Shehena ya Kilo 15 za Madawa ya Kulevya aina ya Heroine yakamatwa Uwanja wa Ndege wa KIA..!!

Money Stunna

JF-Expert Member
Aug 9, 2011
13,054
6,281

ONYO la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe la kuwafukuza kazi vigogo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kama atasikia dawa za kulevya zimepita uwanjani hapo, limezaa matunda ambapo jana raia wawili wa kigeni walikamatwa wakiwa na kilo 15 za dawa za kulevya aina ya heroine. Wiki iliyopita akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Kampuni ya Uwakala wa Uendeshaji wa Kia (KADCO), Dk Mwakyembe alisema ana taarifa za kutosha kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, hasa Kitengo cha Usalama na Uhamiaji wanaohujumu sifa za kiwanja hicho.
Alidai kuwa wafanyakazi hao wamekuwa wakishiriki kutoa hati feki za kusafiria, kuvusha dawa za kulevya na nyara za Serikali, jambo ambalo alionya kuwa hatalivumilia kwa kuwa linaitia doa nchi kimataifa. Siku chache baada ya onyo hilo, wanawake hao wawili, mmoja Mnigeria na mwingine Mliberia walikamatwa kwa nyakati tofauti wakiwa na dawa hizo wakiwa njiani kwenda nje.
Kukamatwa kwa wanawake hao kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alipopigiwa simu na gazeti hili kuthibitisha tukio hilo.
Vyanzo vya habari vilisema wa kwanza kukamatwa alikuwa raia wa Liberia, aliyekuwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo tano akiwa tayari kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Addis Ababa nchini Ethiopia saa 9 usiku.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, mwanamke huyo raia wa Liberia alionekana hajiamini kupita kiasi na alipokaguliwa, alikuwa na mzigo huo uliokuwa umefichwa kwa ustadi katika mabegi yake kwa kushoneshwa kwa ndani.
Mwanamke mwingine raia wa Nigeria alikamatwa na kilo 10 za dawa hizo saa 11 alfajiri jana akitaka kusafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Precision kwenda Nairobi nchini Kenya.
Habari zilisema kuwa raia huyo wa Nigeria, alikuwa na mabegi kama ya raia huyo wa Liberia, hali iliyosababisha atiliwe shaka kuwa huenda anafahamiana na mwenzake ingawa walikuwa wapande ndege tofauti. Kamanda Boaz alisema kwa sasa wanawake hao wako chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano na atakuwa tayari kutaja majina ya watuhumiwa leo.
“Siko ofisini lakini tukio hilo lipo na majina ya watuhumiwa nitayataja kesho (leo) kwa kuwa kila kitu kipo ofisini… kuwa na subira,’’ alisema.
Inadaiwa baada ya Serikali kuimarisha ulinzi na kuwabana wasafirishaji dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara hao walianza kutumia KIA kusafirishia dawa hizo haramu.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa KIA, Bakari Murusuri alipokuwa akizungumza katika kikao cha Dk Mwakyembe, alisema kati ya Machi hadi Oktoba, mwaka huu, watu watano wamekamatwa wakisafirisha dawa za kulenya aina tofauti, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Mwandishi ni John Mhala, Arusha.
Source: Habarileo
 
Yani toka tupate uhuru Kia nimesiki leo inamaana zigo lishapita sana pale eh eh mungu wangu kizazi cha nyoka
 
Back
Top Bottom