Shairi: Mzungu na mwaarabu mbaya wetu ni nani

kaligopelelo

JF-Expert Member
Jun 20, 2013
2,761
3,938
1.Alianza mwaarabu,kutafuta mali zetu
Kupitia marikebu,akafika pwani zetu
aliwakuta mababu,wakinena lugha zetu
Mzungu na mwaarabu,mbaya wetu ni nani?

2. Akauza zake shanga,vikombe na mabirika
Wateja wakajipanga,vitu vingi walitaka
Wakarudi kujipanga,wakabeba na mikeka
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

3. Maeneo wakateka,wakapanda karafuu
Mababu walitumika,kukwea minazi juu
Na pembe walizisaka,za ndovu na zake faru
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

4. Wakaanzisha masoko,utumwani wakaenda
Wakacharazwa viboko,na melini wakapanda
Kukataa kwao mwiko,bunduki inawalinda
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

5. Aliwepo tiputipu, huruma kwake dharura
Hata kama unajipu,akikwona atafura
Kuua kwake ni supu,hakuna kwake kafara
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

6. Wazungu nao wakaja,wakaligawana bara
Mali zetu wakafuja,wakatia na hasara
Wakajipanga kwa hoja,ili tuwe mafukara
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

7. Wakanunua watumwa, kutoka kwa mwaarabu
Migodini walitumwa,wakatafute dhahabu
Na chakula walinyimwa,maisha yakawa tabu
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

8. Watu walidhalilishwa,wakawekwa mazizini
Kwa pesa walioneshwa,wakafanywa kama nyani
Ngozi ikaguswaguswa,rangi ili kubaini
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

9. Na damu zikamwagika,mateso yalipo zidi
Uhuru wakautaka, heshima Yao irudi
Risasi zikasikika,zikaua na wahindi
Mzungu na mwaarabu, mbaya wetu ni nani?

10. Uhuru tukaupata,kwa chozi jasho na damu
Wazalendo tukapata,walopinga wahujumu
Tamaa walipokata,wakatuua kwa sumu
Mzungu na mwaarabu,mbaya wetu ni nani?

11. Kalamu naweka chini,mpate kutafakari
Mengi mmeyabaini, kwenye vyombo vya habari
Ubaguzi wa rangini, duniani wakithiri
Mapigano mauaji,vifo vingi chanzo wao

12. Akili tuzishikeni,tuutafute ukweli
Mengi yako mafichoni,kutupumbaza akili
Tusome ya vitabuni,tuulize na maswali
Mababu wahadithie,mengi wao wameona
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom