Serikali yataka taarifa za uagizaji wa mafuta | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali yataka taarifa za uagizaji wa mafuta

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by PROFESA KYANDO, Aug 22, 2012.

 1. PROFESA KYANDO

  PROFESA KYANDO Member

  #1
  Aug 22, 2012
  Joined: Jul 24, 2012
  Messages: 81
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Jumatano, Agosti 22, 2012 06:02 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

  HATIMAYE Serikali imeamua kuingilia kati na kutaka kupata taarifa kamili kuhusu mpango wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS). Kuingilia kati kwa Serikali katika mpango huo kumetokana na hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyeagiza kupatiwa taarifa za kina kuhusiana na mfumo huo.

  Kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo, baadhi ya wafanyabiashara waagizaji wa mafuta walikuwa wakilalamikia kuhusiana na kuwapo kwa vitendo vya uchakachuaji mafuta yaliyozidishwa ethanol na kuathiri soko la ndani na nje ya nchi.

  Wafanyabiashara hao walisema hatua iliyochukuliwa na Profesa Muhongo itasaidia Serikali kupata undani kuhusiana na mfumo huo, hivyo kuchukua hatua zinazostahili kukomesha vitendo vya uchakachuaji na hasara.

  Wiki iliyopita, Profesa Muhongo aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Kampuni ya Uratibu wa Uagizaji Mafuta (PIC) na kampuni za mafuta kila mmoja kuandika taarifa kuhusiana na mfumo wa BPS.

  Aidha, alitaka kuwasilishiwa taarifa kuhusiana na mfumo huo, hatua itakayoifanya wizara kutambua changamoto zinazokabili uagizaji huo wa mafuta kwa pamoja ulioanza kutumika rasmi Januari, mwaka huu.

  Wiki iliyopita, baadhi ya wabunge walijitokeza na kupendekeza kampuni iliyohusika na kuagiza mafuta yaliyochakachuliwa kiasi cha kuingizia Taifa hasara ya mabilioni ya shilingi ichukuliwe hatua, ikiwamo kufungiwa.

  Mbali ya kufungiwa kwa kampuni hiyo, mamlaka husika nazo zilitakiwa kueleza jinsi ya kufidia hasara ya Sh bilioni 20 kutokana na kuingizwa petroli iliyochanganywa na kiwango kikubwa cha ethanol.

  Wakizungumza mjini Dodoma, baadhi ya wabunge hao walipendekeza Serikali kuifungia Kampuni ya Augusta Energy SA, iliyoingiza mafuta hayo chini ya mfumo wa BPS kati ya Januari na Mei, mwaka huu.

  Akichangia makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini, Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, alisema Taifa lililazimika kulipa Dola 1,000 za Marekani kwa tani ya ethanol iliyochanganywa na petroli tofauti na bei ya Dola 200 za Marekani katika Soko la Dunia.

  Alisema katika kipindi hicho, petroli yenye thamani ya Sh bilioni 210 iliingizwa nchini kupitia BPS kwa mafuta ya soko la ndani na yale yaliyopelekwa nchi jirani.

  Kutokana na kuingizwa nchini kwa mafuta yaliyochakachuliwa, baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta walilalamika na kusababisha mamlaka husika kupeleka sampuli 11 kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

  Matokeo hayo yalionyesha kuwa kati ya sampuli hizo, 10 ziligundulika kuwa na ethanol nyingi kuliko kiwango kinachotakiwa.

  Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kusema kwa sasa linafanyiwa kazi.

  Alisema Serikali itaangalia mfumo huo wa uagizaji mafuta kwa ajili ya kudhibiti mianya yote ya uchakachuaji.

  Tangu kuanza kwa mfumo huo wa BPS Januari, mwaka huu, tani 1,191,780 za mafuta zilingizwa nchini na kati ya kiasi hicho, tani 617,178 zilisafirishwa kwa ajili ya soko la nje.
   
Loading...