Serikali yamega ngome kuu ya Mbunge Zitto Kabwe Kigoma

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,184
671
Serikali yamega ngome kuu ya Mbunge Zitto Kabwe Kigoma
Na Richard Mwakyambo, Kigoma

NGOME kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Uchaguzi la Kigoma Kaskazini, mkoani Kigoma ambalo Mbunge wake ni Zitto Kabwe (Chadema), huenda ikavunjwa baada ya serikali kukusudia kulimega jimbo hilo na kuihamishia ngome hiyo katika wilaya mpya.


Mpango huo, umeelezwa na serikali kuwa ni katika mchakato wa kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wengi kwa wakati.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, John Mongella, Jimbo la Kigoma Kaskazini litakabiliwa na hali hiyo kutokana na mpango wa kuigawa Wilaya ya Kigoma na kuanzisha wilaya mpya ya Uvinza.


Akiwasilisha taarifa ya serikali katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kigoma (RCC) hivi karibuni, Mongella, alisema jimbo hilo lenye kata 10, sasa litamegwa na kubaki kata saba tu na kwamba, Kata Mwandiga iliyokuwa ngome kuu ya Chadema, itahamia katika Jimbo la Kigoma Mjini, hivyo kuongeza ushindani katika Uchaguzi Mkuu ujao utaoafanyika nchini mwaka 2010.


Mwandiga, imekuwa ngome kuu ya upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, na chama hicho kimekuwa kikishinda chaguzi zote, kuanzia serikali kuu na serikali za mitaa tangu mwaka 1994 na kuibwaga CCM.


Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema kuwa, kumegwa kwa jimbo lake na kuhamishwa kwa kata hiyo, ni pigo kwa chama chake.


Mapendekezo hayo yanayolenga kuigawa wilaya hiyo iliyokuwa na halmashauri mbili za wilaya ambazo ni a Kigoma Ujiji na Wilaya ya Kigoma, yalizua mjadala mkali miongoni mwa wajumbe wa RCC.


Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma iliyokuwa na kata 22, itagawanywa na kuanzisha Wilaya ya Uvinza ambayo itabaki na kata 12.


Jimbo la Kigoma Kusini, litagawanywa na kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni la Buhingu ambalo litakuwa mwambao wa Ziwa Tanganyika na Malagarasi maeneo ya nchi kavu kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi.


Kutakuwa na majimbo mawili ya Kalinzi na Kigoma Mjini na kila wilaya, itakuwa na halmashauri moja ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na ya Wilaya ya Kigoma.


Halmashauri hizo, zimezua mjadala mkali na kuwagawa wajumbe, baadhi wakitaka halmashauri tatu na wengine wakitaka zibaki mbili kama ilivyokuwa awali.


Baadhi ya viongozi waliopigania kubaki halmashauri mbili ni pamoja na Mongella, Zitto na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba.


Wakati viongozi hao wakitaka hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Kassim Nyamkunga alipingana nao na kupendekeza iongezwe halmashauri nyingine moja ili ziwepo tatu.


Mapendekezo hayo yanaonyesha kwamba makao makuu ya wilaya mpya ya Uvinza, yatakuwa Rugufu ambako kuna kambi ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wanaotakiwa kuondoka kurudi kwao ifikapo Desemba 31, mwaka huu.


Mapendekezo hayo yanatokana na kuwapo kwa miundombinu ya kutosha, kama ofisi, nyumba za kuishi, huduma za mawasiliano ya simu, barabara na maji ya bomba, ambavyo vitasaidia katika hatua za awali za uanzishaji wa wilaya mpya.


Wakitoa maoni yao, baadhi ya wakazi wa wilaya ya Kigoma, walisema bado kuna mapungufu katika mapendekezo hayo kutokana na hisia kudai kwamba baadhi ya wanaoishi mwambao wa Ziwa Tanganyika, wataendelea kupata shida kutokana na umbali uliopo kutoka wanakoishi hadi makao makuu ya wilaya.


Simon Kisozi, mkazi wa Mwanga, mjini Kigoma alisema wakazi wa Kata za Kalya, Buhingu na Igalula, wataendelea kupata shida kutokana na kutumia usafiri wa meli na wakifika mjini Kigoma, watalazimika kupanda magari kuelekea Rugufu yaliko makao makuu ya wilaya hiyo mpya .

http://www.mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=3175
 
Mbinu za kienda wazimu zina mwisho.Maendeleo hayaletwi kwa kugawa mikoa na wilaya bali kwa kupeleka huduma.Hata wakigawa majimbo yakawa saizi ya mtaa,kama hawajui sababu zinazopelekea sehemu hizo kuwa masikini kamwe hawatofaninkiwa.
 
Kutakuwa na majimbo mawili ya Kalinzi na Kigoma Mjini na kila wilaya, itakuwa na halmashauri moja ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na ya Wilaya ya Kigoma.



Hii yote ni biashara ya peter serukamba. Tunajua ujiji hakubaliki ndio maana anataka apewe jimbo lake. Hii biashara ya ubinafsi na umimi ndio imetufikisha hapa tulipo. Leo hii, badala ya kujadili daraja la maragarasi, wenyewe wanakalia politiki ya kugawana majimbo, ilimradi kila mtu apate kasungura. Hii habari ilikwisha julikana siku nyingi. Haya, kazi kwenu.
 

Kutakuwa na majimbo mawili ya Kalinzi na Kigoma Mjini na kila wilaya, itakuwa na halmashauri moja ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na ya Wilaya ya Kigoma.


.....ili wapate kuongeza majimbo bungeni kwa kura za wizi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom