Sherehe za Uhuru wa Tanganyika: Unasherehekea kama Raia Daraja la kwanza au kama “Div. 5”?- Tafakari

Jan 8, 2013
20
8

KWELI Tunasherehekea siku ya uhuru wa Tanganyika. Mimi pamoja na maccm wote tumeungana kwa pamoja. Hata na wewe unayedhani husherehekei tumekulazimisha kusherehekea nasi iwe ni kuadhimisha machungu ya zaidi ya miaka hamsini ya utawala wa mkoloni mweusi au hata kusherehekea jinsi mkoloni mweusi anavyokukumbuka hata kwa kukupa makombo na kukudanganya kuwa mpo pamoja ila kumbe ni kama mashariki ilivyo mbali na magharibi. Mimi kwa upande wangu pia ninasherehekea kwa kutafakari madhila yasababishwayo na mkoloni mweusi hata kufikia kuwa na raia wa daraja la kwanza na raia wa daraja la tano (Div.5!) katika nchi yake! Unashangaa nini kusikia kuwepo kwa raia daraja la kwanza?
Hebu kumbuka umesahau kuwa kuna daraja la kwanza la Watanganyika ambao wao wakiugua wanapaswa kupelekwa Afrika Kusini? Huenda hakuna sababu nzuri zaidi ya kusema kwamba hao ni raia wa daraja la kwanza. Ninaamini kwamba hali hii tumeilea na kuiruhusu wenyewe yaani mimi pamoja na wewe iwe ni raia wa daraja la kwanza au daraja la tano. Hapa ndipo msingi wa mimi na wewe tuamue kwa sauti moja kuhakikisha kuwa kiongozi yeyote wa kiserikali au anayotokana na kuchaguliwa na wananchi tuhakikishe kwa sauti moja asiwepo wa kupelekwa kutibiwa Afrika ya Kusini. Kila mmoja awe tayari kufa au kupona kwa” utekelezaji wa kishindo katika uboreshaji wa sekta ya afya uliofanywa na chama tawala”
Hivi inaingia akilini wale tuliowapa jukumu la kuboresha huduma za afya ndio tuwakimbizao kwenda Afrika ya Kusini. Halafu hao hao ndio wanatuambia huduma za afya zimekuwa ni bora sana hapa nchini., Hivi kweli tuwaamini? Hawa ni sawa na mtu anayekuambia hii sumu ni tamu sana wewe ile au inywe huitapata madhara ila ukimwambia aionje anakataa kwa nguvu zote. Sasa tumeamka na unapaswa kuamka kuwa unaweza kuitumia siku hii ya uhuru kuanza upya katika kuhakikisha asiwepo raia wa daraja la kwanza kwa upande mmoja na wengine wa madaraja mengine.
Imani yangu ni kwamba hawa tuliowapa dhamana wakifa pale Muhimbili kwa Umeme kukatika au kukosekana kwa vipimo sahihi na hivyo kupasuliwa kichwa badala ya mguu nauhakika kuwa wataamka na kuhakikisha madhila haya tuyapitiayo sisi wapiga kura yataisha kwa uhakika.
Ukitaka kujua kuna raia wa madaraja mbalimbali wewe tembelea hospitali yeyote ya serikali kuanzia ile ya wilaya utashuhudia nikisemacho. Kuna wale wa kina sie wa daraja la tano wodini tumejaa mpaka sakafuni. Kimsingi katika vitanda kuna wagonjwa kuanzia wawili hadi watatu. Wamama waliojifungua wanawekwa wawili katika vitanda na vitoto vyao! Hivi hawa tuliowapa dhamana watakubali wake zao na dada zao walazwe kitanda kimoja na mgonjwa mwingine ambaye hata hujui anaumwa nini? Hebu piga picha ya mke wa kiongozi yeyote analazwa kitanda kimoja na mtanganyika masikini alipindukia kama hataanza kutapika unadhani ni nini kitafuatia?
Ili kuwadanganya wasomi wetu wenye uwezo wa kusema na kwa hakika wameamua kuwa “mabubu” nao katika hospitali hizi za wilaya hadi taifa zimeanzishwa wodi za madaraja ya juu tofauti na kule “Kajambanane” nao wanasherehekea mimi ni mtu mkubwa nimepewa chumba cha peke yangu! Huo ni upuuzi kuendelea kuuvumilia kwa sababu mwisho wa siku wapo wa kupelekwa Afrika Kusini wakafie au kurudi wakiwa hai huko na wapo ambao wanapaswa kufia Muhimbili. Kwa hakika kama tunaona kuna haja ya kila mgonjwa kuwa na chumba chake iwe hivyo kwa hospitali za serikali. Kama tunaridhika kulala wawili hadi watatu katika hosipitali iwe hivyo kwa kila mmoja.
Madaktari walilisema hili, ila propaganda za TBC zikatufanya tuamini kuwa walikuwa wanataka maslahi yao tu yawe bora! Mimi ninayesema haya sio daktari na siwezi kuwa kwa sababu shule niliyosoma hatukuwa na mwalimu wa fizikia, baiolojia, wala Kemia. Hivyo mtihani wa mwisho nilipata F zote tatu kwa kipindi kile walisema kuwa nilifeli ila katika zama hizi za Mulugo unaweza kusema kuwa nilifaulu ila kwa ufaulu hafifu tu. Ninakushukuru Mulugo kwa hilo kwa kuwakosoa watangulizi wako walionionea. Nirudi katika mada kiukweli ni kwamba mimi na wewe ambao kimbilio letu ni katika hospitali hizi za serikali tunajua hali mbaya iliyopo lakini si kwamba ipo juu ya uwezo wetu bali tumeruhusu tuliowapa mamlaka ya kusimamia na kuamua matumizi ya kodi zetu wawe na nafasi ya kwenda kutibiwa Afrika ya kusini wao pamoja na yeyote wanayeona wakimpeleka Afrika ya kusini vyombo vya habari vitaonesha wema wa serikali katika kujali watu wake wakienda kufa wakipata matibabu Afrika ya Kusini.
Ninasema wanapelekwa kwenda kufia Afrika ya Kusini kwa sababu wakati mwingine wanapatwa na matatizo ghafula na ni lazima upate huduma bora kabla ya kwenda nje kwa matibabu zaidi. Ni hapa majuzi tu gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa Mtanganyika aliyehitajika sana kutokana na elimu yake na uadilifu wake katika kulitumikia taifa alipoteza maisha kutokana na kutokupewa huduma sahihi katika hospitali ya taifa muhimbili. Hiyo ni ripoti ya madaktari bingwa wa hospitali iliyopewa kandarasi ya kuhudumia raia wote wa daraja la kwanza Tanganyika pamoja na raia wengine wote watakaoteuliwa kupelekwa huko ikionekana wanaweza kusaidia kuonesha kwa Watanganyika wa daraja la tano kuwa serikali yao inajali sana raia wake hata kama watalala wawili hadi watatu katika kitanda kimoja wodini au hata sakafuni na ikibidi kuombwa kwenda na godoro lako ni kutokana tu na utendaji mbovu wa wawtu wa chini! Yaani eti hawatoi taarifa sahihi ndipo pale huwa tunasisisitiza “raisi anashauriwa vibaya” au “ wasaidizi wanamuangusha raisi”
Ombi langu kwako hebu katika siku hii ya kusherehekea uhuru wa Tanganyika hebu tuwalazimishe hawa ndugu wawe tayari kufia nyumbani au katika hospitali ya taifa kama ambavyo Mandela alivyokufa kwa amani nyumbani kwake. Hili jambo linawezekana. Huo ndio uwe uzalendo kwa viongozi wetu. Asiwepo wa kwenda hospitali ya binafsi huko tuwaachie watanganyika hususani wafanyabiashara, wakulima wakubwa, na wajasiriamali waliopiga hatua. Viongozi wetu pamoja na wake zao na ndugu zao ambao hata wakifa tuwe na uhakika kabisa nao watapata uchungu mkubwa sana!
Sarakasi Zilezile katika Elimu!
Kwa sababu mimi mwenyewe ni mwalimu ninasita kuliongelea tatizo linalofanana na katika sekta ya afya. Huenda wakadhani ninasema haya kwa kutafuta maslahi ya walimu ili wameemeke. Ila ukweli ni kwamba walimu tuna hali ngumu sana tuliopo katika shule za serikali. Siku hizi wanafunzi tunaowafundisha ni wa watoto wa masikini tu wanaoandaliwa vema kuja kuwa wapiga kura watiifu kwa watoto waliosomea huko mnakokujua. Tumekumbuka sana na sisi kufundisha watoto wa wakubwa kama tulivyosoma pamoja na watoto wa wakubwa hapo zamani kama ilivyokuwa kwa wale wa Nyerere. Ni aibu kukuta hata mh. Dkt. Shukuru Kawambwa na naibu wake Profesa Mulugo watoto wao hawasomi katika hizi shule tunazozifundisha kwa kisingizio kuwa hazina ubora! Hivi hii kweli ni sawa ndugu zangu? Kwa hiyo huku tunakofundisha hawana mpango kabisa wa kutengeneza ubora zaidi ya “BIG RESULT NOW? Ila nawashukuru kwa mpango huo kabambe kwa sababu masomo yote ya sayansi niliyofeli zamani sasa hivi ninaufaulu hafifu ila nimefaulu. Hatutaki kuandaa kundi la watanganyika wataopigiwa kura na wale watakaopiga tu kura katika maisha yao yote! Siku hii ya Uhuru ninaomba tutafakari mambo haya mawili!
ANGALIZO
Ninaweka angalizo tu kwamba nisichukuliwe tu kuwa mimi ni mtu nisyetaka kuona maendeleo yaliyofikiwa na Tanganyika yetu. Tanganyika tuitazame kama mtoto aliyedumaa baada ya kulelewa na mama wa kambo yaani CCM baada ya kifo cha mama yake ambaye ni TANU. Hivi kama unalea mtoto akawa anaonesha hatua zote za ukuaji halafu punde anaanza kusuasua halafu majirani na matabibu wanapokuambia mtoto wako anamatatizo, je itakuwa ni busara kuwaambia kuwa wanawivu wa “kike” tu au wana roho ya kwa nini kwa sababu tu eti wanakuambia kuwa mtoto wako katika muda huu alipaswa kuwa na uwezo wa kula mwenyewe, kuzungumza, kucheza na wenzake kwa kujitegemea? Tanganyika ni mtoto asiye “mlemavu” alipaswa katika miaka hii 52 kuwa na uwezo wa kula mwenyewe sio kuendelea kulishwa, alipaswa kuwa amevuka hatua ya kukaa mwenyewe na kutambaa. Alipaswa kuwa ameweza kusimama na awe na uwezo wa kupiga hatua hata kama sio kukimbia. Pamoja na hayo tunamshukuru Mama wa kambo (ccm) walau hajaamua kumuua kabisa huyu mtoto Tanganyika ni matumaini yetu kuwa Watanganyika wenyewe watakuwa tayari kuzikwepa hila za dhahama za huyu “mama wa kambo” Tuungane kwa pamoja kwa ustawi wa Tanganyika ili iwe mahali salama pa kuishi hadi kifo!
 
Back
Top Bottom