SHAIRI: TANGA KUNANI? In Michuzi- 03/03/12 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

SHAIRI: TANGA KUNANI? In Michuzi- 03/03/12

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Dopas, Mar 4, 2012.

 1. D

  Dopas JF-Expert Member

  #1
  Mar 4, 2012
  Joined: Aug 14, 2010
  Messages: 1,151
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Kwa jina la Rahmani, Mola aso na mfano,
  Naingia uwanjani, kwa beti kumi na tano,
  Lengo langu si utani, wala mengi malumbano,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Wakati wa kampeni,viwanja vya Tangamano,
  Tulipokea ugeni, wa ‘bosi' wa Muungano,
  Akatutoa huzuni, Tanga mambo ni ‘mswano',
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Viwanda kama Amboni, vilikuwepo zamani,
  Mabasi na matreni, sambamba kuwa njiani,
  Leo katiza relini, hata husikii honi,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Tulikuwa na ‘Mbolea', njia ya Raskazoni,
  Wazazi waliponea, mkono kwenda kinywani,
  Wapi kimepotelea, kiwanda hiki jamani?
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Mji watoa matunda, mkonge hata korosho,
  Vipi ukose viwanda, ewe mwana wa Mrisho?
  Muagize japo Pinda, afanye matayarisho,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Tanga tunayo bandari, nzuri na ya kuvutia,
  Meli zije kwa fahari, tupate pa kushibia,
  Ukitupatia feri, Unguja twaenda pia,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Bandari kuu ni Dar, ya Tanga imedorora,
  Meli huko zimejaa, hadi yatia hasira,
  Zinachelewa bidhaa, kuzitoa ni hasara,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Reli ya kwenda Uganda, nayo naikumbushia,
  Mbao huko zinakwenda, tatizo ni hiyo njia,
  Vipi na mama Makinda, bungeni aigusia?
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Mazuri nayasifia, msiseme tu ni kero,
  Mradi wa Milenia, Tanga kwenda Horohoro,
  Bara bara yanyinyia, yashinda hata ya Moro,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Na wale wawekezaji, nawakaribisha Tanga,
  Mji wetu una maji, yeyote hawezi pinga,
  Mzuri kwa ufugaji, uvuvi hata wa tenga,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Tuna mawe kiomoni, na samaki baharini,
  Machui na Maforoni, fukwe nzuri kama nini!,
  Tafadhali wekezeni, Tanga ni nambari wani!,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Tanga pia kuna chumvi, kaoneni Kisosora,
  Twatengeneza majamvi, ila soko ladorora,
  Twavua hata uduvi , na kuuza Makorora,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Ninakuomba Kikwete, Rais wa Tanzania,
  Ahadi zisiwe tete, Tanga tutakulilia,
  Najua huwezi zote, japo mbili kazania,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Tanga ni maendeleo, si kuja kurudi leo,
  Tupatieni koleo, tufyatue pembejeo,
  Kamwe hatutaki vyeo, ukoloni mambo-leo!
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Beti ninakamilisha, nisije nikawachosha,
  Ujumbe nimefikisha, Mtanga nimejikosha,
  Wakuu wasijebisha, eti sikuwakumbusha,
  Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.

  Mwamgongo,Mwenyeji wa Tanga2 / Machi / 2012

  My take: Shairi nzuri sana. Namsifu Mtunzi wake.
  Lakini maeneo yote ambayo wanaona kofia, kangha na skafu za ccm ni mali wasahau mabadiliko. Ahadi wazisikie, hata ikiwa ni ya kugeuza "Kigoma kuwa Dubai". Tanga ni mojawapo ya maeneo hayo, ambayo wanadhani ccm ni mama yao. Wabaki walie tu....
   
 2. U

  Uwezo Tunao JF-Expert Member

  #2
  Mar 4, 2012
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 6,947
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Jamani, JF kweli ni kila kitu. Hongera kwa malenga wetu hawa akiwemo Mzee Mwanakijiji na kazi ya ufikishaji wa ujumbe kwa njia ya kutumia chombo hiki cha sanaa; mashairi.

  Hakika mnanikonga sana moyo kwa kuweka lugha yetu ya Kiswahili mbeeele kama tai pale ambapo wengine wanaonyesha kulionea aibu kulizungumza hadharani hata akakamilisha ujumbe wake bila ya kunyunyizia KIDHUNGU katikati eti kwa kuonyesha msisitizo wa kuonekana msomi zaidi.
   
Loading...