Serikali yatakiwa kuwalinda wawekezaji wazawa

Muracha

Member
Aug 26, 2019
35
79
Serikali imetakiwa kuwalinda wawekezaji hususani wazawa wenye viwanda vidogo ili wasaidie kukuza uchumi wa Taifa kupitia viwanda kama yalivyo maono ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi wa ranchi ya mifugo ya Mrito iliyopo Nyamongo Wilaya Tarime mkoani Mara, Mwita Isack aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa Serikali ikiweka mazingira rafiki, wawekezaji wadogo wataweza kufikia malengo yao na kuleta tija kwa Taifa.

Alisema kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo utitiri wa kodi, baadhi ya wawekezaji wadogo wameshindwa kuendeleza shughuli zao akitolea mfano kiwanda chake cha kuzalisha mafuta ya kula yatokanayo na mbegu za alizeti yaitwayo SUNLISHE ambacho kimesimamisha kwa muda uzalishaji.

Isack alisema kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na changamoto ya upatikanaji wa malighafi, mbegu bora za kilimo pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yamesababisha mvua nyingi zilizoathiri kilimo cha zao la alizeti kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo mashamba yaliyopo katika ranchi yake ya Mrito.

Aidha alibainisha kuwa kwa sasa shughuli zinazofanyika kwenye ranchi hiyo yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 1,200 ni pamoja na kilimo, ufugaji na unenepashaji wa ng’ombe pamoja na upandaji miti kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.

Ranchi ya Mrito ni kampuni tanzu inayotokana na kampuni mama ya kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti aina ya Sunlishe iitwayo Issack and Sons.

Na Helena Magabe, Tarime

 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom