Sheikh Ponda aomboleza kifo cha Mwandishi wa Zanzibar Kinyang'anyiro na Utumwa, Sheikh Issa Nesser Ismaily

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,881
30,226
MANENO YANGU KUHUSU KIFO CHA SHEIKH ISSA BIN NASSER MWANDISHI WA ‘’ZANZIBAR KINYANG’NYIRO NA UTUMWA’’

Na Sheikh Ponda Issa Ponda

Mimi ni mmoja katika watu wanaofanya uchunguzi katika historia ya Zanzibar.

Wajibu huo naufanya kama kiongozi Mtanzania.

Katika kutekeleza wajibu huo nimezungumza na watu makini wa kada mbalimbali na nimesoma vitabu kadhaa muhimu vya historia ya Zanzibar

Miongoni mwa vitabu hivyo ni, ‘’Kujenga na Kubomolewa Zanzibar,‘’ cha Kiongozi Mkubwa Ali Muhsin Barwani, ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,’’ cha Dk. Harith Ghassany, ‘’Historia ya Pwani ya Azania,’’ cha Mwalimu Hussein Bashir na ‘’The Partnership,’’ cha Rais wa Pili wa Zanzibar Aboud Jumbe.

Vingine ni ‘’Zanzibar hadi mwakaka 2000,’’ cha Bwana Ali Shaabani Juma, ‘’Tanzania na Propaganda za Udini,’’ cha Profesa Ibrahim Noor Sharif, ‘’Ukweli ni Huu,’’ cha Katibu wa ZNP Amani Thani Fairoz, ‘’Zanzibar Kinyang'anyiro na Utumwa,’’ cha Issa bin Nasser Al Ismaily na machapisho mengine.

Katika uchunguzi wangu marehemu Sheikh Issa Nasser ana upekee.

Nasema hivi kwa sababu yeye ameanisha jambo kubwa ambalo watu wengi hatulioni labda kwa sababu miaka mingi imepita na Wazanzibari hawazungumzi vya kutosha historia ya nchi yao.

Jambo lenyewe ni undani wa muundo wa utawala wa Zanzibar ulivyokuwa kabla ya taifa hilo kupata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1963.

Katika kitabu chake (Kinyang'anyiro) Sheikh Issa Nasser ameeleza hali ya utawala kabla ya Sultani Said bin Said.

Muhimu katika taazia hii ni kuitazama Zanzibar kuanzia utawala huo wa Sultani Said bin Said (1804 – 1856) kama Sheikh Issa alivyoichambua vuzuri katika kitabu chake na kwa lugha nyepesi na yenye kueleweka.

Kama tujuavyo utawala wa Said bin Sultan ulikuwa wa Kifalme.

Hata hivyo Sheikh Issa bin Nasser ameonesha utawala huo wa Sultan akiwa na madaraka kamili uliishia katika kipindi cha yeye Said bin Said.

Sheikh Issa Nasser ameeleza wakati Mfalme Said akiwa madarakani, Wazungu ambao aliwakaribisha na kufungua balozi zao (Wamarekani 1837, Waingereza 1841, Wafaransa 1844), chini chini walimrubuni na kumuandaa mwanaye Majid Said kwa maslahi yao kufanya mapinduzi mara tu baba yake atakapofariki.

Tarehe 19 Oktoba, 1856 Sultan Said bin Said alifariki na Majid aliingia Ikulu kwa nguvu na kujitangaza kuwa yeye ndiye Sultani badala ya kaka yake Thuwein bin Said ambaye ndiye aliyepashwa kurithi utawala ule.

Thuweni alipojaribu kuchukuwa hatua za kijeshi kumuondosha Majid Wazungu walimkabili Thuwein kijeshi.

Kuanzia hapo Majid sasa akiwa Sultani alishirikiana na Waingereza wakaunda utawala ambao Waingereza walijichomeka wakawa na sauti kubwa katika uendeshaji wa serikali ya Zanzibar.

Waingereza wakachukua fursa hii kuandika katiba ya Zanzibar.

Kwa Katiba hiyo nafasi ya Sultani katika utawala huo wa ilikuwa ya heshima tu lakini madaraka yote makubwa ya kidola yalikuwa kwa mwakilishi wa Mfalme wa Uingereza ambaye alikuwa balozi anaeiwakilisha Uingereza Zanzibar.

Ilipofika miaka ya 1950, wazalendo wa Zanzibar walianza harakati za wazi za kudai uhuru na mwaka wa 1963, Waingereza walitoa uhuru na kukabidhi nchi kwa chama kilichoshinda katika uchaguzi wa kidemokrasia - ZNP-ZPPP.

Kwa muktadha huo Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, yalikuwa dhidi ya serikali halali na huru ya watu wa Zanzibar iliyoshika madaraka baada ya kuondolewa utawala ule wa Waingereza na Sultani.

Hili ni jambp muhimu likafahamika.

Kwa hakika Marehemu Issa bin Nasser ameandika mambo mazito na ameuamsha ulimwengu kutoka katika kiza kinene kwa kufundisha historia halisi na ya kweli ya Zanzibar.

Ukikisoma kitabu chake kitakufungulia njia ya kuelewa kwa nini uchaguzi wa Zanzibar ya leo umekuwa na matatizo ya kukataliwa matokeo yake au kuyafuta.

Kitakusaidia kuelewa kwa nini bado wazanzibari wanayo ari na hamu kupitia sanduku la kura ya kutaka kuchagua serikali yao wenyewe inayotakiwa na wananchi wengi wa Zanzibar.

Kwa namna alivyoainisha historia ya Zanzibar Sheikh Issa Nasser amewafanyia watafiti wa sasa na wa baadaye hisani kubwa na kuwapa mahali pa kuanzia katika kuelewa matatizo mengi yanayogubika visiwa hivi kwa miaka mingi.

Mwenyezi Mungu alifanye kaburi lake kuwa ardhi katika ardhi ya peponi.

Amin
SHEIKH ISSA NASSER ISMAILY 1.jpeg
 
Allah amrehemu mzee wetu na ndugu yetu Issa bin Nasser, na amlaze mahala pema peponi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom