Sheria mpya ya Vizazi, ndoa yaja

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,491
54,884
SERIKALI kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) inakamilisha mchakato wa kuwa na sheria mpya, itakayoendana na mabadiliko yanayotokea na kurahisisha na kuhamasisha usajili wa takwimu za matukio ya vizazi, vifo, ndoa na talaka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Kabla ya hapo, muswada utawasilishwa bungeni ili sheria hiyo ipitishwe na baada ya hapo tuwe na sheria mpya. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, iliyohusu maboresho ya Mfumo wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Ukusanyaji wa Takwimu (CRVS) iliyofanyika mkoani Morogoro jana.

Profesa Kabudi alisema hali ya usajili na takwimu za matukio ya vizazi, vifo na sababu zake, ndoa na talaka sio nzuri, kwani idadi kubwa ya wananchi wamekuwa hawasajili matukio hayo yanapotokea, japo wengi wamekuwa na nia ya kufanya hivyo, lakini wameshindwa kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema wananchi wengi wamezaliwa na kufariki bila ya kuwepo kwenye kumbukumbu zao za matukio muhimu katika mfumo wa usajili wa kiserikali. “Wananchi hawa wanaishi lakini hawaonekani katika picha kubwa ya taifa inayochorwa kwa kutumia takwimu na sababu kuu ya kwa nini hawaonekani ni kwamba hawakusajiliwa wakati walipozaliwa,” alieleza Profesa Kabudi.

Aliongeza kuwa kumekuwepo na sababu mbalimbali, zinazochangia hali hiyo nchini na kati ya hizo ni umbali uliopo kutoka kwenye vituo vya tiba, ambapo usajili wa vizazi hufanyika kwa mtoto anapozaliwa.

Alisema wazazi hulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda eneo la kuwasilisha maombi ya kumpatia mtoto cheti cha kuzaliwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Hivyo alisema kutokana na changamoto hizo, wananchi wengi wamelazimika kutowasajili watoto wao na hivyo kuongeza mlundikano wa wananchi wasio na vyeti vya kuzaliwa nchini.

Pamoja na hayo, alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, zilionesha kuwa asilimia 13.4 ya wananchi ndio wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Alisema hiyo ni idadi ndogo na ni kiashiria kuwa serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi.

Alieleza kuwa serikali kwa kulitambua tatizo hilo, tayari imeanza kuchukua hatua kwa kufanya maboresho ya mfumo wa usajili uliopo na kuanzisha mfumo utakaofanya kazi vizuri ili kusajili matukio muhimu ya binadamu na takwimu (CRVS).

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Profesa Hamis Dihenga kabla ya kumkaribisha waziri kufungua semina hiyo, alisema Rita ina wajibu wa kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kusajiliwa ili nchi iwe na idadi kamili ya watu wake kwani kwa sasa asilimia 87 ya Watanzania hawajasajiliwa na hiyo ni idadi kubwa.

Profesa Dihenga alisema ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anakuwa na taarifa zake kikamilifu; hivyo alisema elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa wananchi na kuelezea pia changamoto za mfumo na sheria zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikichangia kukwama kufikiwa kwa baadhi ya mambo

Chanzo: Habari leo
 
Blaaa blaaa hiyo mi sitaki kusikia
July hiyo hapo tuanzie na marupurupu tuliyoahidiwa
 
Back
Top Bottom