Serikali yataja sababu ya kushindwa kutekeleza bajeti iliyopita

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,245
2,000
Kama ulikuwa unajiuliza kwa nini Serikali imetekeleza bajeti yake kwa asilimia 38 pekee, imekusikia na ndio maana imetoa sababu.


Imeeleza changamoto tatu ilizokumbana nazo katika mwaka wa fedha unaoisha Juni .

Akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2017/18 jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alizitaja sababu hizo kuwa ni mwenendo wa upatikanaji wa fedha, upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na matayarisho hafifu ya miradi ambayo baadhi imeonekana ama ipitiwe au majadiliano yaanze upya ili kulinda masilahi ya Taifa.

“Serikali ilipanga kutumia Sh11.82 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini hadi Aprili ni Sh4.52 trilioni tu zilikuwa zimetolewa sawa na asilimia 38 ya bajeti ya maendeleo. Utekelezaji wa mpango wa bajeti mwaka 2016/17 umekabiliwa na changamoto kadhaa,” alisema.

Kati ya Sh11.82 trilioni zilizotengwa mwaka jana, Serikali ilitarajia kukusanya Sh8.7 trilioni kutoka vyanzo vya ndani na kupanga kukopa Sh3.1 trilioni kutoka taasisi za kimataifa na wadau wengine wa maendeleo.

“Mpaka Aprili, Sh907.8 bilioni pekee zilipatikana kutoka nje hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kutotekelezwa kwa miradi iliyokusudiwa.”

Alisema makusanyo ya fedha za ndani yalikuwa yakiongezeka na kupatikana kwa wakati na kuiwezesha kutoa Sh3.6 trilioni.

Akielezea changamoto ya kukopa kutoka nje kama ilivyotarajiwa, Waziri Mpango alisema kulikuwa na kuchelewa kwa upatikanaji wa mikopo yenye masharti ya kibiashara kutokana na mazungumzo na ukamilishaji wa maafikiano kuchukua muda mrefu.

Kwa mwaka 2016/17, alisema: “Ilionekana ipo haja ya kusitisha kukopa baada ya riba kupanda kutoka wastani wa asilimia sita mpaka tisa,” alisema, “Hatua kadhaa zimechukuliwa kukabiliana na hali hiyo. Licha ya kuimarisha makusanyo ya ndani, Serikali imejipanga kuelekeza fedha zinazopatikana kwenye miradi yenye tija na kuboresha mazingira ya biashara nchini.”

Ili kufanikisha hilo, Serikali imesema itarahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu ya biashara, itahuisha sheria, kanuni, taratibu na kupunguza ada, kodi na tozo za uwekezaji na uendeshaji biashara. Pia, itaendeleza majadiliano na taasisi za fedha kupata mikopo hiyo.

Kuhusu upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji, Dk Mpango alisema baadhi imekuwa na utekelezaji hafifu kutokana na migogoro ya ardhi kutokana na kutokamilika kwa ulipaji wa fidia akibainisha kwamba kulikuwa na udanganyifu kwa watu wanaostahili kulipwa fidia.

Katika kukabiliana na hilo, waziri huyo alisema Serikali imeongeza kasi ya upatikanaji wa Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZ na SEZ) na maeneo ya viwanda kwa ngazi zote za mikoa. “Halmashauri zote zimeagizwa kutenga maeneo ya viwanda na biashara ndogo,” alieleza.

Utegemezi wa Bajeti

Ili kukabiliana na changamoto hizo katika bajeti mpya, Serikali imepanga kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje hivyo kuimarisha vyanzo vya ndani.

Kati ya Sh11.99 trilioni zilizopangwa kutumika mwaka ujao wa fedha, Sh8.97 trilioni zitatokana na vyanzo vya ndani na Sh3.03 trilioni kutoka nje ikiwa ni pungufu kwa Sh3.12 trilioni za mwaka jana.

Kufanikisha hilo, Serikali imesema itaimarisha mitaji ya benki za ndani za maendeleo; kilimo na uwekezaji (TIB na TADB) na kuzitumia kama vyombo vya ukusanyaji wa mikopo ya muda mrefu na ya gharama nafuu kwa wawekezaji.

Maeneo ya kipaumbele

Serikali imebainisha shabaha na malengo manane ya kiuchumi kwa ujumla yanayojumuisha kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka 2017 kutoka asilimia 7.0 za mwaka jana.

Imejipanga kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei ili uendelee kubaki kwenye tarakimu moja na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kufikia asilimia 16.5 ya GDP kutoka asilimia 14.6 huku mapato yatokanayo na kodi yakitarajiwa kufikia asilimia 14.2 mwaka 2017/18 kutoka asilimia 12.6 za mwaka huu.

Lengo la tano ni kupunguza uwiano wa matumizi ya umma hadi kufikia asilimia 24.9 ya GDP kutoka asilimia 27.0 za mwaka huu. Uwiano huo uliongezeka kwenye bajeti iliyopo kutoka asilimia 23.2 zilizokuwapo mwaka 2015/16.

Serikali pia imepanga kupunguza nakisi ya bajeti mpaka asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.5 iliyopo huku akiba ya fedha za kigeni ikitarajiwa kutosheleza mahitaji yasiyopungua miezi minne kama ilivyokuwa mwaka huu. Vilevile, Serikali inakusudia kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa thamani ya sarafu ya ndani.

Kwa kuzingatia shabaha na malengo hayo, miradi ya kipaumbele itakayotoa matokeo makubwa yatakayoendana na malengo na Dira ya Taifa ya Maendeleo imeainishwa na mingi inaendelea kutekelezwa.

Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha standard gauge, kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), miradi ya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma na uanzishaji wa EPZ na SEZ. Mingine ni ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asilia mkoani Lindi na uendelezaji wa shamba la miwa Mkulazi.
 

Rweye

JF-Expert Member
Mar 16, 2011
16,383
2,000
Sijaona kununua meli ziwa Victoria. Nchi hii na mkoa wa Kagera ipo siku litatokea ambalo halijawahi kutarijiwa
 

Herbert Nkuluzi

JF-Expert Member
Aug 10, 2015
1,000
2,000
Moja ya maelezo ya kujikanyaga ndo haya.Utawalaumu vipi watu kushindwa kwako kufikia bajeti uliyojipangia wakati ya kwako tu imekushinda kufikia?

unasema eti vyanzo vya nje mligemea trilioni 3 huku vya ndani mkitarajia karibu 10 afu ninyi hao hao mmeishia 4 huo ni upuuzi kabisa mnaotueleza.

Mmeshindwa kabisa kutuongoza , hilo kubalini.
 

MENGELENI KWETU

JF-Expert Member
Oct 23, 2013
8,864
2,000
Sababu huwa hazikosekani kwa serikali hii..

Mlitegemea kupata 3Trillion kutoka nje.. Mlikuwa na uhakika wa kuzipata?? Au ndio mliziweka kwenye bajeti halafu ndio mkazitafute?? Si mnaona mlivyo bounce??
Hopeless kabisa.

Anzeni kuandaa visingizio vipya kwa kufeli kwa bajeti hii.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom