Weston Songoro
JF-Expert Member
- Feb 17, 2014
- 2,793
- 1,083
- Sheikh Ponda amkubali JPM
- Amuunga mkono urudishaji mali za Waislam
- Amuomba kuingilia kati zuio la mikutano ya kisiasa.
Ni miongoni mwa dondoo zilizopo kwenye gazeti la Majira. Hakika Rais Magufuli anakubalika kwa kila makundi ya kijamii
==========
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuahidi kusaidia kurudisha mali ambazo Waislamu wamenyang’anywa au kurubuniwa,
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameibuka na kusema anamuunga mkono Rais katika hatua hiyo huku akimtaka kukaa na jumuiya yao ili washauriane juu ya mahitaji yao ya msingi.
Sheikh Ponda, ambaye alipiga simu kwenye chumba cha habari cha Nipashe jana, alisema Rais Magufuli ameonyesha moyo wa kusaidia dini hiyo kwa kitendo chake cha kutoa fedha za kusaidia wanaokwenda hija.
Alimshauri Rais sasa kukaa na jumuiya yao ili asaidie maeneo ya kipaumbele kama elimu na afya, baada ya kutoa mchango kwa watu wanaokwenda kuhiji.
“Jana (juzi) nimeona ametoa hela kusaidia wanaoenda hija, lakini ukweli ni kwamba Jumuiya ya Waislamu ina mambo ambayo ni vipaumbele, mambo kama ya afya na elimu ambayo itakuwa vizuri tukae tuone ni namna gani atakavyotusaidia,” alisema Ponda.
Alipoulizwa kama haoni kwamba Rais anasimamia mambo hayo mawili kwa ngazi ya taifa, Ponda alijibu; “Ukiangalia wenzetu Wakristo wana hospitali na shule, na sisi pia tunayataka hayo mambo kwa hiyo ingekuwa vizuri kama tukishauriana naye ili aone namna ambavyo ataweza kutusaidia.”
Akizungumza kwenye Baraza la Idd El Fitr, juzi jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema anafahamu kwamba wapo baadhi ya watu wenye mali ambao huwatumia viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwarubuni kwa kuingia nao mikataba mibovu na hatimaye mali za baraza hilo hupotea.
“Mtu anakuja na kuwadanganya danganya katika kiwanja chenu eti atajenga kituo cha mafuta, ambako mngejenga msikiti. Kwani kituo cha mafuta na msikiti wapi na wapi, kipi bora?" alihoji Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliitaka Bakwata kutumia wanasheria wake kuhakikisha mali hizo zinarudishwa na kuwaonya wasiingie mikataba mibovu ambayo inasababisha migogoro.
“Serikali inapenda kuona mali za waislamu zinarudi mikononi mwa waislamu na mali za wakristo zinarudi mikononi mwa wakristo,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana na kauli hiyo, Sheikh Ponda, ambaye amekumbana na misukosuko mingi na vyombo vya dola katika miaka ya karibuni, alisema: “Kauli ya Rais inaonyesha namna anavyojali wananchi, suala hili limeniponza kuwa na kesi mahakamani kwa miaka miwili mpaka nikashinda na sasa Rais amekuja na kauli hii, kwa kweli tutaamunga mkono.”
Chanzo: Nipashe