Sheikh Yahya usiigeuze Ikulu hekalu la wapiga ramli! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Sheikh Yahya usiigeuze Ikulu hekalu la wapiga ramli!

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by asha ngedere, Sep 13, 2010.

 1. a

  asha ngedere Member

  #1
  Sep 13, 2010
  Joined: Nov 6, 2009
  Messages: 92
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Sheikh Yahya usiigeuze Ikulu hekalu la wapiga ramli!
  * Kama ni uhuru, sasa anautumia vibaya
  * Serikali haiongozwi kwa ushirikina

  Na Daniel Mbega

  BADO Watanzania tunajiuliza kuhusu kitendo cha baadhi ya viongozi wetu kuigeuza Ikulu, sehemu takatifu kama inavyojulikana na kusisitizwa na Mwalimu Julius Nyerere kuwa mahali pa biashara.

  Bado tungali tunakumbuka namna Ikulu ilivyotumiwa na baadhi ya viongozi kujilimbikizia mali za umma kwa faida yao, huku Watanzania wakiendelea kupiga miayo na kuogelea kwenye lindi la umaskini.

  Lakini wakati wananchi wakiomba Mungu apishilie mbali mabaa yote yaliyotokea kwenye ‘Nyumba Takatifu’, sasa yameibuka mengine, makubwa zaidi kuliko yale ya awali.

  Haya sasa yanatisha kwa sababu yanahusisha masuala ya ushirikina, tena ule wa kutisha, ambayo yamewafanya Watanzania wote washtuke na kushangaa kuona kama Tanzania sasa inaongozwa kwa nguvu za wachawi, wapiga ramli na watabiri wa nyota!

  Awali mtabiri ‘maarufu’ wa nyota, Sheikh Yahya Hussein, alitabiri mwishoni mwa mwaka 2009 kwamba Rais Jakaya Kikwete angepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kwamba atakayejitokeza kumpinga kiongozi huyo ndani ya chama chake cha CCM katika kuwania nafasi hiyo, angekufa ghafla.

  Alijtokeza Magale John Shibuda kutaka kuwania nafasi hiyo huku akipinga kwamba hayo ni mambo ya kishirikina tu. Hata hivyo, dakika za mwisho aliamua kumuunga mkono Kikwete na hakuna mwingine tena aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM.

  Kwa kiasi kikubwa, tishio la Sheikh Yahya lilikuwa na nguvu kwa sababu siyo wote waliokuwa na ujasiri wa kujitokeza tena baada ya tamko lake, hivyo Kikwete akapita kiulaini bila kupingwa.

  Hii ni kwa sababu Sheikh Yahya alikwenda mbali zaidi wakati aliposema kwamba kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Lawrence Gama, mwaka huo ilikuwa ni ishara ya ushindi mkubwa wa Rais Kikwete katika kura za maoni na kupata tiketi ya CCM, ili kugombea urais katika muhula wa pili.

  Alisema njia ilikuwa nyeupe kwa Rais Kikwete kuingia tena Ikulu na kwamba wale watakaoshindana naye, watasambaratika kwa sababu uongozi wa Kikwete ni urithi kutoka kwa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.


  "Kwa hiyo Kikwete alirithi urais huu kutoka kwa Nyerere. Ngoja awamu ijayo, mwachie Mkapa, kauli hiyo bado haijafutwa kwani mirathi kutoka kwa mwalimu ni ya awamu mbili," alisema Sheikh Yahya.

  Hakusema watakaojitokeza watakufa ghafla kwa “staili” gani? wangekufa kwa sumu, kwa kugongwa na gari, kupigwa risasi, kwa kumwagiwa tindikali au watakufa kwa ugonjwa? Kwa mtazamo wa kawaida, utabiri huo unaua demokrasia ya kweli na dhana zima ya utawala bora kwa kumfanya mtu aliyepo madarakani asipingwe hadi amalize kipindi cha miaka kumi.

  Utabiri wa aina hii haufai kwa vile unamfanya Rais aliyepo madarakani ajisahau akijua hawezi kupata mpinzani mpaka amalize muda wake wa uongozi. Nchi yetu haiwezi kuendeshwa kwa utabiri wala ndoto.

  Wanaoamini masuala ya unajimu waliamini pia hata unajimu wake wa awali kwamba kungetokea kwa kifo cha kiongozi mmoja wa zamani wa kitaifa katika kipindi cha kati ya Desemba na Aprili 2010.

  Wale wanaoishi kwa Imani ya Kweli ya Mungu walimpuuza na kusema kauli hizo hazina tofauti na zile za wapiga ramli kama wa enzi za utawala wa Mfalme Nebkadreza wa Babeli aliyetegemea kila ndoto anayoota itafsiriwe na wachawi na waganga na wapiga madogoli lakini akashangazwa na uwezo wa Mungu aliye Hai uliokuwa ndani ya Nabii Daniel, ambaye yeye alimwita Belteshazar.

  Wakati hayo yakingali yanaelea kwenye fikra za Watanzania, huku kukiwa hakuna tamko lolote la Serikali ambayo inadai haiamini masuala ya uchawi na ushirikina. Sheikh Yahya ameibuka tena Alhamisi iliyopita, yaani Septemba 9, 2010 na kuingiza ushirikina kwenye uchaguzi mkuu ambapo amesema kuwa utatawaliwa na mambo ya giza.

  Sheikh Yahya amekwenda mbali zaidi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwa kutangaza kwamba atatoa ulinzi usioonekana kwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, huku akihusisha kupatwa kwa jua, mwezi Juni 2010 kama ishara ya watu wengi kutumia nguvu za giza kushinda uchaguzi mwaka huu.

  Katika uzushi huo wa kishirikina, Sheikh Yahya alioanisha “kuchezeana” na tukio lililompata Rais Kikwete wakati akihutubia mkutano wa kampeni Agosti 21, mwaka huu katika Viwanja vya Jangwani, hivyo akasema kutokana na matukio hayo, atatoa ulinzi usioonekana kwa macho, kumkinga Rais Kikwete, ili mtu yeyote asijaribu kumfanyia mchezo wowote kama ilivyotokea Jangwani.

  “Mtu yeyote asijaribu kumfanyia mchezo wowote kama ule wa Jangwani kwa sabababu litakalomkuta atajua mwenyewe,” alionya katika taarifa hiyo ya ukurasa mmoja kuwa amefikia hatua hiyo kutokana na uchungu alionao kwa nchi na kwa Rais Kikwete anayempenda.
  Labda niulize tu, je, hivi tumefikia hatua ya Serikali yetu kuongozwa kwa nguvu za giza? Ulimwengu mzima unaichukuliaje kauli ya Sheikh Yahya, kwamba kumbe Rais wetu tuliyemchagua wenyewe analindwa kwa nguvu za kishirikina zisizoonekana kwa macho ya kibinadamu?

  Tunaambiwa katika Torati ya Musa kwamba; "Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu." - Kumb 18:10,11.

  Hebu niulize tena, tumefikia mahali pa kuitia unajisi Ikulu yetu kiasi cha kuruhusu ikaongozwa na wapiga madogoli na wanajimu kama Sheikh Yahya? Hivi ni kweli walinzi wote, ambao serikali yetu imetumia muda na fedha nyingi kuwapa mafunzo, wameshindwa kumpatia ulinzi Rais kiasi cha kuhitaji ulinzi wa vigagula?

  Sitaki kuamini nchi yetu ama Serikali yetu inataka kuendeshwa kwa nguvu za kichawi kama mojawapo ya imani za dini kama kule Guatemala, ambako ibada za kichawi za Wicca ni maarufu zaidi hata katika sheria za kimila.

  Tuliambiwa kwamba kuanguka kwa Rais Kikwete pale Jangwani Agosti 21, 2010 ilikuwa ni sababu ya swaumu, lakini kauli ya Sheikh Yahya imepingana kabisa na taarifa za Ikulu, kwa sababu yeye anasema kwamba Rais ‘alichezewa’ ndiyo maana ameamua kujitolea kumpa ulinzi usioonekana.

  Naomba niulize, ameajiriwa na nani kufanya kazi hiyo ya ulinzi wa Kikwete? Na tangu lini amekuwa msemaji wa mambo binafsi ya Rais Kikwete? Tuamini taarifa yake au ya akina Dk. Mwafisi na Janabi? Hivi Sheikh Yahaya anapata wapi ujasiri wa kutangaza hayo?

  Hakika inatia aibu na kinyaa kwa taifa linaloheshimika kama Tanzania, kwamba pamoja na karne hii ya sayansi na teknolojia, lakini bado viongozi wetu wanaishi kwa mazindiko kutoka kwa wanajimu. Ni hatari kwa mustakabali wa taifa na demokrasia kwa ujumla kwa masuala ya kitaifa kuhusishwa na imani fulani.

  Tuliambiwa tangu mwaka 2005 kwamba JK ni Chaguo la Mungu na viongozi wote wa kidini wameendelea kutuaminisha hivyo, lakini leo hii tunaposikia kauli za wanajimu kumpa zindiko tunakuwa na mashaka makubwa kwa sababu Mungu hachangamani na Shetani!

  Kwa tafsiri ya Sheikh Yahya ni kwamba, madaktari wa Rais hawaaminiki tena na hawahitajiki, vivyo hivyo, walinzi na hata Mkuu wa Usalama wa Taifa hafanyi kazi yake ipasavyo, jambo ambalo kwa asilimia zote naamini siyo kweli!

  Hivi Sheikh Yahya Hussein, aliyezaliwa mwaka 1932 huko Bagamoyo kwa wazazi wa Kimanyema, anajipendekeza kwa Rais Kikwete ama anautumia uhuru wake wa mawazo vibaya? Pamoja na uswahiba wake kwa JK, hivi anaweza kuthubutu kutamka hadharani kwamba yeye ndiye anayemlinda Rais wetu?

  Kuna wakati Sheikh Yahya alisema baadhi ya wabunge wangeburuzwa mahakamani kwa kashfa. Kwa hali ilivyokuwa hata kabla Shekh hajatabiri, mtu yeyote yule angeweza kutabiri hayo maana nchi ilikuwa imegubikwa na malumbano, wabunge kutuhumiana au mawaziri na watendaji serikalini kutuhumiana.

  Huu utabiri ni upuuzi mtupu. Kutabiri kitu katika hali ya kawaida kama "kesho kuna ajali itatokea Kibaha" ni upuuzi kwa sababu ukipita barabara ya Morogoro unaweza kukuta ajali zaidi ya 10 kila siku. Ndiyo aina ya utabiri wa Yahya. Utabiri wake wa mwaka jana kwamba "Mengi atajiunga na siasa" ulikuwa ni wa kichekesho kwa sababu siku zote Mengi alikuwa amejiunga kwenye siasa – Chama Cha Mapinduzi.

  Kinachotokea ni kwamba, yeye anasoma alama za nyakati na kuweka makisio kidogo pale, basi! Hata mimi nikisema kuna kiongozi wa nchi atakufa, huo ni utabiri wa uhakika sana, maana ni wazi lazima kiongozi yeyote atakufa, kama ilivyo kwa binadamu wengine, atakufa tu!

  Tuseme ukweli tu kwamba, imani za kinajimu au ramli ndizo zinazoleta matukio ya ubakaji na ukatili dhidi ya makundi mbalimbali ya jamii. Mbona Sheikh Yahya hajasema kuhusu kuanguka kwa Rais kule Mwanza, Jangwani mwaka 2005 na hata uwanja wa ndege huko Ubelgiji? Huko nako ‘alichezewa’ na nani?

  Sheikh Yahya huyu huyu alishatabiri kwamba atatokea rais mwanamke, lakini wagombea wa nafasi hiyo wote ni wanaume, tofauti na mwaka 2005! Anazungumzia uchaguzi wa mwaka huu, mbona alikwishatabiri huko nyuma kwamba hakutakuwa na uchaguzi? Au amesahau tumkumbushe?

  Watanzania tunasubiri kusikia kauli ya serikali kuhusu mauzauza haya ya Sheikh Yahya maana yameitia doa nchi yetu, vinginevyo hatutaeleweka hata kwa mataifa mengine ulimwenguni, kwamba sisi sote ni washirikina!

  Kikwete ni Rais wa Tanzania, hivyo hakuna kuliacha suala hili vivi hivi kwa sababu ya tafsiri nyingine ya watu kwamba suala hili ni la binafsi. Lolote litakalomtokea Kikwete binafsi litahusisha serikali pia, mpaka wakati ule atakapokuwa nje ya madaraka.

  Nimalizie tu kwa kusema maneno haya ya Biblia Takatifu aliyoyaandika Mfalme Daudi ndani ya Zaburi 127: 1-2: “Bwana asipoijenga nyumba, Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji, Yeye aulindaye akesha bure. Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi.”

  Tanzania tutubu jamani, utawala wa mwovu Shetani utatuangamiza.

  SOURCE; DIRA YA MTANZANIA Septemba 13, 2010
   
 2. Safari_ni_Safari

  Safari_ni_Safari JF-Expert Member

  #2
  Sep 13, 2010
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 22,481
  Likes Received: 5,862
  Trophy Points: 280
 3. Ndibalema

  Ndibalema JF-Expert Member

  #3
  Sep 13, 2010
  Joined: Apr 26, 2008
  Messages: 10,916
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Huyo mwandishi asimchimbie mkwara shekh yahya.
  kwani yeye anatoa ulinzi kwa mkuu mwenyewe binafsi na si serikali. na hilo hata Jk mwenyewe analijua na hasemi kitu.
  Shekh Yahya sio mwehu hadi aropoke kitu ambacho hakipo. tena kwa rais.
  Wa kumlaumu hapo ni rais.
   
 4. Iza

  Iza JF-Expert Member

  #4
  Sep 13, 2010
  Joined: Jan 8, 2009
  Messages: 1,848
  Likes Received: 120
  Trophy Points: 160
  Kwanini asitoe ulinzi wa wizi za mali ya Umma kama ana-uchungu na nchi hii...:mad2:
   
 5. Kiranja Mkuu

  Kiranja Mkuu JF-Expert Member

  #5
  Sep 13, 2010
  Joined: Feb 18, 2010
  Messages: 2,100
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Tatizo sio Sheikh...
  Taztizo CCM na Kikwete walimuona Sheikh kama Mungu.
  Wakamuabudu na kumsujudia, na kuwaambia Watanzania kuwa tumsujudie Sheikh kwa lile tamko lililosema Sheikh yuko sahihi kusema watakaompinga Kikwete watakufa.
  Mbona Nyerere alimtimua Sheikh Yahya?
  Je alikuwa mwehu????
  Tujiulize
   
 6. B

  Boramaisha JF-Expert Member

  #6
  Sep 13, 2010
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 820
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Sheikh Yahya mwenye kutabiria wenziwe vifo na maovu mengine naye ni binadamu kama walivyo binadamu wote. Naye iko siku yake atakufa na huenda siku hiyo haiko mbali! Binadamu hawezi kushindana na Mungu!
   
 7. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #7
  Sep 13, 2010
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Huyu jamaa ananikera, amepewa kazi na ccm hadi anajisahau. Baada ya kumsaidia Kikwete kama ambavyo Makamba na timu yake walitegemea anazidi kumchafua, na zile tetesi kwamba kila wiki mkuu huenda kijini kwao kusujudia majoka zinaanza kupata mashiko
   
 8. M

  Mbega Mzuri Member

  #8
  Sep 13, 2010
  Joined: Aug 1, 2008
  Messages: 44
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Sitaki kuamini kama hizi ndizo zama za yule mnyama 666!!! Yule ambaye anatajwa na manabii kuwa ndiye chukizo la uharibifu, ambalo sasa limekwishakaa mahali patakatifu...
   
 9. a

  asha ngedere Member

  #9
  Sep 13, 2010
  Joined: Nov 6, 2009
  Messages: 92
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kwa mtaji huu inabidi uamini tu, wanaturejesha enzi za Mfalme Suleiman aliyekuwa akizungumza na majini
   
 10. M

  Mbega Mzuri Member

  #10
  Sep 13, 2010
  Joined: Aug 1, 2008
  Messages: 44
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Tuiombee Tanzania, maana tangu nizaliwe ndiyo kwanza ninasikia rais anapewa ulinzi usioonekana - wa kichawi ili kuzuia asilogwe.
   
Loading...