SHERIA YA MATUMIZI YA PESA YAANZA RASMI;Mbunge agawa mchele, nyama kujipigia debe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

SHERIA YA MATUMIZI YA PESA YAANZA RASMI;Mbunge agawa mchele, nyama kujipigia debe

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by major mkandala, Mar 23, 2010.

 1. m

  major mkandala Member

  #1
  Mar 23, 2010
  Joined: Mar 6, 2010
  Messages: 74
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mbunge agawa mchele, nyama kujipigia debe[​IMG]Salim Said

  MBUNGE wa Jimbo la Wawi wilayani Chake, Hamad Rashid Mohamed (CUF) ameongeza changamoto katika udhibiti wa rushwa kwenye uchaguzi baada ya kugawa mchele, nyama na vifaa vingine vyenye thamani ya zaidi ya Sh1.5 milioni, akijitetea kuwa analindwa na sheria.

  Wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alisaini kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambayo inadhibiti matumizi ya fedha, lakini wakati maandalizi ya matumizi ya sheria hiyo yakiendelea, watu wanaotarajia kuwania ubunge wamekuwa wakilalamikia wabunge wanaoshikilia viti kwenye majimbo yao kuwa wanatoa rushwa za wazi kutokana na kulindwa na sheria.

  Hamad Rashid ameungana na wabunge wanaojitetea kuwa wanalindwa na sheria hiyo baada ya kufadhili sherehe iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwapongeza wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari ya Mwandani ambao walifaulu kwa asilimia 100 mtihani wa kidato cha pili na kuifanya shule hiyo kuwa ya kwanza kisiwani Pemba na ya pili kitaifa.

  Rashid pia ameshatoa misaada ya vifaa vya michezo kwa zaidi ya timu 30 za jimboni kwake ambazo ziko daraja la kwanza, pili na tatu.

  Kwa mujibu wa msaidizi wake wa karibu, miongoni mwa vifaa hivyo ni viatu, mipira, jezi na soksi.

  "Mkataba wangu ni wa miaka mitano... nimeomba tafsiri ya sheria kwa Mwanasheria Mkuu inayohusu rushwa katika kampeni na ameniambia ukomo wangu ni baada ya uteuzi, sasa wao wamelitoa wapi hilo," alisema alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kitendo chake cha kutoa misaada hiyo.

  Rashid alisema anawashangaa wananchi wanaohusisha misaada anayotoa na kujipigia debe kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, akisema kwamba sheria haimkatazi kuendelea na shughuli zake kama mbunge na kwamba anayo haki ya kufanya hivyo hadi pale shughuli za bunge zitakapokoma.

  Misaada hiyo imetolewa katika kipindi ambacho baadhi ya wananchi wa jimboni kwake, wamekuwa wakimlalamikia mbunge huyo kwa madai kuwa amelihama jimbo lake na kwamba, anaonekana wakati wa uchaguzi unapokaribia tu.

  Wananchi pia wanadai kuwa katika kuonyesha kuwa mbunge huyo haishi jimboni humo, hata gari lake la ubunge amelihamishia Tanzania Bara.

  “Angalia hivi sasa akija anatumia gari la Mbunge wa Konde, Dk Tarab Ali au la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Maalim Rashid Seif,” alisema mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

  Mwananchi ilishuhudia mbunge huyo akitumia gari na dereva wa mwakilishi wa Jimbo la Ziwani katika safari zake tangu juzi.

  Shamra shamra za shughuli ya kuwapongeza vijana hao zilianza mapema jana asubuhi wakati gari linalotumiwa na mbunge huyo lilipofika shuleni hapo na kushusha kilo zipatazo 45 za nyama, wakati mchele ulishatumwa tangu juzi.

  Shughuli hiyo ambayo mbunge huyo alikuwa mgeni rasmi ilipambwa na maulidi ya kumsalia Mtume Muhammad (S.A.W), dua na kufuatiwa na utenzi, risala na hotuba ya mgeni rasmi iliyoanzia saa 7:00 mchana.

  Akisoma utenzi wa hafla hiyo, mwanafunzi wa kidato cha tatu Asha Masoud alimpongeza mbunge huyo kwa kuisaidia shule hiyo, malori 13 ya mawe kwa ajili ya kujenga jengo jipya.

  Naye Mwalimu Hamad Kombo alimpongeza na kumsifu mbunge huyo kwa kuweza kufadhili shughuli yote ya kuwapongeza vijana hao.

  "Mheshimiwa tunakushukuru kwa kufadhili shughuli yote ya leo (jana). Hii si kwa kujionyesha kama una fedha nyingi, bali ni kwa imani, upendo na uchamungu wako. Tunamuomba Mungu akuzidishie... insha Allah," alisema Kombo katika risala yake kwa mgeni rasmi.

  Akijibu risala hizo kwenye hafla hiyo, Rashid alisema katika elimu hana masihara na kwamba hata kama ni kukopa popote, atafanya hivyo ili kufanikisha maendeleo ya elimu jimboni kwake.

  "Ombi langu kwenu, kama mwalimu mkuu alivyosema, muhakikishe nyote mnafika chuoni. Tumieni vizuri muda wenu, kuweni na nidhamu shuleni na nyumbani na mhakikishe kwamba masomo ya sayansi mnayapa kipaumbele," alisema Rashid.

  "Nitasaidia vitu na vifaa mbalimbali vya sayansi, kwa hiyo kama tulivyofanya kwa shule nyingine jimboni hapa. Pia naahidi kutoa kompyuta moja... mwalimu mkuu andika vifaa hivi naweza kuleta siku yoyote kuanzia sasa... katika elimu sina masihara, nitakopa popote.”

  Awali Rashid alisema amekuwa akisaidia jamii ya Jimbo la Wawi katika michezo, elimu na matatizo mengine ya kijamii.

  “Hivi sasa wazee wanacheka; timu za mpira zinacheka na shule wanafunzi si mnacheka jamani; mbunge wenu yupo safi, ataendelea kuwasaidia kwa hali na mali,” alisema Rashid.

  Mbunge huyo amepata upinzani mkali jimboni kwake baada ya watu watatu kutoka chama hicho kikuu cha upinzani visiwani hapa kuchukua fomu za kugombea ubunge wa jimbo hilo, jambo lililomfanya Rashid kupiga kambi kisiwani Pemba kwa ajili ya kuweka mambo sawa. Rashid ni katika wabunge waliopita kwa kura chache za maoni ndani ya vyama vyao katika uchaguzi wa 2005.
   
Loading...