TANZIA Sheikh Suleiman Kilemile afariki dunia

kunguni wa ulaya

JF-Expert Member
Mar 16, 2014
4,132
6,100
TAARIFA YA MSIBA WA SHEIKH SULEIMAN AMRAN KILEMILE

INNAA LILLAAHI WA INNAA ILAYHI RAAJI'UN

Kwa huzuni na masikitiko makubwa tumepokea taarifa za kufariki dunia Mwanachuoni Mkubwa wa Tanzania na Afrika Mashariki, Sheikh Suleiman Amran Kilemile.

Umauti ulimfikia Sheikh usiku wa Leo Tarehe 06 May 2020, Katika Hospitali ya Sinza Dar es Salaam Baada ya Kuzidiwa na Sukari na baada ya kuwa mgonjwa kwa muda.

Maiti kwa sasa ipo Masjid Thaqafa - Tandika, Kuiandaa kwa ajili ya kuzikwa.

Kifo cha Sheikh Kilemile ambae ni miongoni mwa Masheikh wakubwa na wenye Elimu kubwa ni pigo na pengo jengine kubwa mno katika uwanja wa elimu ya Kiislamu na DA'AWAH sio tu Tanzania, bali Afrika Mashariki na ulimwengu mzima wa Kiislamu kwa kuwa alikuwa mahiri katika kila fani miongoni mwa fani za Kiislamu.

Ameandika na kutafsiri vitabu kadhaa na kutoa mamia kama sio maelfu ya wanafunzi mahiri wengi na Sheikh ni mmoja wa Masheikh wachache waliotoa Darsa muda mrefu katika Msikiti wa Chihota - Tandika miaka ya Themanini.

Tunatoa mkono wa pole kwa Umma wa Kiislamu amma, Waislamu wa Tanzania khaswa, familia, masheikh, maustadh, walimu kwa msiba wa kuondokea na nguzo kubwa katika Uislamu.

Tunamuomba Allaah Taala Amsamehe marehemu, Amrehemu na kumuingiza katika Jannat Firdaws.

Aidha, Tunamuomba Allah Ta'ala awalipe malipo makubwa wafiwa na kuwamakinisha kwa subra na istiqaamah katika kipindi hiki kizito cha Msiba.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

FB_IMG_1588740027197.jpg

MAZISHI YAKE:

 
Tanzia (Nimenukuu kutoka facebook)

Kaburi ni tumbo lisiloshiba, mwanazuoni Sheikh Suleiman Kilemile dunia ilikua ni jukwaa njema kwako, ulitumia ujana wako na nguvu zako kuisimamisha dini yako, ulivunja matabaka, ukajenga daraja na hata wengine tukakufikia kirahisi tu, haukuwa mjivuni, mtu wa watu, umetufundisha kusimamia mambo unayoyaamini tena kwa dalili, mbali na neema ya elimu yako lakini bado ulishuka chini tukawa sote, wanazuoni mlio hai mnayo nafasi ya kujifunza kwa marehemu sheikh Kilemile.

Daima tutaikumbuka sauti yako ya mamlaka hasa unapofanya tashkir ya mambo (ukiyaita majambo) Subhanallah au ulipotaka kufafanua jambo lililowatanza wengi, kutoa rai, nani asiyejua daima ulihimiza umoja na mshikamano baina ya waislamu, sauti nzito iliyobeba maarifa sufufu hatutoisikia tena ikiwa mubashara bali kwenye kumbukizi za kaseti kutoka kwenye makavazi ya kambi uliyoijenga muda wote pale Thakafa Tandika.

Miaka mitano iliyopita ulikuwa mshenga wangu, ukanifungisha ndoa pale msikiti wa bamaga mwenge, tukiwa kwenye gari yako aina ya Toyota Ipsum ukaniambia hivi, tunafanya haya kwa maslahi ya akhera yetu, usiache kuniombea duah hata siku ukisikia nimetawafu dunia nakutakia kizazi chenye kheri na wewe na ukamaliza, ulikua baba bora kwa hakika.

Wanazuoni wa mfano wako ni wachache sana na wala hawapo kila mahala kwenye dunia ya leo. Kwa hakika Tanzania imefiwa, Mzizima(Dar es salaam) inazizima kwa majonzi mazito, tuliokujua tunaelewa.

Mola awape subra wanazuoni wote uliofanya nao harakati za dini, taasisi za kiislamu, waumimi na wanafunzi wako, familia na watu wako wa karibu, tunamuomba Allah akuthibutishie kauli thabiti.

Bustani ya taaluma uliyoiandaa kwa hakika itamea na yatapatikana matunda yenye rutuba, Sheikh Suleiman Kilemile wewe ni kielekezo cha wanazuoni wa kupigiwa mfano kwenye khairat.

Hatusemi ila yanayompendeza Allah, Inna lilahi wainna ilayhi raj'unn.

Ishaka Kihemba Abuu Ishmaal Ayoub.
 
Baada ya kifo ni hukumu swali ni je nitasimamaje hukumuni nitaitwa mtakatifu kuurithi uzima au muovu moto wa milele, Bwana atusaidie sisi tulio hai kuzihesabu siku zetu na tuishi sawa na mapenzi yake.

Sheikh amemaliza mwendo wake naye amelala, pole kwa family na ummah wote wa kiislamu kwa msiba wa mwanazuoni huyu.
 
Inna lillah waina ilayhi rajiun, moyo umehuzunika, macho yametoa machozi hatusemi ila yanayompendeza M'Mungu. ALLAH akupe kauli thabiti sheikh wetu.

Sent using Jamii Forums mobile app
Nimeswali sana msikitini kwake pale Tandika Thaqafa.

Alikua na kawaida kila baada ya swala ya Ijumaa anakua na mawaidha (darsa) la lisaa limoja!

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom