Sheikh Haidar Mwinyimvua

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,854
30,200
KALAMU YA ABDALLAH TAMBAZA INAPOOMBOLEZA HUTOA MACHOZI

SHAJARA YA MWANAMZIZIMA:

Buriani Sheikh Ahmed Haidar
Na Alhaj Abdallah Tambaza

JUMUIYA ya wanazuoni wa Kiislamu kote ulimwengu; wafuasi wa dini ya Kiislamu wa Tanzania— hususan wa Jiji la ‘Dar ul Salaam’ na vitongoji vyake— Jumanne ya Januari 19, mwaka huu, itabakia kuwa ya simanzi nzito kwao.

Mchana wa siku hiyo, mara baada ya Sala ya Adhuhuri tu kumalizika; kwa kasi ya ajabu sana, habari zilizagaa kwamba; aliyekuwa Imam Mkuu wa Masjid Mwinyikheri, Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua, amefariki Dunia hospitalini Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Nilikuwa nimejibanza nje pembezoni mwa Msikiti wa Manyema nikisubiri jua kali la adhuhuri liponge (lipungue); ghafla, simu yangu ya kiganjani ikalia nikaipokea:

“Uko wapi bwana wewe; njoo haraka twende Muhimbili Sheikh Ahmed amefariki muda huu hospitalini,” ilisikika sauti ya ‘kwikwi na kilio’ kutoka kwa Mzee Mwinyi Mussa; ambaye, yeye na mimi ni wadhamini wa kudumu wa Msikiti wa Mwinyikheri uliopo Kisutu, Dar es Salaam.

Hali ilinibadilikia.

Saa ileile kichwa kikaniuma sana; damu nayo ilipanda juu na kushuka chini, kwenye mishipa kwa nguvu mno.

Niliwaza na kuwezua namna ya kuziba pengo la kiungozi kwenye msikiti ule mkongwe, ambao Sheikh Ahmed Haidar amekuwa akiuongoza kwa zaidi ya miaka hamsini sasa—nusu karne na ushei amekuwapo pale—jibu sikulipata mpaka wakati huu nikiandika taazia hii!

Nilimfahamu Sheikh Ahmed (85), wakati tukiishi ‘kijijini Kisutu’ tokea miaka ya 1950s, mimi nikiwa mtoto mdogo kabisa kwake.

Nyumba zetu zilikuwa jirani mno; mita chache tu kutoka mahala yalipo makaburi ya Kisutu ya jijini Dar es Salaam.

Kwa uhakika kabisa ni yale maeneo ambayo kwa sasa yametapakaa majengo ya Chuo cha Biashara (CBE) na Taasisi ya Ufundi na Teknolojia (DIT).

Hakuwa mtu wa makamu yangu kwa jambo lolote lile; yeye ni ‘darja’ kubwa isovukwa kirahisi namna hiyo—ni ‘mithili ya kichuguu na Kilimanjaro’.

Ila, nakumbuka kwamba alikuwa ni mtu aliyezaliwa kwenye familia adilifu ya sheikh mwengine mashuhuri, Mzee Haidar Mwinyimvua—mmashomvi mwenye asili ya Bagamoyo.

Sasa, ni nani basi huyu Alhaji Mzee Haidar Mwinyimvua baba?

Mzee Kassim Haidar, ni mmoja wa watoto wa Alhaji Mzee Haidar Mwinyimvua bin Hatibu. Yeye ni wa tatu kuzaliwa akimfuatia hayati Sheikh Ahmed Haidar.

Nilikwenda nyumbani kwake Magomeni Mwembechai, kumpa ‘mkono wa tahnia’ (kumpa pole), kufuatia kifo cha kakake mpenzi Imam Ahmed Haidar.

“Mzee wetu alikuwa na wake wawili ambapo kwa mke mkubwa alipata watoto watano akiwamo Mtumwa, Ahmed, Kassim, Twahir na Adam… na kule kwa mama mwengine kulikuwa na wanawake Asiya, Sauda na wa mwisho ni mwanamme anaitwa Haji…

“Baba yetu ni mwenyeji wa Bagamoyo kijiji cha Nzoe; ambapo babu yake baba, ndiye aliyekuja mahala hapo miaka mingi nyuma akitokea kijiji cha Siyu, kule Lamu, Mombasa…

“…Akiitwa Mzee Mwinyimvua Khatibu, ambaye, habari zinasema, ndiye mtu wa mwanzo kuanza kuifundisha Qurani, kule Bagamoyo,” amesema Kassim Haidar kwa sauti ya unyonge sana kutokana na uzee, msiba mzito, pamoja na maradhi ya miguu inayomsumbua.

Mzee Haidar Mwinyimvua, siku zote alikuwa mpinzani mkubwa wa ukatili wa utawala wa kikoloni; hususan kuhusu ubaguzi wa utoaji wa huduma muhimu za kijamii, ikiwamo elimu, makazi na afya.

Hivyo basi, alijitosa na kushiriki kwa hali na mali katika harakati za ukombozi wa nchi hii, akiwa mmoja wa watu wa mwanzo kabisa kujiunga na chama cha ‘TANO’ siku hizo mara tu kilipozinduliwa.

Kwenye harakati zile, Sheikh Mwinyimvua alikuwa Mwenyekiti wa Tawi la Mvita na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama pamoja na Baraza la Wazee wa chama hicho kilichopambana kudai uhuru wa Tanganyika.

Katika mgogoro mashuhuri kati ya aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee la TANU— Sheikh Takadir na Nyerere— alikuja kuwa mwenyekiti wa baraza hilo baada ya Sheikh Takadir kufukuzwa uanachama. (Rejea kitabu mashuhuri cha ‘Shajara ya Mwanamzizima’ kilichoandikwa na mwandishi huyu; na kile cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, kilichoandikwa na Mwanahistoria nguli nchini Mzee Mohammed Said).

Mzee Mwinyimvua, alikuja kuwa mwenyekiti wa tawi mashuhuri la Mvita mjini Dar es Salaam; na baadaye akiwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama cha TANU, alipata nafasi ya kuwamo kwenye safari nyingi za kuzunguka nchi kukinadi chama na makusudio yake.

Kwenye mkutano mashuhuri wa mwaka 1958, uliofanyika Tabora kujadili ushiriki wa TANU kwenye uchaguzi wa utatanishi wa KURA TATU; Haidar Mwinyimvua alikuwa mmoja wa wajumbe wa Jimbo la Mashariki (Eastern Province), ambapo alitoa mchango mkubwa sana wa mawazo, yaliyosababisha kuzuia chama kusambaratika kabisa kufuatia sintofahamu na kutoelewana miongoni mwa viongozi waandamizi.

Pale Kisutu alikokuwa akiishi na wanawe; alikuwa fundi cherehani maarufu wa ushonaji wa kanzu asilia za kudarizi pamoja na makoti yake; vazi lilokuwa rasmi la Waswahili wa Mzizima siku hizo.

Sifa kuu aliyokuwa nayo fundi huyu mshoni, ni kwamba alikuwa ni mkweli na mnyenyekevu ambaye hakupendelea kuwapa wateja wake ahadi za uongo hata mara moja—akikuahidi siku ya kuchukua kazi yako, basi hutimiza ahadi yake!

Katika kazi yake hiyo, Mzee Haidar, alimudu kumiliki nyumba kadhaa za kupangisha mjini Dar es Salaam, ambapo aliweza kuwapatia elimu bora kabisa ya dini na ile ya mazingira (secular) watoto wake wote.

Katika orodha ya watoto wake, wamo waliokuwa wanasheria; maofisa wa benki; maofisa serikalini na kwenye mashirika mengine ya umma na serikali; jambo ambalo lilikuwa ni nadra sana kulishuhudia katika jamii nyonge ya Waafrika wa Tanganyika.

Sasa basi, hayati Sheikh Ahmed Haidar, tunayemuomboleza leo; akiwa mtoto wa pili kuzaliwa, tokea mwanzoni babake alihakikisha anapata malezi bora na elimu kubwa kwa kupambana na ubaguzi wa utoaji huduma usiozingatia usawa uliokuwa ukifanywa na ukoloni wa Kiingereza.

Hayati Sheikh Ahmed, alipata elimu yake ya madrassa kutoka kwenye chuo maarufu cha ‘Aljamiatul Islamiya fi Tanganyika’ kilichojengwa na wakazi wa kizalendo wa Mzizima kwenye miaka ya 1930s, ili kupunguza ombwe la kukosekana kwa elimu hiyo kwa wazalendo wenyewe—elimu ya kikoloni iliwalenga Wazungu na Wahindi.

Sasa basi, katika elimu ya mazingira (secular), Sheikh Ahmed alisoma kwenye shule mahsusi zilizotengwa na wakoloni kwa ajili ya ‘watu weusi’ za Mchikichini na ile ya Kitchwele Government African School (sasa Uhuru Mchanganyiko).

Alipotoka hapo, babake alimpeleka Unguja kwenda kusoma elimu ya dini ya Kiislamu kutoka kwa masheikh wakubwa wa siku hizo akiwamo na Sheikh Suleiman Alawi msikiti Gofu; Abdallah Saleh Farsy barazani kwake; pamoja na Sheikh Jamalilail nyumbani kwake Vikokotoni.

Kutokana na uhodari aliouonyesha kiielimu, kijana Ahmed Haidar, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo kupendekezwa kujiunga na ‘Zanzibar Muslim Accademy’ (chuo cha juu cha Kiislamu Zanzibar) pale kilipoanzishwa mnamo mwaka 1957.

Hapa, pamoja na wanafunzi wengine kutoka Tanganyika; alikutana na kusoma pamoja naye, aliyepata kuwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania hayati Sheikh Issa Simba.

Mwengine aliyekutana naye hapo chuoni, ni hayati Sheikh Yahya Hussein Juma Karanda; ambaye pia alikuja kuwa mwanachuoni mwengine wa kupigiwa mfano katika Afrika Mashariki na Kati, akibobea zaidi kwenye usomaji wa Qurani kwa njia ya Tajwiid na utabiri kwa kutumia nyota.

Alidumu pale Zanzibar Muslim Accademy kwa miaka mitano; ambapo pia alisoma kwa masheikh wakubwa wa Kizanzibari wa miaka hiyo katika masomo ya Dini ya Kiislamu kwenye darsa za jioni.

Baadaye, kwa kupitia taasisi iliyojulikana kama Jumuiya ya Kiislamu ya Afrika Mashariki (East African Muslim Welfare Society), kijana Ahmed Haidar alipata ufadhili (scholarship) wa kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Al-azhar Sharif kule Cairo, Misri.

Kutokana na uhaba wa ndege wakati ule, safari ile ilibidi aende kwa kutumia meli iliyokuwa ikizunguka sehemu nyingi na kuchukua muda wa miezi kadha mpaka kufika Cairo.

Baada ya safari ndefu na misukosuko ya baharini, meli ile ilichelewa kuwasili nchini Aden, ambako Ahmed alitakiwa abadilishe na kupanda meli nyengine ya kuelekea Cairo.

Aliposhuka bandarini nchini Aden, meli yake ya kumpeleka Cairo ilikuwa tayari imeshaondoka.

Alilazimika kubakia nchini Aden akawa anasoma ‘tajwiid’ misikitini na kupatia umaarufu mkubwa sana.
“Hayati Sheikh Ahmed, alikuwa akipenda sana kusoma ‘Tajwiid’ kwa mtindo wa msomaji mwengine mashuhuri wa Misri, hayati Sheikh Mustapha Ismail; na wakati mwengine akitumia njia za Sheikh Mahmud Sadiq Alminshawi wa hukohuko Misri,” Hiyo ni kwa mujibu wa Sheikh Mohammed Nassor ambaye ndiye ‘mjawiid’ bingwa Tanzania kwa sasa, ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Mufti Zubeir bin Ali.

Akiwa bado kijana mdogo kabisa, aliishi nchini Aden kwa miezi 6 akisubiri kuendelea na safari iliyomtoa kwao kuelekea Cairo, Misri, kwenye Chuo Kikuu cha Al azhar Sharif.

Baada ya miaka saba ya masomo pale Al azhar, Imam Ahmed Haidar, alitunukiwa shahada yake ya mwanzo ya (BA) katika sheria ya Dini ya Kiislamu.

Pale Al- azhar Sharif, Misri, hayati Sheikh Ahmed Haidar, anatajwa kwamba aliacha rekodi ya kuwa mmoja wa wanafunzi bora na mahiri kusoma katika chuo hicho chenye uhai wa karibu miaka elfu (1000) tokea kianzishwe.

Alipohitimu, alikwenda kuwa mwalimu wa Qurani katika nchi za Arabuni ikiwamo na nchi ya Aden; ambako alifundisha Qurani Tukufu, kwenye vyuo mbalimbali.

Wanafunzi aliowafundisha nchini Yemen, sasa wamekuwa masheikh wenye majina makubwa na wamezagaa bara zima la Arabu.

Akiwahutubia waombolezaji mazishini; Sharrif Abdulkadir, amesema amepokea chungu nzima ya salamu za rambirambi zilizotumwa na masheikh wakubwa duniani, wakielezea kusikitishwa kwao na kifo cha mwanazuoni huyo mkubwa.

Taarifa zilizopo ni kwamba, Sheikh Ahmed Haidar, ameweka ‘kibindoni’ mwake, elimu mbalimbali za Dini ya Kiislamu; ikiwamo usomaji wa Tajwiid, tafsiri, hadith, mirathi na sheria mbalimbali za miamala mingine.

Sheikh Ahmed, amewahi pia kuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro akifundisha sheria za Kiislamu – Islamic Law.

Amepata pia kuwa mshauri mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Markaz, pale Chang’ombe mjini Dar es Salaam, ambacho ni ‘chuo dada’ (sister college) na Al-azhar sharif cha kule Misri.

Aliyepata kuwa Imam Mkuu wa Msikiti wa Kitumbini jijini Dar es Salaam, Myemen, hayati Sheikh Juneid, alipata kumwelezea Marhum Sheikh Ahmed Haidar katika uhai wake (kwa msisitizo wa mara tatu); kama ni mtu msomi ‘Alim!.... Alim!…. Alim! ambaye hajionyeshi’.

Naye Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ali, kabla ya kuongoza sala ya janaza ya Marehemu Sheikh Ahmed Haidar alisema hivi:

“Hakuna mfano wake katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati… katika wanazuoni wakubwa wachache waliobakia duniani, mmoja ni huyu aliyekuwa akiishi nasi katika ardhi ya Tanzania…

“Ni bahati mbaya, kwamba tulibahatika kuwa na mtu wa namna hii na tukashindwa kuchukua ‘japo robo’ ya robo ya elimu yake…

“Nikiwa Mufti wa nchi hii, nilifika hapa msikitini kwake kuja kuchota kwenye kisima hiki cha elimu ambayo leo inakwenda kuzikwa… anayezikwa hapa si huyu sheikh kamwe, bali na elimu yake pia imeondoka…”

Kwa waumini wa Msikiti wa Mwinyikheri ambao wamekuwa wakimsikia akiwaswalisha sala zote, siku zote, wakati wote; daima watamkumbuka kwa ‘khutba’ zake nzuri siku za Ijumaa zilizosheni mafunzo, hekima, hadithi pamoja na aya za Qurani zilizofafanuliwa vilivyo!

Kwa wale waumini ambao hawakupata bahati ya kuswali nyuma ya imam huyu; itoshe tu kusema kwamba ‘ilikuwa ni bahari kubwa sana iliyojaza mengi’ katika maelekezo ya Dini ya Kiislamu, ambayo amezikwa nayo juzi.

Sheikh huyu, mbali ya kuwa alikuwa mahiri katika Qurani, alikuwa mwerevu, mjuzi na mfuatiliaji wa matukio ya duniani (General Knowelege na current affairs).

“Katika moja ya khutuba zake za Ijumaa alipata kuwashambulia wale wanaozungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa uwepo wa Taasisi ya Umoja wa Kimataifa (United Nations) hapa duniani, akisema; ‘U.N katika miaka miwili tu ya mwanzo, Palestina walipoteza nchi yao; “1952/53 Vita vya Korea ikaigawa Korea vipande viwili hasimu; baadaye Suez Canal nayo ilidhulumiwa; mwaka 1960 Patrice Lumumba kapoteza uhai wake Congo na UN ipo ikitazama na Katibu Mkuu wake akauawa pia…
“Mauaji ya Sharpeville (Sharpville massacre); Mauaji na mgawanyiko wa Checkoslovakia chini ya Warsaw Pact iliyoongozwa na Urusi; Vita ya Vietnam na Marekani…

“Hayo ni mafanikio gani ya kusifiwa nayo mtu?’ Umoja wa Mataifa ni taasisi dhalimu kabisa ile… iliyosimamia maovu yote huku ikiwa kimya bila ya kuchukua hatua stahiki… kamwe si sawa kuipa sifa bali ni stahili yake kulaaniwa kwa nguvu zote kwa kuifikisha Dunia hapa ilipo leo,”amesema Faraj Abdallah Tamim mhadhiri wa MUM Morogoro, akimnukuu Sheikh Haidar, ambaye amefanya naye kazi kwa karibu sana, katika ujenzi wa Msikiti wa Mwinyikheri.

Siku moja mnamo mwaka 1979, mimi na hayati babangu tulikwenda kwa Sheikh Haidar kumtaka anifanyie dua katika kesi Mahakama Kuu ambayo nilikuwa naelekea kupoteza haki yangu.

Siku hiyo hayati Sheikh Haidar alidhihirisha miujiza ya Qurani:

Alifungua msahafu akasoma aya fulani ndogo tu; kisha akamwelekeza babangu awe anasoma kipande hicho cha Qurani yeye mwenyewe kila siku ya kesi.

Akimaliza kufanya hivyo, achukue kidole changu gumba aandike harufu ya ‘Jim’ kwenye ukucha na kukifumba kidole muda wote tukiwa mahakamani.
Akasema, kwa uwezo wake Allah haki itakuwa upande wako mwisho wa kesi!

Ndivyo ilivyokuwa dhuluma ile ikapeperushwa nikapewa haki yangu kwa kupewa ushindi hukumu iliposomwa!

Kitendo cha kukatwa mguu baada ya kuharibika kwa sukari, kilimsononesha sana yeye na wale nduguze wa karibu waliokuwa wakimhudumia na kumliwaza pale wodini.

Sasa, siku moja alizungumza na nduguze wanaomwuguza pale hospitalini Muhimbili:

“Nawaona sura zenu hazina furaha… mimi jana nilioteshwa usingizini kwamba huko ninakokwenda ni kuzuri…

“Sasa nyinyi msiwaze sana kwa hilo… namwomba Allah awalipe malipo mema kwa haya yote mliyonifanyia mimi,”alinisimulia mmoja wa wajukuu zake tulipomtembelea Sheikh siku chache kabla ya kufariki kwake.

Aidha, siku tatu kabla kufariki kwake; ikiwa ni Jumapili, Januari 17, 2021; mbele ya watu kadhaa tuliokuwa kitandani pale, hayati Sheikh Ahmed alituonyesha ‘karama’ zake pale mmoja wa wale vijana wake alipomwomba ruhusa ya kumnyoa nywele ili awe msafi!

Sheikh alimwuliiza; leo kwani siku gani? Alipojibiwa kuwa ni Jumapili, basi akaanza kuhesabu polepole kwa sauti ya kigonjwa; ‘Jumapili…Jumatatu…Jumanne’ na kusema: “Ninyoweni Jumanne mchana!”

Subhanallah! Tulidhani mgonjwa alikuwa anajipa muda tu wa kupumzika ili asisumbuliwe.

Hakuna kati yetu aliyeelewa kwamba Sheikh alikuwa akitutabiria siku yake ya kifo itakuwa Jumanne mchana; na kwa hivyo ni bora akawa msafi siku hiyo na wakati huo!

Januari 19, 2021 ‘Jumanne mchana’ sheikh alikutwa amekufa kitandani mwake kama vile amelala tu!

Huyo ndiyo Sheikh Ahmed Haidar tunayemzungumzia na leo hatunaye tena!

Tunamwomba Allah amfanyie kama alivyomwotesha na sisi tuliobakia atupe kauli thabiti kama yeye kwenye wakati wa kuondoka hapa duniani.

Tunamwomba pia kaburi liwe moja ya viwanja vya peponi; na wala asilifanye kuwa moja ya mashimo ya motoni!

Ameen.

atambaza@yahoo.com; 0715808864
 
Picha ya Sheikh Haidar Mwinyimvua
Screenshot_20210204-162500.jpg
 
Allah ampe kauli thaabet

Mwamba katila Miamba niliyowahi kuishuhudia ambayo haina mbwembwe kabisa, usipomuongelesha au mkianzisha ligi ya jambo lolote hata kama la dini atapiga kimya kama hayupo

Kwny Mazishi yale Sheikh Walid aliuliza swali lenye jibu ambalo hakuna aliejibu kwa kuwa sote tulijikuta tunatafakari

Aliuliza 'mshawahi kumuona kwny Kamera au hata kwny siti za mbele kwny shughuli yeyote…?
 
IMG_20210206_173458.jpg

Wakati napewa taarifa ya kifo chake, nilichanganyikiwa hadi kujiuliza ndio yupi!
 
Picha ya Sheikh Haidar MwinyimvuaView attachment 1694282
Allah amjaalie kauli thabit, amsamehe madhambi yake, amjaalie Jannat Al Firdaus iwe ndio mafikio yake.
اللهم اغفر لهم وارحمهم وعافهم وااعف عنهم واكرم نزلهم ووسع مدخلهم واغسلهم بالماء والثلج. واجعل قبورهم روضة من رياض الجنة. برحمتك يا أرحم الراحمين.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom