Serikali za Mitaa:Vyama vya upinzania vyaanza kujichimbia mizizi

paesulta

JF-Expert Member
Mar 13, 2009
227
29
Date::10/26/2009
Serikali za Mitaa: Makamba ashindwa kumzima Dk Slaa Karatu
Na Waandishi Wetu

MATOKEO ya awali ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi nchini kote, yanaonyesha kuwa vyama vya upinzani vimeanza kupata nguvu kubwa baada ya kujipenyeza sehemu mbalimbali na kukibwaga chama tawala, CCM.

Pamoja na kuwa CCM, imeibuka mshindi sehemu mbalimbali, vyama vya upinzani vimeonekana kuja kwa kasi maeneo ya Kigoma, Kilimanjaro, Shinyanga, Arusha ambako vimeongeza idadi ya viti tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, huku vikichukua mitaa katika baadhi ya maeneo ambako upinzani ulikuwa haujawahi kushinda.

Mkoani Kilimanjaro, Chadema ilipata viti 21 (sawa na asilimia 35) katika Manispaa ya Moshi, hali iliyoonyesha kuwa imeongeza idadi kwa zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na mwaka 2004 wakati chama hicho kilipopata viti nane tu.



Matokeo yaliyopatikana kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi katika manispaa hiyo, yanaonyesha kuwa CCM imejinyakulia mitaa 35, sawa na asilimia 65.



Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema alisema pamoja na matokeo hayo kutokidhi matarajio yao, yameonyesha wazi kuwa chama hicho kinakubalika kwa wananchi.



Akizungungumzia kwenye Jimbo la Vunjo, Lema alisema wamepata vijiji 13 na vitongoji 34 tofauti na mwaka 2004 ambapo chama hicho kilipata vijiji viwili na vitongoji vitatu.



Katibu wa CCM wilayani Moshi Vijijini, Cosmas Kasangani alisema katika uchaguzi huo CCM imejinyakulia viti 103 katika jimbo hilo, huku upinzani ukipata viti 37.



Katika Wilaya ya Same, CCM imepata viti 89, Chadema (kimoja) sawa na PPT-Maendeleo.

Mkoani Arusha, CCM imefanya vibaya katika mji mdogo wa Karatu baada ya kupata viti sita tu, huku Chadema ikinyakua viti 21.

Matokeo hayo yanaonekana kuwatia hofu viongozi wa CCM mkoani Arusha, ambao baadhi yao walianza kuondoka juzi usiku mara tu baada ya kutangazwa matokeo ya Karatu, eneo ambalo chama hicho tawala kiliweka kambi na ambako Katibu Mkuu Yusuf Makamba alizindulia kampeni zao.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa mji huo, kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, Clemence Berege alisema uchaguzi huo ulishirikisha wakazi wa kata mbili za Ganako na Karatu Mjini.

Berege alisema kati ya vitongoji (mitaa) 28, Chadema imeshinda viti 21, CCM viti 6 na NCCR- Mageuzi kitongoji kimoja, ambacho mgombea wake, Peter Sanka alipita bila kupingwa baada ya wagombea wa Chadema na CCM kujitoa.

Katika matokeo mengine, Chadema imeendelea kuongoza kwa kushinda vitongoji 71 na CCM ikiwa imeshinda vitongoji 54 pekee. Hadi jana jioni matokeo ya vitongoji vingine 77 yalikuwa hayajatangazwa.

Katika uchaguzi wa vijiji, Chadema pia ilikuwa inaongoza kwa kushinda vijiji 12 dhidi ya 11 vya CCM, huku matokeo ya vijiji vingine 21 yakiwa hayajatangazwa.

Katibu wa Chadema wilayani Karatu, Laurent Bother alisema matokeo yaliyotangazwa yanaonyesha wameongeza viti vya vijiji na vitongoji tofauti na uchaguzi uliopita.

"Katika ule uchaguzi tulikuwa na vitongoji 74 pekee, lakini hadi sasa tuna jumla ya vitongoji 98 na bado matokeo ya vitongoji 67 hayajatangazwa na tulikuwa na vijiji 16 na hadi sasa tuna vijiji 12 na bado tuna taarifa ya kushinda vijiji 10 vingine kati ya 15 ambavyo matokeo bado," alisema Bother.

Mkoani Mbeya wagombea wa CCM katika maeneo mengi walipita bila ya kupingwa, lakini matokeo ya awali yanaonyesha Chadema kimefurukuta kwa kuzoa viti vingi hasa vijijini, ukilinganisha na mwaka 2004.



Katika uchaguzi wa mwaka 2004 Chadema ilishinda viti 36 kwa mkoa mzima, lakini taarifa za matokeo ya awali zinaonyesha imeshazoa viti zaidi ya 60 kwa baadhi ya halmashauri za wilaya kwa ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa.



Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mbeya, George Mtasha alisema mpaka sasa chama chake kimeshinda viti vingi tofauti na mwaka 2004 na kwamba, wanatarajia kupata viti vingine baada ya matokeo yote kutangazwa.



Alisema wilayani Chunya mpaka jana saa tisa mchana, Chadema ilikuwa imeshinda viti 32 kwa matokeo ambayo yalishawasilishwa wilayani.



Wilayani Kyela, matokeo yanaonyesha kuwa CCM imeshinda nafasi ya wenyeviti wa vijiji 88 huku Chadema ikiambulia kimoja, wakati CCM imezoa viti 361 vya vitongoji huku Chadema ikipata viti saba na TLP viti viwili.

Katika Halmshauri ya Jiji la Mbeya, CCM imeibuka kidedea kwa kushinda mitaa 169. Matokeo ya mitaa mingine minne bado hayajatolewa na chaguzi za mitaa miwili zitarudiwa.



Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Peter Bitware alisema CCM imenyakua mitaa mingi ikifuatiwa na Chadema (6) na NCCR – Mageuzi (1).



Mkoani Mara, CCM imepata ushindi mkubwa katika Wilaya za Tarime na Rorya baada ya kushinda viti 57 vya vijiji kati ya 78, huku Chadema ikizoa viti 17.

Katika mji wa Tarime, CCM ilishinda viti na mitaa 10 kati ya 14, lakini ushindi wa kitongoji cha Mwangaza unalalamikiwa kutokana na karatasi 46 za kura kuandikwa CCM badala ya jina la mgombea.

Matokeo ya awali wilayani Rorya yanaonyesha CCM inatwaa vitongoji 312 kati ya 435 huku matokeo ya kata nne yakiwa bado kuwasilishwa.

Mkoani Kigoma, matokeo ya awali ya uchaguzi kwenye vijiji 33 vilivyo Jimbo la Kigoma Kaskazini yanaonyesha CCM imeshinda vijiji 16 na kufuatiwa na Chadema (12). Matokeo ya vijiji vitano bado. Mwaka 2004, CCM ilishinda vijiji 31 na Chadema viwili tu.

Katika Jimbo la Kigoma Kusini ambalo lina vijiji 43, CCM imeshinda vijiji 17, Chadema (8), NCCR-Mageuzi (8), CUF (2) na matokeo ya vijiji nane bado hayajapatikana. Mwaka 2004, CCM ilishinda vijiji 16 na upinzani 27.

Mkoani Shinyanga, kambi ya upinzani imejipatia viti 12 dhidi ya 63 vya CCM hivyo kushangaza wadadisi wa mambo ya uchaguzi kwa ushindi huo kwa mara ya kwanza tangu uanze mfumo wa vyama vingi. Upinzni haujawahi kupata kiti chochote.

Matokeo yaliyokusanywa kutoka kwa katibu wa CUF wa wilaya, Said Sizya na pia katibu wa CCM wa mkoa, Mohammed Mbonde na ofisi ya msimamizi wa uchaguzi, Chadema wameshinda katika Kata ya Ndala na CUF kijiji cha Mwamalili kwa nafasi za wenyeviti.

Katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, CCM imejipatia viti 604 na upinzani 13 na wilayani Kahama vyama vya upinzani vimejizolea viti 22 dhidi ya 948 vya CCM.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bukombe, Kelvin Makonda alisema kuwa kati ya vitongoji 582, CCM imeshinda vitongoji 572 ambayo ni asilimia 98.2 na wapinzani yaani CUF wameshinda vitongoji (8) na Chadema (2) sawa na asilimia 1.7.

Hata hivyo, katika matokeo ya jumla CCM imetwaa nafasi 97 na upinzani nane katika jimbo hilo ambalo ni ngome ya chama hicho na ni mara ya kwanza kwa upinzani kushinda viti, jambo linaloashiria kuanza kushuka umaarufu kwa chama tawala kwenye eneo hilo.

Pamoja na uchaguzi huo kumalizika jana, polisi katika mikoa mbalimbali inawashikilia baadhi ya watu kwa kufanya vurugu.

Mkoani Dar es Salaam, Jeshi la Polisi linawashikilia watu 18 kwa kukiuka sheria mbalimbali za uchaguzi wa serikali za mtaa uliofanyika nchi nzima Oktoba 25.

Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, SACP Sulemani Kova alisema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika vituo mbalimbali kutokana na makosa mbalimbali.

Mkoa wa Pwani, watu watano wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya fujo katika maeneo mbalimbali ya vituo vya uchaguzi, likiwemo tukio la mtu mmoja kupiga teke sanduku la kupigia kura na kupasuka hatimaye kura kumwagika.



Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi uliofanyika juzi, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma alisema tukio hilo limetokea kijiji cha Mgomba, Kitongoji cha Kingwande wilayani Rufiji baada ya David Malecela, 41, kufanya fujo hizo na kusababisha uchaguzi huo kusitishwa ukisubiri tarehe nyingine.

Kamanda wa Kanda ya Tarime na Rorya, Costantino Massawe alisema jeshi lake linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kufanya vurugu wakati wa uchaguzi na watafikishwa mahakamani.

Mkoani Shinyanga, mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu wakati wa uchaguzi huo.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Daudi Siai aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtu huyo, Liswa Saguda, 32, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nkololo wilayani Bariadi aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani.



Habari hii imeandikwa na Rehema Matowo, Mussa Juma, Brandy Nelson, Julieth Ngarabali, Suzy Butondo, Samson Chacha, Jackson Odoyo na Hadija Jummane.
 
Back
Top Bottom