Serikali yaweza kulipa Sh. 315,000 ikisitisha matanuzi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali yaweza kulipa Sh. 315,000 ikisitisha matanuzi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Magezi, May 18, 2010.

 1. M

  Magezi JF-Expert Member

  #1
  May 18, 2010
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  Gazeti MwanaHalisi

  RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali haina uwezo wa kulipa kima cha chini cha mshahara wa Sh. 315,000 kwa watumishi wake.

  Anasema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa ikilinganishwa na mapato ya serikali. Alitaka wafanyakazi wasioweza kufanya kazi kwa mshahara wa sasa wa Sh. 104,000 kwa mwezi, kuondoka ili kupisha wengine.

  Akiongea kwa sauti na kauli iliyojaa vitisho, Kikwete alisema, “Hata kama wafanyakazi watagoma miaka 10 hawataweza kupata wanachokidai.”

  Kikwete alitoa kauli hiyo wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, alipozungumza na wazee wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

  Kauli ya Kikwete ilikuja kufuatia Shirikisho huru la Wafanyakazi (TUCTA) kuchagiza serikali kulipa watumishi wake mshahara wa Sh. 315,000 kwa mwezi ikisema angalau zinaweza kukidhi mahitaji ya maisha kwa sasa.

  Je, kauli ya Kikwete kwamba serikali haina uwezo wa kulipa wafanyakazi wake kiasi hicho cha fedha kinachotakiwa na TUCTA ina ukweli kiasi gani?

  Jibu liko wazi, kwamba serikali inaweza kulipa si Sh. 315,000 zinazodaiwa na wafanyakazi, bali inaweza kulipa hata Sh. 400,000 kwa mwezi kwa mfanyakazi wa kima cha chini.

  Kinachotakiwa ni umakini katika ukusanyaji wa kodi, ugawaji sawa wa pato la taifa, kupungua kwa ukubwa wa serikali na kutumia kidogo kinachopatikana kwa maslahi ya wengi.

  Lakini katika mazingira ya sasa ya ukwepaji kodi uliokubuhu, matumizi yasiyo na msingi ya viongozi wa serikali, upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi, serikali haiwezi kulipa hata robo ya kile kinachodaiwa.
  Kwa mfano, wakati serikali inasema haina fedha za kuwezesha kulipa kima cha chini cha Sh. 315,000 kwa watumishi wake kwa mwezi, ni serikali hiyohiyo inayolipa kila mbunge mshahara wa Sh. 1.9 milioni kwa mwezi.

  Mbali na mshahara huo, mbunge analipwa mafao mengine kadha wa kadhaa ambayo hayakatwi kodi yanayofikia karibu Sh. 6 milioni kila mwezi.

  Vilevile mbunge wa Bunge la Jamhuri analipwa posho ya Sh. 210,000 kwa kila siku za mkutano wa Bunge au wakati mikutano ya Kamati za Bunge.

  Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri, Bunge linakutana siku 167 kwa mwaka kati ya siku 365. Kwa hesabu hizo mbunge wa Bunge la Jamhuri anachota katika mfuko wa taifa kitita cha zaidi ya Sh. 148.6 milioni kwa mwaka.

  Mbali na mtunga sheria huyo kulipwa mamilioni yote hayo ya shilingi, serikali inampa mkopo wa Sh. 80 milioni kununulia gari mara baada ya kuapishwa.

  Akimaliza kipindi chake cha miaka mitano, serikali inamlipa kiinua mgongo kinono. Kwa mwaka 2005 kila mbunge alilipwa kiasi cha Sh. 45 milioni; mamilioni hayo ya fedha huwa hayakatwi kodi.

  Hiyo ni nje ya malipo ya fedha za kuhudhuria semina, warsha na makongamano ya kila Jumamosi mjini Dodoma wakati wa mkutano wa Bunge.

  Hata akirejea bungeni mara tano, bado mamilioni hayo ya fedha yataendelea kummiminikia.
  Bunge la sasa la Jamhuri lina wabunge 325 na tayari serikali imetangaza kuongeza majimbo mapya saba katika uchaguzi ujao. Nyongeza hiyo italifanya taifa kuhudumia wabunge 332.

  Mbali na hilo, Bunge linahudumia matibabu ya ndani ya kila mbunge pamoja na familia yake isiyopungua watu wanne.

  Serikali inamlipa kila mbunge lita 1000 za mafuta kwa ajili ya matumizi ya gari lake binafsi kwa hesabu ya kila lita Sh. 2500.

  Pamoja na kwamba serikali inajua kuwa hakuna mahali popote katika taifa hili ambako mafuta ya petroli au dizeli yamefikia Sh. 2500 kwa lita, serikali ya Kikwete inaendelea kulipa mamilioni hayo ya fedha kwa kila mwezi.

  Kwa mafuta pekee, serikali inatumia Sh. 9,750,000,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuhudumia wabunge pekee.

  Hawa ni wabunge. Nje ya Bunge kuna orodha ndefu ya watumishi wa umma ambao serikali inabeba gharama kubwa kuwahudumia – kuwalipia malazi, posho ya kuhudumia wageni na papohapo ikiwalipa mamilioni ya shilingi wakiwa kazini.

  Kwa mfano, wakati mbunge anakopeshwa gari lenye thamani ya Sh. 80 milioni, waziri na naibu mawaziri ambao nao ni wabunge, wanakopeshwa gari lenye thamani ya Sh. 120 milioni.

  Wanahudumiwa kwa matibabu, wanapewa nyumba za kuishi na kila waziri anatengewa katika bajeti yake, fedha za kutembelea jimbo. Fedha hizo ni nje ya zile zinazolipwa na bunge kwa kila mbunge akiwamo waziri.

  Hao ni mawaziri na naibu wao. Lakini kuna makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakurugenzi na makamishina. Baadhi ya wizara zina wakurugenzi hadi watano. Wote hawa wanalipiwa na serikali, nyumba, gari na matibabu.

  Orodha ni ndefu. Kuna wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa. Nao, kama ilivyo kwa wabunge, wanahudumiwa na serikali kwa kila kitu.
  Kuna taarifa kwamba mshahara wa wakuu wa wilaya waliotapakaa nchi mzima na ambao kazi zao hazijulikani wazi, una hadhi sawa na ule wa mbunge.

  Nao wanahudumiwa na serikali kwa kupewa magari, madereva na nyumba zilizojaa thamani. Wengi wa watumishi wa serikali huyatumia magari hayo kwa shughuli binafsi na Rais Kikwete analijua hili, lakini hajalisemea.

  Hiyo ni tofauti na watumishi wa kawaida serikalini. Huyu anakamuliwa hadi damu. Hana mkopo wa gari. Hana mafuta ya kuendeshea gari lake kwa wale wachache waliobahatika; wala hana uhakika wa matibabu yake na familia.

  Mfanyakazi akimaliza muda wake wa utumishi serikalini, atalazimika kusotea malipo yake ya uzeeni kwa miaka nendarudi. Wengine wanafikwa hadi na mauti bila kuambulia mafao yao.

  Lakini si hivyo tu, wakati serikali inakondesha mfanyakazi wake kutokana na kumlipa kiduchu, mtumishi wa mifuko ya wafanyakazi – NSSF, PPF na mingine – analipwa si chini ya Sh. 500,000 kwa mwezi.
  Wakati wafanyakazi hawa wanaendelea kusotea malipo yao ya uzeeni kutokana na sheria kandamizi za mifuko ya wafanyakazi, wafanyakazi wanaofanya kazi katika mifuko hiyo, wanalipwa mara tu wanapostaafu.

  Wakati Kikwete anasema serikali yake haina uwezo wa kulipa wafanyakazi mshahara angalau unaoweza kufika tarehe 30 ya mwezi unaomalizika, kuna taarifa kwamba kuna mpango wa kuongeza wilaya mpya na hata mikoa mipya kabla ya mwaka 2012. Hivi sasa, kuna wakuu wa wilaya 123 na mikoa 26.
  Mbali na wakuu wa wilaya, kuna idadi kubwa ya watendaji wengine wa serikali – maofisa utumishi wa wilaya, makatibu tawala, maofisa usalama wa taifa, maofisa wa kilimo na mifugo, misitu na nyuki, maofisa wa shule za sekondari na msingi na hata maofisa mgambo wa wilaya, wote hawa wanahudumiwa na serikali kama vifaranga vya ndege.

  Katika mazingira haya, si kwamba serikali haina fedha za kulipa wafanyakazi wake mshahara unaokidhi mahitaji, bali ni kwamba nyingi ya fedha za serikali zinatumika kuhudumia kikundi kidogo cha wateule.
  Huwezi kuwa na maendeleo wakati serikali ni kubwa na haina ufanisi. Kodi hazikusanywi kama inavyotakiwa na kidogo kinachopatikana kinatumika vibaya.

  Kwa mfano, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha upotevu wa mabilioni ya shilingi za umma zilizotengwa katika bajeti ya kila mwaka zinatumika kwa matumizi ambayo hayakukusudia.

  Wizara kadhaa za serikali na mashirika yake zimekuwa zikipata hati chafu kutokana na kushindwa kusimamia fedha za umma.

  Kikwete analijua hili. Anajua kwamba baadhi ya watendaji wake wakiwamo mawaziri, si waadifu; wengine wanakabiliwa na lundo la tuhuma na wengine tayari walishaonyesha udhaifu wa uongozi huko nyuma.

  Rais anajua kwamba mamilioni ya shilingi za umma yanaishia kwa baadhi ya wafanyabiashara au watu walio katika mkondo wa utawala.

  Anajua kuwa fedha nyingi za serikali zinaishia kwa makampuni machache ya nje yanayoingia nchini kwa kisingizio cha uwekezaji; ambayo ama hutengenezewa mazingira ya kukwepa kodi na wale walioko madarakani au hupewa mwanya wa kukwepa kodi.

  Kwa mfano, ripoti ya Kamati ya Bunge ya Fedha za serikali ya mwaka 2007 inasema, hadi kufikia mwaka huo, makampuni ya nje ya madini yalikuwa hayajalipa kodi ya mapato ya zaidi ya dola 300 milioni (karibu Sh.400 bilioni).

  Haya yote Kikwete anayajua kwa kuwa alikuwa ndani ya serikali tangu enzi za utawala wa awamu ya pili ya rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi.

  Lakini hatujawahi kumsikia mahali popote pale, Kikwete akikaripia watendaji hawa wanaosababisha serikali kushindwa kulipa mishahara inayokidhi mahitaji ya watumishi wa umma kwa sauti ileile aliyoitoa kwa viongozi wa TUCTA.

  Kikwete anajua kuwa hospitali hazina dawa, hazina magari ya kubebea wagonjwa na hazina wataalamu wa kutosha wa afya.

  Rais anajau kuwa kila mwaka wananchi wanapoteza maisha kwa magonjwa yanayoweza kutibika na mengine kuzuilika; miongoni mwake yakiwa matatizo ya uzazi, kifua kikuu na malaria.

  Lakini badala ya serikali kutoa kipaumbele katika maeneo hayo, inajikita katika kuongeza majimbo ya uchaguzi na kugharamia safari zisizo na tija.

  Tayari kuna taarifa kwamba serikali ya Kikwete imeongeza fungu la posho za viongozi wake wanaosafiri kila kukicha kufikia Sh. 216 bilioni kutoka Sh. 171 billioni za mwaka wa fedha uliopita.

  Hili ni ongezeko la Sh. 45 bilioni ambazo zingeweza angalau kuongeza kima cha chini cha mshahara kinachodaiwa na wafanyakazi.
   
 2. Z

  Zebaki Member

  #2
  May 18, 2010
  Joined: Sep 25, 2007
  Messages: 43
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hii sio haki!!! Inasikitisha jinsi wafanyakazi wa kima cha chini wanavyoonewa!!!
   
 3. Bigirita

  Bigirita JF-Expert Member

  #3
  May 18, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 13,976
  Likes Received: 689
  Trophy Points: 280
  Hivi ile budget ya vitafunwa kwa mwaka ni bei gani vile? Mawazir na manaibu na makatibu wakuu, majamishina' wakurugenzi, wakuu Wa mikoa na wilaya. Wanapata posho za kipuuzi bri gani kwa mwaka. Je, kwa nn kamishina mmoja apate posho/marupurupu ambayo ni 3times mshahara Wa kima cha chini.


  AggggrrrrR!
   
Loading...