Sheria ya Katazo la Utoaji Mimba Tanzania na uhalisia wa maisha mtaani

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Miaka inavyosogea ndivyo mabadiliko ya digitali yanazidi kushika kasi, mabadiliko hayo yanaenda sambamba na mabadiliko ya vyakula, vinywaji na dawa zinazotumiwa na binadamu.

Hivyo ndivyo ambavyo magonjwa yanayohusu afya ya uzazi yamekuwa yakiongezeka, hii ni kwa jinsia zote Wanaume na Wanawake.

Kwa tamaduni za Kitanzania miaka ya nyuma haikuwa kitu cha kawaida kuwa na mjadala au mijadala hadharani kuhusu masuala ya afya ya uzazi, lakini kwa sasa mambo yamebadilika, elimu imefika kwa wengi na suala la afya ya uzazi linachukuliwa kama suala lingine la afya.

Ukimya uliokuwepo ndio ambao ulichangia kuwe na ongezeko la watoa huduma wengi ‘feki’ wa dawa za nguvu za kiume, dawa za uzazi kwa wanawake na nyingine nyingi.

Mimba za utotoni.jpg

TANZANIA INATANUKA KATIKA ELIMU YA AFYA YA UZAZI
Tanzania haipo nyuma katika suala hilo ndio maana ilikubali kusaini Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu – Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika maarufu kwa jina la MKATABA WA MAPUTO.

Mkataba huo ulitungwa kuwa sehemu ya nyongeza ya Mkataba wa Haki za Binadamu na Watu wa Mwaka 1981.

Ujio wa nyongeza ya mkataba huo ulitokana na kuonekana kuna mambo yanakoseka kuhusu haki za Wanawake, ambapo ulisainiwa Julai 2003 na ukaanza kutumika mwaka 2005, lakini kwa Tanzania ulianza kutumika mwaka 2007.

IBARA YA 14 (2c) YA MKATABA WA MAPUTO
Kuna mengi ndani ya mkataba huo ambayo Tanzania imeyachukua na kuyatumia lakini kuna moja ambalo halijachukuliwa kwa ukubwa kama inavyotakiwa, suala hilo lipo katika IBARA YA 14 (2c).

Kipengele hicho kinahusu masuala ya afya ya uzazi hasa katika kutoa mwanya kwa Mwanamke kutolewa/kutoa mimba pale anapokabiliana na mazingira kadhaa ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwake.

UTOAJI MIMBA NI KOSA TANZANIA ISIPOKUWA…
Sheria za Tanzania zinaeleza kuwa utoaji mimba ni kosa lakini inaruhusiwa pale tu inapoonekana ujauzito unahatarisha afya au maisha ya mama.

Ndani ya MKATABA WA MAPUTO kuna vipengele vinavyotoa uwanja mpana wa mazingira ya utoaji mimba pale kunapokuwa na uhitaji huo, na baadhi ya Nchi ambazo nazo zimesaini mkataba huo zimechukua vipengele vingine kadhaa.

The Protocol to the African Charter on Human and Peoples’ Rights on the Rights of Women in Africa (the Maputo Protocol)
Under Article 14 (2) (c) of the Maputo Protocol, States Parties are called upon to take all appropriate measures to “protect the reproductive rights of women by authorizing medical abortion in cases of sexual assault, rape, incest, and where the continued pregnancy endangers the mental and physical health of the mother or the life of the mother or the foetus”.

Maputo saini.JPG

IBARA YA 14 YA MKATABA WA MAPUTO (2c) inatoa uwanja mpana wa kulinda haki ya afya ya uzazi kwa Wanawake, mfano wa baadhi ya ‘situation’ ambazo zimeruhusu mwanamke kutoa mimba mbali na suala la afya ya mwanamke:

~Unyanyasaji wa kingono
~Kufanya mapenzi na mtu wa ukoo
~Iwapo mimba inahatarisha akili au afya ya kiumbe cha tumboni


MIFANO YA SHERIA YA UTOAJI MIMBA
Rwanda
nao wamesaini mkataba huo, ambapo Sheria zao zinaruhusu Mwanamke kutoa mimba kukiwa na sababu za: Kubakwa, ndugu kujamiiana, ndoa ya kulazimishwa, ujauzito kuhatarisha afya.

Msumbiji Mwanamke anaruhusiwa kutoa mimba kwa ombi katika wiki 12 za kwanza za ujauzito, ruhusa nyingine ni katika kesi za ubakaji au kujamiiana ambapo utoaji mimba unaruhusiwa wiki 16 za kwanza, na kama kiumbe tumboni kina shida ya afya wiki 24 za kwanza.

Ndogo.JPG
NINI KINATOKEA TANZANIA?
Kutokana na Sheria yetu kutoa mwanya mmoja tu wa kumruhusu Mwanamke kutoa ujauzito, matokeo yake kumekuwa na matukio mengi ya utoaji mimba yanayodaiwa kutokea kinyume cha taratibu za kiafya.

Matukio ya aina hiyo yamesababisha madhara makubwa kwa kuwa mchakato unafanyika katika hali ya uficho, hivyo hata ufanisi wa utendaji wake unakuwa wa kiwango cha chini na matokeo wengi wameishia kupata matatizo ya kiafya na wengine kupoteza maisha.


MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA TANZANIA
Je, kwa mazingira hayo ya MKATABA WA MAPUTO, IBARA YA 14 2c inayobainisha mazingira yanayompa ruhusa Mwanamke kutoa mimba, Tanzania inatakiwa kuendelea kuishi katika ulimwengu wa sheria zilezile za kuruhusu kipengele kimoja tu cha kuruhusu utoaji mimba?

Vipi kama binti mdogo au mtu mzima kabakwa na kugundua amepata ujauzito baada ya muda?

Vipi kama aliyebakwa hana mpango wa kutunza ujauzito huo, aendelee nao?

Mfano Mwanamke hajabakwa lakini hana uwezo kiuchumi wa kuhudumia ujauzito na mtoto atakayezaliwa?

Vipi kama Mwanamke alifanya ngono na ndugu yake wa damu kisha akapata ujauzito, aendelee kuishi nao?

Vipi kama kondomu ilipasuka na akapata ujauzito lakini kutokana na mazingira hatakiwi kuwa mjamzito, ataendelea kulea mimba?

Vipi kama alifanya ngono kisha akatumia dawa za kuzuia ujauzito zikagoma? (kitaalum inawezekana dawa kutofanya kazi)

1600x960_464510-mtp-2021-abortion-law-women-gender1600.jpg

PICHA ZOTE: MTANDAONI
WADAU WATOA MAONI KUHUSU SHERIA ZA KATAZO LA UTOAJI MIMBA
Ni wazi kuwa jamii ya watu wengi Nchini haina uelewa mkubwa kuhusu Mkataba huo wa Maputo.

Nini maoni ya Wadau wenye nafasi katika jamii kuhusu IBARA YA 14 YA MKATABA WA MAPUTO 2c, Je, Tanzania iasili baadhi ya vifungu vya kipengele hivyo au iache kama ilivyo sasa ya kipengele kimoja tu?

NB: Kutakuwa na mwendelezo wa sehemu ya pili wa makala hii ambapo kutakuwa na maoni ya wadau wa Sheria, Haki za Binadamu, Madaktari, Waandishi wa Afya, Wananchi wa Kawaida na Tamko la Serikali…


Je, unadhani uhalisia upoje mtaani kuhusu utoaji mimba kinyume cha sheria na Serikali ifanye nini kusaidia Wanawake wanaopata ujauzito katika mazingira tata ikiwemo bila ridhaa yao?
 
Back
Top Bottom