Shairi: Nawasihi kina dada (ushauri)

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,498
40,046
Sitaupoteza muda, ninalo la kuusia,
Hasa kwenu kina dada, ninyi wa Kitanzania,
Nilisemalo si ada, bali onyo na wosia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Aloupanda jirani, acha kuutamania,
Usijifanye mhuni, ndizi ukajichumia,
Mwenyewe asibaini, kuna mtu aibia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Mgomba huo ni wake, wewe ukauvamia,
Ukazila ndizi zake, bila yeye kujulia,
Kwa kicheko na makeke, ndizi wazifakamia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Utamu wa ndizi hizo, wewe ukazisifia,
Ukasema si mchezo, ndo maana wajilia,
Miye ninakupa funzo, hizo ndizi achilia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Ni ndefu tena ni nene, ndizi wazishangilia,
Katika chani zione, zilivyojipangalia,
Hata ziwe nchi nane, wewe wazitamania,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Wazishika mkononi, wazimenya kwa hisia,
Asubuhi na jioni, shamba lake waingia,
Wewe wala huna soni, ndizi wajitungulia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Ewe binti wa kibongo, miye ninakuusia,
Uache yako maringo, jirani wamuudhia,
Ufanye wako mpango, ndizizo kujilimia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Kilo chako ukishike, cha jirani kuachia,
Sifa yako mwanamke, vya kwako kushikilia,
Utampiga mateke, mwingine akivamia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

Nimefikia kikomo, beti nakuandikia,
Kwako hili liwe somo, hekima kukupatia,
Bila kuleta mgomo, ndizi hizo achilia,
Mgomba huo si wako, acha kula ndizi zake.

M.M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
 
naona dhamira kuu katika hili shairi lako ni kuwapa ushauri kina dada waepukane na waume za watu.

imetulia,

we mwanakijiji si mchezo kama mshahiri,
 
Mimi sasa Jambo forum sisomi tena upuuzi wa kina chenge, nasoma tu mashairi naburudika na malenga
 
anachokifanya mwanakijiji ni kutuburudisha tu,pia kutoa mafunzo kwa jamii husika.

ila lile lengo lingine la wana jf yaani kutokomeza ufisadi speed bado ile ile 120km/s

ndio mwanakijiji sasa njoo la shairi la mafisadi.
 
MMkjj sasa kama huo MKUNGU upo barazani mwangu? Maana saa nyingine nao MGOMBA hulemewa na MKUNGU kutua kwa JIRANI
 
natumaini ni burudani tosha... kile kisa kingine cha Mapenzi kwa Ijumaa hii kiko njiani...
 
Sitaki kuwa shabiki, wa hoja kuparamia
Kuna kitu nasadiki, si kwa ndizi hata bamia
Ndizizo hazishikiki,ka kuku anaetamia
kwa vitenge na batiki,ndizi itatumia

Migomba mingine jamani,Inasinzia shambani
Ndizi zabaki tamani,Kujitupa uwanjani
Utakuta ndizi njiani,Zishakimbia shambani
Ndizi zanunua jamani,He!! haya si ya firauni?
 
Sishauri wale ndizi
Migomba ndiyo iache uchizi
Kama usipochunga mwizi
Basi utaenda Omo na tezi
Mgomba wahsa lako kurunzi
Shime kuna wezi wakufunzi

Kina dada ndizi zinashawishi
Kuna nyingine zina utashi
Zaja na pesa kama moshi
Na gari za joji bushi
Usipojawa utashi
Utashangaa kama burushi
 
Mkkj nakupa kudo kwa mashairi,hebu tunga la kina baba wanaosarandia wake wa wenzao ao wasichana wadoogo!
Unaendeleaje jirani,nimekumiso!!!!
 
Zee la shamba kazoza, kwa hao akina dada
Tena pia akabeza, kwa wizi wa hao dada
Wala tena hakusaza, kuponda kama akida
Enyi ndugu kinadada, zee la shamba kazoza!

Sikieni kwa makini, kwa kina amehubiri
Muache usheitwani, onyesheni ujasiri
Na wala siyo utani, kakasirika ngangari!
Enyi ndugu kinadada, zee la shamba kazoza!

Usia huo wa bure, mwenyewe kawaambia
Hataki mcheze shere, sherehe ya kuibia
Bukoba hadi ukwere, ni wote kawakemea!
Enyi ndugu kinadada, zee la shamba azoza!
 
Asante Mwanakijiji, mbali ya usia kwa kina dada pia ni burudani. Nimesoma shairi naona nikapumzike niweze kulitafakari na kuliendeleza kuanzia ulipoishia.
 
mwanakijiji hiyo imetulia ila iko kwa wanawake
tupe la kuwabana wanaume wanaokimbilia waume z watu wapo wala si la kushangaza ukimaliza tumwagie wanume wanaiba wake za watu ...ila naliitaji hili la wanaume wanaokula waume za watu na zambi zao...
 
Mwanakijj,
Haya mashairi yako yataka ufafanuzi, kwani tafsida na pia takriri kibao, ila hongera
 
Back
Top Bottom