Serikali yamwaga misaada kwa Babu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali yamwaga misaada kwa Babu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Lucchese DeCavalcante, Mar 29, 2011.

 1. Lucchese DeCavalcante

  Lucchese DeCavalcante JF-Expert Member

  #1
  Mar 29, 2011
  Joined: Jan 10, 2009
  Messages: 5,473
  Likes Received: 53
  Trophy Points: 145
  Yatamka dawa yake haina madhara kwa binadamu
  *Barabara inayokwenda huko sasa kukarabatiwa
  *Kituo cha afya Samunge kuboreshwe, maji yapelekwa

  [​IMG]
  Mchungaji Mwasapile Kushoto na Kulia ni Waziri Mkuu M.Pinda

  SERIKALI imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ngororo mkoani Arusha kuhakikisha inaimarisha huduma kijijini Samunge kama moja ya
  njia ya kusaidia maelfu ya wananchi wanaomiminika kupata tiba ya 'kikombe' kwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ambilikile Mwasapile.

  Pia imetangaza maeneo makuu matatu ambayo magari yote yanayokwenda Loliondo yatakusanyika kabla ya kuruhusiwa kuanza safari ya kwenda kwa Babu, huku Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiweka bayana kuwa dawa hiyo haina madhara kwa binadamu.

  Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijijini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alipongeza hatua ya mchungaji huyo kusitisha kwa muda utoaji huduma ili kupunguza msongamano ulipo sasa eneo hilo.

  Akijibu swali lililotaka kujua msimamo wa serikali kuhusu kusadia tiba inayotolewa na Mzee Mwasapile maarufu kama 'Babu,' Bw. Pinda alisema kutokana na hali ilivyo, kuna kila sababu eneo hilo kuangaliwa vizuri wakati huu ambapo maelfu ya watu wanamiminika kupata tiba.

  Alisema serikali imekubali ombi la mchungaji huyo kutaka isadie katika kusimamia suala hili. Alieleza kuwa hivi sasa miundombinu ya barabara ni mibovu hali inayosababisha magari mengi kukwama na kufanya magari yaliyoingia eneo hilo kushindwa kutoka.

  "Anataka utaratibu uwekwe ili magari yaende kwa uchache. mimi nimeliafiki hilo hata Rais amekubali," alisema Bw. Pinda na kuongeza;

  "Tunaomba mikoa yote nchini ituelewe. Kwa siku saba hatutaruhusu magari kwenda Samunge. Tumeandaa vituo vitatu ambapo magari yote yanayokwenda Samunge yatakusanyika. Vituo hivyo ni NMC Arusha mjini ambapo magari yanayotoka mikoa kama Dar es Salaam yatafikia. Kituo kingine ni Babati, Manyara na Kanda ya ziwa ni kituo cha Bunda, Mara."

  "Vituo hivi vitakuwa na radio za mawasiliano na zikiruhusiwa zitapita Mto wa Mbu. Malori na mabasi mabovu hayataruhusiwa tunataka yaende mabasi mazuri yanayoweza kusafiri salama. Magari yote hayo yatapewa namba na kupakwa rangi maalum na yatakutana Mto wa Mbu."

  "Polisi wajipange pawe na radio NMC, Babati, Bunda na Mto wa mbu. Ahudumie(Babu) alau wagonjwa 1,000-1,500 ili naye apate muda wa kupumzika tofauti na sasa ambapa anahudumia watu zaidi 2,000 kwa siku,"alisema Bw. Pinda

  Alisema katika kuhakikisha huduma zinaimarishwa, serikali imeagiza Halmshauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuhakikisha maeneo korofi barabara ya kwenda Samunge, yanakarabatiwa haraka sambamba na ujenzi wa vyoo vya kutosha na kupeleka bomba la maji eneo hilo.

  Alisema mbali na hilo, serikali imeiagiza halmashauri hiyo kuboresha kituo cha afya kijijini hapo kwa kupeleka dawa za kutosha ili kusaidia wagonjwa watakaohitaji dawa za hospitali sambamba na kuongeza maturubai nyumbani kwa Babu Mwasapile na kwenye zahanati hiyo ili kuwawezesha wagonjwa kupata eneo la kupumzikia.

  "Tumegundua pia kuwa hapo kwake kuna tatizo la mazingira lakini kwa kuwa anatumia kuni kavu ambazo ukweli hazina athari ya mazingira, tumeagiza mamlaka ya halmashauri hapo wamsaidie. Sufuria na vikombe tutaongezea tukiona inafaa," alisema.

  Bw. Pinda alisema serikali imechukua jukumu la kusaidia tatizo hilo kwa mtazamo wa kiutu na kwamba wanaokwenda ni wananchi wake kwa imani waliyonayo kuhusu tiba hiyo.

  Matokeo ya utafiti wa dawa

  Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema kuwa dawa inayotolewa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Ambilikile Mwaisapile haina madhara yotote kwa binadamu.

  Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bi. Charys Ugullum alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti walioufanya kuhusu dawa ya Babu wa Loliondo mjini Arusha kwa kushirikiana na taasisi nyingine zilizoko chini ya wizara hiyo.

  Taasisi hizo mbali na TFDA, ni Taasisi ya Utafiti wa Dawa asili ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

  "Awali jambo hilo lilizua hofu kwa serikali, wataala mbalimbali na Watanzania kwa ujumla," alisema.

  Bi. Ugullu alisema dawa inayotolewa Loliondo na Mchungaji Mwaisapile wameichunguza na kupata matokeo kutokana na kipimo anachotumia kutibu wagonjwa wameridhika nacho na haina madhara yoyote kwa sasa.

  Alisema wao kama watafiti walichukua sampuli ya dawa ambayo haijatengenezwa na iliyotengenezwa ili kuifanyia uchuguzi katika maabala zao.

  "Tuliichukua dawa hiyo na kuja nayo Dar es Salaam na kuifanyia uchunguzi na tumegundua kwamba ni salama.

  "Sisi sote tuliofanya utafiti tumeridhishwa na dawa anayotoa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapile," alisema Bi.Ugullum.

  Hata hivyo alisema hatua ya uchunguzi itaendelea zaidi ili kubaini kama kweli dawa hiyo inatibu magonjwa matano kama alivyosema mchungaji huyo.

  Aliongeza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi huo ili kujua kama dawa hiyo inafikia viwango na vigezo ambavyo vinakubalika kitaifa na kimataifa kwa matumizi ya binadamu.

  Alisisitiza kuwa katika uchunguzi huo ambao utachukua muda mrefu ili kupata matokeo, watafuatilia maendeleo ya wagonjwa 200 ambao wameshapata kikombe cha babu na kukubali kupima afya zao kujua maendeleo yao.

  "Tutafanya utafiti kupitia kwa wale ambao wameshakunywa dawa ili tujue kama wamepona magonjwa yao waliyokuwa nayo," alisema.

  Bi. Ugullum alisema sanjari na hilo wataendelea kufanya utafti na uchambuzi wa kisayansi katika maabala zao kwa kutumia sampuli waliyopewa na mchungaji huyo.

  Aliongeza kuwa wao kama wadu wa afya wameandaa utaratibu madhubuti wa kufuatilia matumizi ya mti huo ambao unatambulika kama 'Carissaspinarum' katika sehemu nyingine za nchi yetu ili kujua kama ni mmea wa tiba.

  "Tuna taarifa kwamba kwa kipindi kirefu makabila mbalimbali yamekuwa yakitumia mti huo kama tiba. Tutafanya utafiti kwa Wagogo, Wamasai, Wabarbaig na Wasonjo wa kule Samunge ili kupata ukweli zaidi juu ya dawa hii," alisema.

  Alitoa mwito kwa Watanzania kuwa wavumilivu kwa sababu tafiti za aina hii hazina njia ya mkato na kuahidi kutoa taarifa za kina kuhusu dawa hiyo mara tu watakapokamilisha utafiti wao.

  Alimshukuru Mchungaji Mwasapile kwa ushirikiano aliouonesha kwa timu ya watafiti walioenda kumuona kutoka siku walipofika Loliondo.

  Naye Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Mbadala Daktari Paulo Mhane alisema wako katika hatua za mwisho kushughulikia usajili wa huduma ya mchungaji huyo ili kupata cheti cha ukubalifu.

  Msimamo kuhusu Gaddaff

  Mbali na dawa ya Samunge, Bw. Pinda alisema Tanzania ina uhusiano mzuri na Libya hadi machafuko yalipoibuka nchini humo hivi karibuni. Alisema hadi sasa haijatoa msimamo wowote kuhusu kinachoendelea nchini humo na kwamba inasubiri msimamo utakazotangazwa na wakuu wa Umoja wa Afrika (AU)

  "Njia rahisi ni kupitia AU. Tusubiri msimamo utakaotolewa na AU. Lakini kinachosikitisha ni kwamba binadamu wanaendelea kufa si jambo zuri sana, wakubwa watangulize utu kwanza," alishauri.

  Mikoa mipya

  Alisema mchakato kwa ajili ya kuanzishwa mikoa mipya na wilaya zake umekamilika na inatarajiwa kuanza kipindi cha mwaka ujao wa fedha. Alieleza kuwa kilichobaki ni tangazo kwa mujibu wa sheria na maoni ya Watanzania na kuweka tangazo hilo kwenye gazeti la serikali

  Matumizi ya mashangingi

  Bw. Pinda alisema serikali inazidi kushughulikia suala la kupunguza magari ya kifahari serikali maarufu kama mshangingi na tayari ofisi yake imekwisha andaa viwango mbalimbali vya magari yanayopaswa kutumiwa na maofisa wa ngazi mbalimbali wa serikali.

  Malumbano ndani ya CCM


  Kuhusu malumbano yanayoendelea ndani ya chama tawala CCM kati ya makada wake wakongwe na Umoja wa Vijana wa chama hicho, Bw. Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, alisema anasikitishwa na hali hiyo.

  Aliwataka wanachama wa CCM kutumia vikao na kutokuwa woga kutoa madukuduku yao ndani ya chama kwani hiyo ndio njia pekee ya kukijenga chama hicho.

  "Nawasihi tutumie mfumo wa vikao vya chama na tusiwe woga huko ndiko sehemu ya kujenga. Mahali pazuri ni kutumia vikao vya chama...Mifumo mingine haitoi picha nzuri.

  Mgawo wa umeme


  Alisema mvua zilizoanza kunyesha nyanda za juu Kusini zimeleta ahueni ya mgawo wa umeme kutokana na vyanzo vya Kidatu na Kihansi kupata maji ingawa Mtera bado kuna tatizo.

  Hata hivyo alisema serikali inaendelea kuchukua juhudi mbalimbali kuhakikisha megawati 160 zinapatikana mwaka huu kupitia chanzo cha Ngaka na Mchuchuma na kubainisha kuwa miaka miwili hadi mitatu ijayo, tatizo la umeme litapungua.

  Malipo walimu wapya

  Aliziagiza halmashauri za wilaya kote nchini kuhakikisha zinatoa barua zinazoonesha stahili za walimu wapya waliopelekwa wilaya mbalimbali nchini na kuwalipa haki hizo

  Ametoa agizo hilo kutoka na kile alichoeleza malalamiko anayopokea ofisini kwake kuhusu walimu hao 'kupigwa danadana' juu ya haki zao mbali ya kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.

  "Tumepeleka posho zao, halmashauri zisiwababaishe, wawaambie stahili zao kwa mujibu wa taratibu za utumishi serikalini. Wawaambie waziwazi au wawaandikie haki zao," aliagiza

  Kuhusu maofisa kilimo na mifugo 2000 waliotarajiwa kuingia kwenye ajira Mei mwaka huu sasa wataunganishwa na wenzao wapatao 3000 na kuingizwa kwenye ajira katika mwaka ujao wa fedha unaonzia Julai mwaka huu.

  Souce: Gazeti la Majira
   
Loading...