Shaka ataka wachapakazi wabaki makao makuu UVCCM

Nov 30, 2016
7
14
Na Mwandishi Wetu,

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka watendaji na watumishi wa Makao Makuu ya jumuiya hiyo kuanza kujipima, kujitathmini na kujipanga upya kimamakati kwa sababu muda wa kupiga maneno haupo ila vinavyohitajika ni uwezo binafsi na vitendo.

Pia umoja huo umewasisitiza watendaji , wahudumu na watumishi wa jumuiya hiyo kuongozwa na msingi ya nidhamu, uwajibikaji kazini na kuacha tabia za mzaha na masikhara wakati wa kazi.

Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka alitoa maelezo hayo jana alipokutana na kufanya kikao na watumishi wa UVCCM Makao Makuu kwa ajili kutathmini utendaji wa jumuiya kwa mwaka 2016 na kupanga mikakati ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2017.


Shaka alisema pamoja na kusikiliza michango , maoni , ushauri , mawazo na changamoto zinazowakabili watumishi na namna ya kuzitatua kwa mwaka 2017 lazima uwe mwaka wa vitendo na mafanikio.

"Tutabadili kila kona yenye kasoro au dosari , lengo si kukomoana ila ni katika kujipanga tena upya, asiyeweza aseme hawezi ili akae kando , kama mtu hajimudu hatapewa dhamana yoyote kwasababu ya ushikaji na urafiki "Alisema Shaka.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema makao makuu inahitaji kuwa kama kioo, sifa ya kioo ni kujiona na kujitambua, kama umechafuka jisafishe ili uwe nadhifu na makini bila mtu kusukumwa.

Alisema kila aliyepangiwa kazi yake aifanye kwa mujibu wa hadidu za rejea na maelekezo ya kikanuni hivyo asiyetaka kujituma na kutimiza wajibu wake atakuwa haitakii mema jumuiya na hivyo hatavumiliwa na kutazamwa.

"Tukijipanga vyema hapa Makao Makuu, kila mmoja akatimiza wajibu wake naamini mambo yakaenda kama inavyotakiwa, hakuna urasimu wala njoo kesho, wenzetu wilayani na mikoani watatueheshimu, tukiwatuma watatumika na kutupatia majawabu chanya "Alieleza

Hata hivyo Shaka aliwataka wana jumuiya mahali popote walipo nchini wajione na kujihesabu wao ni ndugu wa tumbo moja, wapendane, wasikubali kukaribisha majungu au hasama kwasababu zama hizo zimepita na hazitarejea tena.

Pia aliwakumbusha watendaji hao wa makao makuu kutunza siri za ofisi, nyaraka muhimu ikiwemo na kujiandaa vyema kufanikisha uchaguzi Mkuu ujao kwa mujibu wa taratibu, kanumi na katiba ya ccm.

"Ukipewa jukumu la kusimamia tenda haki, timiza wajibu wako bila upendeleo, ukiharibu na kuvurunda utaadhibiwa bila huruma na si hasha ukajifukuzisha kazi mwenyewe kwa ukiukaji wako wa maadili na kanuni ya utimishi"alisisitiza Shaka .

Kaimu huyo Katibu Mkuu alimsifu na kuwashukuru Mwenyekiti wa UVCCM sadifa Juma Khamis, Makamo Mwenyeliti Mboni Mhita , manaibu makatibu wakuu wake, wakuu wa idara na watendaji wote wa jumuiya hiyo kwa kumpa ushirikiano katika kutimiza majukumu na kuifanya jumuiya yao kuendelea kukamilisha mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutawala.
 
Back
Top Bottom