho-Tendwa
Martha Mtangoo, Dodoma
Daily News; Wednesday,September 17, 2008 @00:03

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amesema sheria ya uchaguzi ni lazima ifanyiwe marekebisho ili suala la mgombea binafsi liingizwe katika sheria hiyo. Alitoa kauli hiyo kutokana na malalamiko kutoka kwa wenyeviti na makatibu wa vyama vya siasa nchini kudai kuwa serikali haina nia thabiti ya kuleta demokrasia ya kweli kuhusu suala la mgombea binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu mjini hapa jana, Tendwa alisema mgombea binafsi ni haki ya kidemokrasia na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu mgombea binafsi kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kuchaguliwa na kuchagua.

Alisema suala la mgombea binafsi haliathiri uchaguzi hata kidogo kwa kuwa tayari baadhi ya nchi wanachama wa Sadc wameshafanya uchaguzi huku wakiwa na wagombea binafsi. Msajili huyo alieleza kuwa haipendezi kila inapofika kipindi cha uchaguzi kesi kuhusu mgombea binafsi ndipo huanza kujitokeza, jambo ambalo mahakama imeliona na hivyo kulifanyia kazi.

"Mwanasheria Mkuu wa Serikali hajaenda kukata rufaa kwa ajili ya kupinga uchaguzi ninachojua mimi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kazi yake si kukata rufaa na kupinga maamuzi ya mahakama anachofanya yeye ni kuelekeza nini kifanyike ili suala la mgombea binafsi lifanyiwe kazi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema suala la mgombea binafsi ni haki ya mfumo wa vyama vingi na hivyo Serikali ya CCM inatakiwa kuonyesha nia ya kuleta demokrasia ya kweli. Kuhusu suala la Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mrema alisema ni bora iundwe tume huru kwa ajili ya kusimamia uchaguzi huo na si Tamisemi kama ilivyo.

"Unajua anayesimamia huu uchaguzi ni Ofisa Mtendaji ambaye pia ni mwajiriwa wa Serikali ya CCM, sasa matatizo yanapotokea, tunashindwa kujua tumshike nani shati,” alisema Mrema. Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Lwakatare alisema suala la mgombea binafsi linampa nafasi mtu wa chini anayefaa kusimamia maendeleo ambaye si mwanasiasa kuchaguliwa na kuwa kiongozi kwa kuwa kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya msingi.

Awali akifungua mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu wa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani, Waziri wa Tamisemi, Celina Kombani alisema serikali imepokea maoni 54 kutoka vyama vya siasa na wadau mbalimbali yakijikita katika maeneo mbalimbali likiwamo suala la mgombea binafsi na uchaguzi usimamiwe na Ofisi ya Waziri Mkuu.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom