Serikali yalaani vikali vitendo vya Ukeketaji wa watoto wa kike Kata ya Kivule Ilala, Dar

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
2,038
2,000
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

(TAARIFA KWA UMMA)

WIZARA YALAANI VIKALI UKEKETAJI WA WATOTO WA KIKE KATA YA KIVULE, MANISPAA YA ILALA, JIJINI DAR ES SALAAM

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakemea vikali vitendo vya ukeketaji vinavyotaarifiwa kufanyika katika Kata ya Kivule, Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, na mikoa mengine ambayo imekaririwa na vyombo vya habari.

Wizara inaagiza wazazi na walezi kuacha mara moja vitendo vya ukeketaji kwani ni ukatili, husababisha madhara kwa watoto wa kike na wasichana ni kosa la jinai.

Athari za ukeketaji kwa wahanga ni pamoja na kusababisha majeraha kwa watoto, vifo, vilema, maradhi kama fistula na mengineyo.

Watoto wa kike na wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa vitendo vya ukeketaji bila ridhaa yao na wakati mwingine ridhaa hiyo huwa imepatikana kwa hila, jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wizara inatoa rai kwa vyombo vya dola kuwakamata wazazi, walezi, mangariba, na wote wanaoendeleza vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wasichana katika kata ya Kivule na maeneo mengine nchini, na kuwafikisha mahakamani ili sheria iwezekuchukua mkondo wake.

Wizara itaendelea kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyotaarifiwa katika jamii zetu, na itaongeza juhudi ya utoaji elimu kwa jamii sambamba na kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na mila potofu ya ukeketaji.

Wito unatolewa kwa kila mwananchi kushiriki katika kuzuia vitendo vya ukeketaji na hasa kufichua matukio ya ukeketaji, na kutoa ushahidi mahakamani ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Wizara inatoa rai kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii katika Mikoa, Halmashauri na Kata katika maeneo ambako kunaarifiwa kuwepo vitendo vya ukeketaji kuhakikisha kuwa wanashirikiana na mamlaka husika kuzuia ukatili huo katika nchi yetu.

Erasto T. Ching’oro

Msemaji wa Wizara-Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

21/12/2016
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom