Sheikh Karume angeshauvunja Muungano

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Sheikh Karume angeshauvunja Muungano

Na Ahmed Rajab

TUNAUHITIMISHA mfululizo huu wa makala matatu kuhusu Zanzibar baada ya kupinduliwa wa serikali huru ya Zanzibar Januari 12, 1964 kwa kuuangalia Muungano ulioundwa baina ya Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, mwaka huo.

Licha ya kuwa hai kwa miaka 55 hakuna asiyetambua kwamba uhai wake una mashaka makubwa. Kusema kwamba Muungano huo umekumbwa na “kero” ni kuuficha ukweli wa hali halisi ilivyo kuhusika na muungano ulioziunganisha nchi mbili zilizokuwa huru.

Hivi sasa moja ya nchi hizo, Zanzibar, kwa uhalisia wa mambo imeupoteza uhuru wake. Badala ya kuwa nchi yenye hadhi sawa na nchi nyenzake, Tanganyika, sasa imegeuka (kwa kila hali) na kuwa na mahusiano yanayofanana na yale ya mkoloni mwenye kutawala na mtawaliwa. Huo ndio ukweli halisi ulivyo na utauona utapouchambua kwa kina Muungano wa Tanzania

Salim Said Rashid ni miongoni mwa watu wachache leo wenye haki ya kudai kuwa wanaijua historia ya karibu ya siasa Zanzibar na Muungano wake na Tanganyika. Ameshiriki kwa karibu katika harakati za ukombozi za Visiwa hivi tangu akiwa mwanafunzi wa skuli ya sekondari katika miaka ya 1950.

Akaendelea na mapambano akiwa Uingereza anasomea masuala ya uchumi na sheria ya kimataifa katika Chuo maarufu cha London School of Economics (LSE). Alirudi Zanzibar na aliteuliwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi wiki moja tu baada ya mapinduzi. Aliendelea akawa naibu waziri wa fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano; naibu waziri wa fedha na utawala wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi wa Tanzania nchini Guinea ambako alikuwa msiri mkubwa wa Kwame Nkrumah, rais wa kwanza wa Ghana aliyekuwa akiishi uhamishoni Conakry. Mwishowe Salim Rashid alikuwa balozi wa Tanzania nchini Ethiopia.

Muungano ulipokuwa unapikwa na Rais Julius Nyerere wa Tanganyika Salim Rashid alikuwa jikoni akiwa msaidizi mkuu wa Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Ni kwa sababu hiyo Raia Mwema imezungumza naye kupata maoni yake:

RM: Hebu tueleze unavyouona Muungano na mafanikio yake.

SR: Muungano umezongwa na migogoro tangu siku ulipoundwa hadi leo. Siyaoni mafanikio yoyote yale yaliyopatikana, si kwa upande wa Zanzibar na hata si kwa Tanganyika. Ni wazi Muungano huu haukuundwa kutokana na hisia za Watanganyika na za Wazanzibari. Muungano umeletwa kwa shinikizo la mataifa ya kigeni.

RM: Unadhani Sheikh Karume angekuwa hai leo angefikiria upya kuhusu Muungano?

SR: Angelikuwa Sheikh Abeid Amani Karume yuhai leo, pasingekuwa na Muungano. Siku moja kabla hajauliwa alinambia kwamba alikuwa na nia ya kuuvunja Muungano. Watu wengi, pamoja na mimi, tunajua kwamba Karume alichukulia suala la Muungano kuwa la muda na sote tunajua kwamba kwa uzalendo wake wa Kizanzibari asingeukubali muundo ulioibuka sasa wa Muungano. Unaelewa kwamba wakati Muungano ulipoundwa hali halisi ilikuwa ya vitisho; ilikuwa jambo ambalo Zanzibar ililazimishwa kulikubali.

RM: Kwa vipi?

SR: Kwa sababu wakati huo ulikuwa wakati wa “Vita Baridi”. Kulikuwa na madola ya Mashariki na madola ya Magharibi. Madola ya Mashariki yalikuwa yameyapokea na yameyakubali mapinduzi ya Zanzibar. Madola ya Magharibi yaliyakataa, yakafanya kila mbinu kuhakikisha kwamba Zanzibar haiendelei na kusalia kuwa dola huru.

RM: Unakusudia kusema kwamba walimtisha Karume ?

SR: Ndio. Walimtisha kuwa watatumia nguvu ya kijeshi kuivamia Zanzibar na kuiondoa Serikali yake. Walimtisha kuwa nchi za Magharibi hazitokubali Zanzibar iselelee kuwa taifa huru la kimapinduzi kwa khofu kuwa wanaweza wakapeleka umaarufu wa mapinduzi katika kanda hii ya Afrika. Lilikuwa jambo gumu hili na utakumbuka mambo yote yalikuwa siri. Hata wahusika katika Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar hawakufahamishwa kitu gani kinatokea mpaka siku ya mwisho. Aliyekuwa akijua kila kitu alikuwa Mwalimu Nyerere.

RM: Wewe ulikuwa karibu sana na Sheikh Karume na mimi najua akikuamini sana, alikueleza habari ya vitisho hivi ?

SR: Naam, alinieleza. Sisi tulikwenda Dar es Salaam siku 10 kabla ya muungano kuundwa na tulipofika kule Karume akakutana na Nyerere. Mwalimu akaniambia mimi niende nikanyowe (kwa vile niliamshwa mapema kwendea Dar sijawahi kunyowa ndevu). Kwa hiyo mimi sikuwapo katika mazungumzo yao, yaani baina ya Nyerere na Karume.
Ni wazi kwamba MNyerere hakutaka niwepo ndio maana akaniondosha kwa ujanja nikanyowe ndevu.

Hapo ndipo Karume alipofahamishwa njama za Magharibi kuhusu Zanzibar na kwamba kuepukana nazo alilazimika kujiunganisha na Tanganyika.

RM: Lakini mbona baadhi ya wasomi wameandika mlikuwa na kikao cha pamoja wewe, Mzee Karume na Mwalimu Nyerere?

SR: Kama nilivyokwambia mimi kweli nilikwenda Dar es Salaam, lakini tulipofika ikaonekana Mwalimu hakutaka mimi niwepo kwenye kikao kile, ndo akanambia nikanyowe ndevu. Lakini baada ya siku mbili tatu makaratasi yenye mapendekezo ya muungano yakaletwa Zanzibar. Mzee Karume tukawa tunayazungumzia makaratasi hayo na nilikuwa namfahamisha kila kitu.
Kuna kitu kimoja muhimu lazima kifahamike, huu muungano tangu upendekezwe mpaka usimame haikuchukua wiki mbili. Na kabla Karume kuitwa na Nyerere Dar es Salaam, ulikuja hapa ujumbe wa Tanganyika na wa Kenya uliomletea barua Mzee Karume.

RM: Barua hiyo ilisema nini?

SR: Barua hiyo ilikuwa ya kumtisha Karume kuwa hapa Umma Party ingeweza ikamuumiza, ikammaliza. Ilikusudiwa kuleta mtafaruku ambao haukuwepo.

RM: Lakini baadhi ya wataalamu, hasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanadai huu ulikuwa muungano wa hiyari na uliridhiwa na Baraza la Mapinduzi (BLM). Ukiwa katibu mkuu wa BLM wakati unaohusika, unasema nini kuhusu hili?

SR: Kuwa muungano ulikuwa wa hiyari au si wa hiyari tusizingatie maneno ya wataalamu wa Chuo Kikuu tu, bali tuzingatie vitabu vya waliohusika wakati ule, hasa wanadiplomasia wa Kimarekani. Ukisoma vitabu vyao utaona ulikuwa muungano wa hila, si wa halali.

Si wa halali kwa sababu Baraza la Mapinduzi halijapata kuitwa hata katika kikao kimoja kuzungumzia Hati ya Muungano, kuithibitisha na kuipitisha kama ilivyopasa kufanywa na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.

RM: Wewe ukiwa katibu Mkuu wa Baraza, si ilibidi ushiriki vikao vyote?

SR: Ilibidi ndio, na mimi ndiye niliyekuwa naviitisha.

RM: Inasemekana kulikuwa na kikao cha pamoja cha BLM na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Kikao hicho kilizungumzia nini?

SR: Hakukuwa na kikao kama hicho. Kilichotokea ni kwamba Mwalimu alikuwa anahutubia Bunge na wajumbe wa BLM wakaalikwa kusikiliza; hakukuwa na mjadala.

RM: Inasemekana Mwanasheria Mkuu wa wakati ule, Wolfango Dourado hakushirikishwa katika hatua za kuelekea Muungano, bali alishiriki wakili kutoka Uganda, Dan Nabudere.

SR: Sio Mwanasheria Mkuu tu ambaye hakushirikishwa, bali hata wizara, pamoja na wizara muhimu ya Mambo ya Nje ya Zanzibar, haikushirikishwa. Hii ilikuwa sera binafsi ya Rais wa Awamu ya Kwanza wa Zanzibar na Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanganyika.

Kuhusu sehemu ya pili ya swali lako kuhusiana na Dan Nabudere, huyu nilimleta mimi hapa baada ya kuona umuhimu wa Serikali kupata ushauri wa kisheria. Lakini bahati mbaya alipofika hapa ilikuwa mkataba wa Muungano ushatiwa saini na akaondoka bila kufanya chochote.

RM: Inasemekana kulikuwa na ofisi za Wizara za Muungano hapa Zanzibar, ilikuaje zikaondoshwa?

SR: Baada Muungano walikuja mawaziri kufungua ofisi za Muungano hapa, lakini Serikali ya Mapinduzi ikakataa. Na napenda kukufahamisha kwamba, namna muungano ulivyoendeshwa katika awamu mbali mbali za Zanzibar inahitilafiana. Wakati wa Awamu ya Kwanza Zanzibar ilikuwa inaendeshwa kama taifa huru.

RM: Kwa vipi ?

SR: Kwa kuwa ilikuwa na jeshi lake, ilikuwa na idara zake, hakukuwa hapa na wafanya kazi wa Muungano, ilikuwa na chama chake, ilikuwa na kila kitu chake, na mamlaka yake ya kimataifa. Mambo yaliyokuwa yanafanya kazi yalikuwa ya Muungano tu. Hata hayo yalikuwa na matatizo. Kwa mfano, sarafu ya fedha za kigeni ya Zanzibar, ambayo ilikuwa nyingi, haikuchanganyishwa na ile ya Tanganyika na ilikuwa chini ya mamlaka ya Zanzibar, haikuwa chini ya mamlaka ya serikali ya Muungano.

RM: Kwa maelezo yako, na unavyoonekana kwa jumla mwenendo wa muungano huu, ni wazi kwamba suala hili liliharakishwa. Inawezekana kuwa kutokana na msukumo huu Karume mwenyewe hakuelewa kilichokuwa kikiendelea?

SR: Sijui kama alikuwa akielewa au hakuelewa, lakini kasi hii ilikuwa kwa sababu nchi za Magharibi zilikuwa zinataka kuleta majeshi hapa. Hawakukubali iwepo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Walitaka hili jambo lifanyike haraka sana. Lakini makosa yaliyotokea ni kwa upande wa Zanzibar, na wa Tanganyika, kutoshirikiana na dola nyingine za Afrika na zilizoendelea ulimwenguni kuelezea suala hili kimataifa, kwenda Umoja wa Mataifa kuonesha shinikizo iliyokuwa ikifanyiwa nchi huru ambayo kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa inayo haki ya kuamua inavyotaka kuhusu mustakbali wake.

Suala hilo lina umuhimu wake hadi leo ambapo Wazanzibari wanalilia haki yao ya kuwa na mamlaka kamili yatayowawezesha kujiamulia mambo yao watakavyo. Tunataka tuwe na mahusiano ya kidugu na ujirani mwema na Tanganyika kinyume na ilivyo sasa ambapo kuna uhasama mkubwa kutokana na muundo wa Muungano ulivyo.

Baruapepe: aamahmedRajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab


IMG_20211022_180450.jpg
 
Back
Top Bottom