Na Mashaka Mgeta
23rd February 2010
B-pepe
Chapa
Maoni
Andrew Chenge
Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya jinai nchini Uingereza (SFO), imesema utaratibu wa kurejesha vijisenti vya Tanzania vinavyotokana na kashfa ya rada, unategemea uamuzi wa Majaji nchini humo. Hayo yamo katika taarifa ya Ofisa Habari wa SFO, David Jones, aliyoituma kwa mwandishi wa habari wa gazeti hili kwa njia ya mtandao.
Jones alisema maelezo kuhusu shauri la SFO dhidi ya kampuni ya BAE System kuhusiana na mkataba uliofikiwa na Tanzania, bado hayajawasilishwa katika mahakama ya wazi jijini London.
Alisema baada ya kukamilisha uchunguzi wao, kitengo kinachohusika kitawasilisha shauri hilo mbele ya majaji ambao wataamua jinsi kiasi cha Paundi milioni 30 kitakavyolipwa na BAE System.
Jones alisema fedha hizo zinajumuisha malipo ya faini na fidia kwa Tanzania. Kwa mujibu wa Jones, shauri hilo litasikilizwa katika mahakama ya Southwark Crown iliyopo katikati ya Jiji la London.
Tarehe ya kuanza kusikiliza shauri hili bado haijathibitishwa na mamlaka za huduma katika mahakama hiyo, alisema.
Jones alisema hivi sasa SFO haiwezi kuzungumzia kwa kina masuala yaliyoulizwa na Nipashe na kwamba hata baada ya uamuzi kutolewa, watagusia maeneo yatakayoamuriwa na majaji.
Ninaamini utaelewa muingiliano wa kisheria uliopo katika sakata hili, alisema Jones katika taarifa hiyo.
Katika maswali yake Nipashe, pamoja na mambo mengine ilitaka kujua mamlaka ya kisheria ya SFO katika kudhibiti taasisi yoyote kwa kushindwa kuhifadhi kumbukumbu vizuri, kama ilivyodhihirika kwa BAEs System.
BAE wamekubali kulipa fidia hiyo kama njia ya kufikisha hitimisho kesi ya rushwa iliyokuwa ikiwaandama, ikiangaliwa kama mbinu ya kukwepa kitiwa hatiani mbele ya safari kwa kesi kubwa ya rushwa ambayo ingekuwa na madhara makubwa zaidi kwake kibiashara duniani. Badala yake BAE waliafikiana na SFO kukiri kosa la uzembe wa kutokuweka kumbukumbu sahihi jinsi kamisheni ya ununuzi wa rada ya Tanzania ilivyogawanywa kwa madalali mbalimbali.
Pia Nipashe ilitaka kupata taarifa za viashiria vya rushwa katika hatua zote zilizofanikisha kusainiwa kwa mkataba na hatimaye ununuzi wa rada hiyo iliyoigharimu Tanzania Dola za Marekani milioni 60.
Kwa upande mwingine, Nipashe iliuliza kuhusu hatma ya uchunguzi wa akaunti ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, huko Jersey, Uingereza na jinsi inavyohusiana na kashfa ya rada.
HOJA YANGU: Watanzania PCCB wanasubiri Ushahidi gani zaidi?