Serikali yaongeza sehemu za kupima corona Uwanja wa Ndege

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,000
9,862
Serikali imeongeza sehemu za kutolea huduma ya upimaji wa virusi vya corona katika viwanja vya ndege kutoka mbili mpaka 10 na kuanzisha huduma ya ulipaji kwa njia ya kielektroniki

Maboresho hayo yamefanyika siku chache baada ya abiria wanaowasili nchini kulalamika kuwa wanakaa muda mrefu viwanjani wakisubiri kupimwa corona.

Mei 15 mwaka huu msanii wa Bongofleva, Richard Martin maarufu Rich Mavoko alisema abiria wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakitokea mataifa mbalimbali wanachukua muda mrefu kupima, kulipia fedha na kupata majibu ya ugonjwa wa Covid-19.

“Nashauri Serikali yetu pendwa iongeze basi walau watu wa kufanya kazi hiyo, kwa kuwa haipendezi mtu umetoka safari umechoka halafu unafika unaanza tena kusubiria foleni ndefu kutoka ndani. Nadhani hii pia inaweza kuwa sababu ya wengine wanaoishiwa uvumilivu kuanzisha vurugu ambazo zingeweza kuepukika.”

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne Mei 18, 2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi ilieleza kuwa huduma hizo sasa zitatumia muda wa dakika 15 pekee na wasafiri wataruhusiwa kuingia ikiwa vipimo vitaonyesha hawana maambukizi.

“Hatua tulizochukua zinalenga kupunguza muda wa mlolongo wa upimaji. Kufuatia maoni haya, maboresho yamefanyika kwa kuongeza sehemu za kutolea huduma ikiwemo vituo vya kupima kutoka viwili hadi 10.

“Ulipaji kwa njia za kielekroniki yaani benki ili kupunguza muda kwa wasafiri kusubiri kufanya malipo. Hivi sasa mteja anatumia wastani wa dakika 15 kukamilisha mtiririko wa malipo na utoaji wa elimu kwa wasafiri juu ya kinga dhidi ya COVID-19. Tunawashukuru wananchi wote ambao wametoa ushauri wa kuboresha huduma hizi,” amesema Profesa Makubi.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na upimaji wa wagonjwa wanaoingia nchini, Profesa Makubi amesema kutokana na mwenendo wa ugonjwa huu duniani na uibukaji wa anuai mpya ya virusi vya Covid-19 katika baadhi ya nchi na kwa kuzingatia namna ambavyo ugonjwa huu unaambukiza Wizara itaendelea kufanya ufuatiliaji.

Amesema wizara ilielekeza wasafiri wote toka nje ya nchi wafanyiwe kipimo cha haraka (Covid-19 Rapid Antigen Test) cha ugonjwa wa Covid-19 pindi waingiapo nchini kupitia mipakani, viwanja vya ndege vya Kimataifa na bandari.

Amesema upimaji huu wa haraka unafanyika pia katika nchi nyingine duniani na mhusika hulipa hivyo si Tanzania pekee ndiyo wanaotoza fedha kwa huduma hiyo.

“Katika nchi mbalimbali, upimaji wa Covid-19 Rapid Antigen Test tayari umeweza kubaini wasafiri kadhaa ambao wana maambukizi ‘Positive’ na walifika na vyeti vilivyoonyesha hawana maambukizi,” amesema.

Amesema gharama ya uchangiaji wa kipimo hiki cha haraka kwa Tanzania ni dola za kimarekani 25 kwa kila abiria.

“Wananchi wote na abiria wanaeleweshwa kuwa kipimo hiki ni muhimu kupimwa tena hata kama umepimwa siku chache zilizopita ili kujiridhisha na hali ya maambukizi, hasa yale yaliyotokea baada ya muda mfupi kabla au wakati wa kusafiri.”

Hata hivyo Profesa Makubi amesema kwa wasafiri wanaolazimika kupima RT-PCR nchini wanapotaka kwenda nje ya nchi, gharama kwa sasa ni dola za kimarekani 100 na fedha hizo ni za uchangiaji wa huduma ya vipimo kwani gharama halisi ni kubwa zaidi na Serikali ya Tanzania imekuwa ikibeba sehemu kubwa ya gharama husika.

Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifello Sichwale amesema atahakikisha anasimamia maofisa afya uwanjani hapo na kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na watashirikiana na wadau wengi katika kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanapata huduma zenye kiwango cha ubora wa juu.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom