Serikali yakemea Ubabe na Vitisho vya TRA kwa Wafanyabiashara, yaitaka kujitathmini

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,023
1,609
Mawaziri wawili wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwashughulikia watumishi wanaotoa vitisho, ubabe na wanatengeneza mazingira ya kupata rushwa kutoka kwa wafanyabiashara.

Mawaziri hao pia wameitaka TRA itathimini utendaji wake kutokana na malalamiko ya kuwakadiria kodi kubwa wafanyabiashara, kutoza kodi kabla ya biashara kuanza na urasimu kwenye ulipaji wa kodi.

Mawaziri hao ni Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, ambapo walitoa kauli hiyo juzi jioni kwenye hafla ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya mlipakodi mwaka 2022 iliyoambatana na utoaji wa tuzo kwa walipakodi bora.

Kauli za viongozi hao zimekuja siku chache tangu Mwenyekiti wa bodi ya TRA, Uledi Mussa atangaze mamlaka hiyo kukiondoa kikosi kazi cha kukusanya kodi wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Waziri Nape ambaye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, aliitaka mamlaka hiyo ijirekebishe kwa kuondoa urasimu wakati mfanyabiashara anapotaka kuanza biashara na wawe na ubunifu mzuri kwa wanaoanza biashara ili zikue na wawe walipakodi wazuri.

“Tushughulikie urasimu, hasa wakati wafanyabiashara wanaanza biashara zao, waruhusiwe kuanza kabla ya kulipa kodi na inapofika wakati wa kulipa kodi makadirio ya kodi zao yawe sawa na biashara yake, wasiongezewe kodi,” alisema.

Hata hivyo, Nape alisema hali ya kukusanya kodi kwa mabavu (kikosikazi) kwa sasa imepungua sana na alishauri ukusanyaji wa kodi wa kujali taaluma uendelee kutumika kwa ajili ya kuongeza mapato.

Pia, Nape alisema suala la kufutwa kwa kikosi kazi limemgusa kwa sababu lilikuwa linaua biashara nyingi kwa wafanyabiashara kutengeneza uadui na TRA na kupelekea kufungwa kwa biashara nyingi.

“Wakati nikiwa mbunge, nakumbuka tulilipigania sana suala la kufutwa kwa kikosikazi na tuliwaambia madhara yake kwenye kuua biashara na wengi waliniambia najisumbua tu na sitafanikiwa, ila leo nina furaha hakipo tena na biashara zimerudi kwenye hali shwari,” alisema.

Februari 9 mwaka jana, katika moja ya michango yake bungeni, Nape akiwa mbunge alizungumzia suala la ukusanyaji kodi, akisema, “ukusanyaji wa kodi ni taaluma ya muda mrefu sana, lakini changamoto tulionayo ni kwamba tumeamua kuacha kuwatumia wataalamu ambao ndio wakusanya kodi.

“Sasa kinachotokea wanakwenda kwa mfanyabiashara hawajali maisha yake ya kesho, hawajali kwamba wanatakiwa kukusanya kodi leo, hawamuachii uwezo wa kuzalisha ili wakusanye na kesho, sasa tunafurahia matokeo ya muda mfupi kwa sababu idadi ya biashara zinazofungwa ni nyingi mno, kesho hatuna ng’ombe wa kumkamua maziwa,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Chande aliunga mkono kauli ya Nape na kuwataka TRA kufanyia kazi changamoto zote wanazolalamikiwa na wafanyabiashara ili kuongeza tija ya makusanyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande

“Urasimu kwenye upatikanaji wa namba ya mlipakodi (TIN), mfanyabiashara kutakiwa kulipa kodi kabla ya biashara kuanza, makadirio ya kodi yasiyoendana na mapato, kufungiwa biashara bila kufanya ufuatiliaji, vitisho kwa wafanyabiashara, kuyumba kwa mtandao mara kwa mara, changamoto hizi zifanyiwe kazi,” alisema.

“Usimtishe mfanyabiashara, nenda kwa lugha nzuri na hekima, mfanyabiashara atachangia vizuri,” aliongeza.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba akizijibu hoja zilizoibuliwa na Nape na Chande wakati wa hotuba zao alisema wizara itayasimamia maelekezo na changamoto zilizotajwa kwa ajili ya kuongeza tija ya mapato.

“Maelekezo uliyoyatoa sisi tutaendelea kuyasimamia na tutahakikisha TRA wanayatekeleza na tutatoa mrejesho kwa wafanyabiashara ili mwakani tukikaa tuone kuwa maelekezo hayo yametekelezwa ili yalete tija kwenye kuongeza makusanyo,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka hiyo, Mussa Uledi alisema lengo la kuandaliwa kwa tuzo hizo ni pamoja na kuthamini mchango wa walipa kodi ambao wanachangia maendeleo ya nchi.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata alisema kukusanya kodi kwa njia za kitaaluma kumeongeza mapato mengi ikilinganishwa na njia za mabavu walizokuwa wanazitumia awali.

Martin Balige, Mfanyabiashara na mmiliki wa Chanika Poultry Farm ambaye aliibuka mshindi wa tatu kwa ulipaji kodi wilaya ya kikodi Chanika alisema kikosi kazi kilikuwa kinafanya kazi kinyume na utaratibu, jambo lililosababisha biashara nyingi kudorora.

“Sasa hivi (baada ya kufutwa kikosi kazi) mazingira ya biashara yapo vizuri kwasababu tunaenda na utaratibu ikilinganishwa na wakati wa nyuma ambapo mimi kikosi kazi kilinivamia na kuifungia akaunti yangu binafsi bila taarifa, jambo ambalo liliniwia vigumu kwenye kuendesha maisha yangu binafsi na biashara yangu,” alisema.

Akizungumzia faida ya ukusanyaji wa kitaaluma, Balige alisema mapato yatazidi kuongezeka kwa TRA kwasababu mazingira wezeshi ya kufanya biashara yapo.

Chanzo: Mwananchi
 
TRA inajifanyia kazi kivyake bila kufuata maelekezo ya serikali kuu?

au serikali inajiliza na kujinyamazisha yenyewe?
 
Ila TRA ni miungu watu kwa wafanya biashara.... Makadirio mtu unayo pewa na biashara haviendani...ukilalamika hakuna msaada......basi njooni mkague biashara tupo busy!!...
 
Huyu nape najua yuko humu namwambia kabisa yeye ni bogus kabisa, tcra na mitandao ya simu imemshinda kuhusu gharama ya bundles eti leo anaenda kukemea jambo ambalo sio la wizara yake.
 
Ukimkadiria mtu kulingana na mauzo kwa siku humtendei haki, angalia katika hayo mauzo amepata faida kiasi gani ndipo ukate kodi kulingana na hiyo faida. Ukiangalia mauzo unafyeka mtaji wake.
 
Ukimkadiria mtu kulingana na mauzo kwa siku humtendei haki, angalia katika hayo mauzo amepata faida kiasi gani ndipo ukate kodi kulingana na hiyo faida. Ukiangalia mauzo unafyeka mtaji wake.
Msingi wao kutumia mauzo kukadiria ni wa ajabu sana. Kodi inatakiwa kukatwa baada ya mtu kupata kipato(earning). Sasa mtaji ni kipato? Watafute formula nyingine kwa kweli.
 
Lakini Nape ajue pia kwamba hakuna mtu anayependa kutoa hela kulipa kodi. Kodi ni ya kushurutishwa. Ukitaka watu walipe kodi kwa hiari, unadhoofisha dola. Utakosa uwezo wa kifedha wa kuendsha serikali, dola na kulipa ruzuku ya CCM na vyama vingine.
 
Back
Top Bottom