Sheria ya Habari: Tamko la pamoja la taasisi zinazoshughulika na waandishi wa habari, Zanzibar

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
APRIL 25,2021

Ndugu waandishi wa habari,

Kama tunavyokumbuka hivi karibuni, Jumatano Aprili 21, 2021 mwandishi wa habari anayefanyia kazi zake Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) Zanzibar, Jesse Mikofu alishambuliwa na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Kadhia hiyo ilitokea baada ya Jesse kupiga picha tukio la askari waliokuwa kazini wakitekeleza jukumu lao la kuwahamisha wafanya biashara wadogo, maarufu Wamachinga, waliopanga bidhaa zao barabarani katika eneo la Darajani, wilaya ya mjini, Unguja.

Baadhi ya mashirika ya habari na vyombo vya habari vilielezwa kusikitishwa kwao na tukio hilo lililomfika mwandishi ambaye alikuwa akitimiza wajibu wake wa kazi wa kukusanya taarifa na kutoa kwa wananchi na hakuvunja sheria yeyote ya nchi bali alitekeleza matakwa ya kisheria na kijamii.

Wakati bado tasnia ya habari ina masikitiko makubwa kwa kutokea kwa tukio kama hili ambalo lilimuumiza mwandishi wa habari kimwili na kisaikolojia, tunapenda hata hivyo, kuchukua nafasi hii kuipongeza SMZ kwa namna ilivyohusika na taarifa hizo.

Mahsusi tunatoa pongezi zetu kwaWaziri wa Habari, Vijana, na Utamaduni Mh. Tabia Mwita na Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ Mh. Masoud Ali Mohamed kwa hatua ilizochukua ikiwemo ya kusikitikia tukio hilo na kuahidi kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya waliohusika na kitendo hicho.

Sisi Mashirika yanayohusika na waandishi wa habari, tumefarijika sana na hali hiyo ya kuonesha kuhusika tena kwa wakati muafaka na kwamba tunawatakia kheri Mawaziri hao katika kuchukua hatua hizo ili kudumisha utawala wa sheria na pia kuhakikisha uhuru wa waandishi wa habari kufanya kazi zao kama watu wa kada nyengine bila ya vikwazo visivyokuwa na ulazima wowote.

Iliripotiwa kuwa Mwandishi Jesse alikamatwa, alipigwa, alijeruhiwa, alilazimishwa kugaragara katika dimbwi la maji machafu na simu yake kuharibiwa licha ya kuwa aliweza kujieleza kuwa yeye ni mwandishi wa habari na kuonesha vitambulisho vyake vyote.

Waandishi wameumizwa sana na kadhia hii na kuchukulia kuwa madhila haya yanaweza kumkuta mwandishi yeyote wa habari ikiwa matukio kama yataendelea kutokea hasa kwa vile umuhimu wa habari katika jamii, katika kukuza na kuendeleza demokrasi na utawala bora. Habari ndizo zinazounganisha wananchi na viongozi wao, zinachochea uwazi na uwajibikaji na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo katika nchi yeyote.

Sambamba na kauli ya Waziri husika kulishughulikia suala hili tunapenda kushauri Serikali kuweka mazingira mazuri ya utoaji na upokeaji wa habari ikiwemo kutumia fursa ya kuandaa sheria nzuri ambayo itatoa nafasi kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kama wataalamu na bila kupata mateso wala manyanyaso yeyote.

Bahati nzuri SMZ imeandaa mswada wa sheria wa habari ambao utabadilisha sheria zilizopo, hivyo tunashauri Serikali kuliangalia hili kama ni somo na hivyo kupata sheria ambayo itakuwa ni nzuri zaidi na kunufaisha siyo tu waandishi wa habari lakini pia Zanzibar kama nchi kutokana na kuwekwa kwa mazingira mazuri ya uwandishi wa habari nchini.

Tunaamini kuwa hatua dhidi ya wakosaji ni muhimu kuchukuliwa lakini zinahitaji kufuatana na sheria na taasisi imara ili kuhakikishwa kuwa masuala hayo hayajitokezi tena katika utawala huu na tawala nyengine zote zitakazokuja. Sheria zilizopo hivi sasa kama ilivyoonekana zimepitwa na wakati lakini pia hazitowi mazingira mazuri na mapana kwa waandishi wa habari kufanya kazi kwa ufanisi.

Na sisi mashirika yanayoshughulika na habari tupo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa tunaandaa sheria nzuri itakayofanikisha malengo hayo ya kihabari na pia malengo ya Serikali katika kuleta ustawi wa nchi.
Uhuru wa habari umetambulika kimataifa, kikanda na kinchi na hivyo ni vizuri kuhakikisha unatolewa na unalindwa kwa hali zote.

Katiba ya Zanzibar kifungu cha 18 (1) kinaeleza kuwa “bila ya kuathiri sharia za nchi, kila mtu ana haki ya kutoa maoni na kujieleza; na uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza habari na mawazo kupitia chombo chochote cha habari bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana haki ya uhuru wa kutoingiliwa mawasiliano yake”.

Without prejudice to the relevant laws of the land, every The person has the right to freedom of opinion and expression, and to freedom of seek, receive and impart or disseminate information and ideas through expression any media regardless of national frontiers and also has the right of freedom from interference with his communications.

Sehemu ya pili ya kifungu cha 18 kinatoa uhakika wa kila mwananchi kuwa na haki ya kupashwa habari kwa matukio mbali mbali yanayotokea nchini na duniani kwa jumla. Kwa hivyo, haki ya kupata habari ni haki ya msingi kwa mwananchi na kwamba mtoaji wa habari hapaswi kunyanyaswa bali anapaswa kupewa mashirikiano anayostahiki.

Tamko la Misingi ya uhuru wa kujieleza la Afrika, lililopitishwa Gambia mwaka 2002 linasema katika kifungu cha pili kuwa (1) kuwa hakuna mtu atakayeingiliwa uhuru wake wa kujieleza na kifungu kidogo cha pili kuwa vikwazo vyovyote vya uhuru wa kujieleza vitatolewa na sheria na vithibitishwe kuwa vina uhalali na ulazima.

1.No one shall be subject to arbitrary interference with his or her freedom of expression.
2. Any restrictions on freedom of expression shall be provided by law, serve a legitimate interest and be necessary and in a democratic society.

Hivyo, tunaiomba Serikali kupitia upya mswaada wa sheria wa habari ili kuhakikisha kuwa inaondosha alama zote za ubinyaji wa uhuru wa waandishi kufanya kazi zao na kwamba unalenga kutimiza matakwa ya kikatiba ya nchi na misingi ya uhuru wa habari ya kikanda na kimataifa.

kuwepo kwa uhuru wa habari kutaongeza kiwango cha demokrasia, uwazi na , uwajibikaji, maendeleo na ukuwaji wa uchumi kwa vile waandishi wengi watajituma kuwa wabunifu zaidi na pia kutaweza kuvutia wawekezaji wengi katika sekta ya habari na sekta nyengine za kimaendeleo.
Mashirika yaliyohusika ni:

Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar (MCT Zanzibar )
Jumuiya ya waandishi wa habari za maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)
Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC)
Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC)
Chama cha waandishi wa habari wanawake Zanzibar (TAMWA ZNZ)


Dk Mzuri Issa
Mkurugenzi
TAMWA,ZNZ
 
Back
Top Bottom