beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,877
- 6,326
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imetoa tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mafua makali unaosababishwa na kirusi aina ya Corona, uliozikumba nchi za China, Thailand, Japan, Korea Kusini na Marekani.
Wizara imesema kuanzia Desemba mwanzo mwaka jana wamekuwa wakiufuatilia ugonjwa huo tangu ulipotokea katika nchi ya China, Thailand, Japan, Korea ya Kusini na Marekani.
Imeeleza kuwa ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na maji maji yenye virusi kutoka kwa mtu mmoja kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusana majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo.
Takwimu za ugonjwa huo zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 23 Januari 2020 watu wapatao 560 wameathirika huku vifo vikiwa ni 17 ambapo China imethibitisha wagonjwa 550 na vifo 17, Thailand wagonjwa wanne hakuna vifo, Hongkong wagonjwa wawili na Marekani pamoja na Japan zimethibitika kuwa na mgonjwa mmoja mmoja.
Dalili za ugonjwa huo ni homa na mafua makali, kuumwa na kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo, kuathiri mapafu, kupumua kwa shida na hata kifo.
Taarifa ya wizara imeeleza kuwa hadi sasa Tanzania haina mgonjwa , hivyo kutokana na mwingiliano mkubwa wa kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na nchi za bara la Asia ikiwamo China na Tanzania inakuwa katika hatari ya ugonjwa huo.
“Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi wote hususani ambao wanasafiri kwenda kwenye mataifa yaliyoathiriwa na mlipuko huo na wale ambao wanapokea wageni kutoka katika nchi hizo,” ilieleza taarifa hiyo.