Serikali yaingiza mabilioni ya shilingi Kesi za Uhujumu Uchumi 2020

GeoMex

JF-Expert Member
Jan 10, 2014
3,793
2,000
Dar es Salaam. Serikali imeingiza zaidi ya Sh123.6 bilioni kutoka kwa washtakiwa mbalimbali wa kesi za makosa ya uhujumu uchumi katika mwaka huu wa 2020.

Kiasi hicho cha fedha ni katika kesi 15 zilizoripotiwa na gazeti hili ndani ya mwaka huu, baada ya washtakiwa kukiri makosa yao na kuanza kurejesha fedha walizokuwa wanadaiwa, kulingana na makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Utaratibu huu ulianza mwaka 2019, baada ya Rais John Magufuli kutangaza msamaha kwa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi kwa sharti la kurejesha fedha walizokuwa wanadaiwa.

Magufuli alitoa msamaha huo Septemba 22, 2019 aliopomshauri DPP kuangalia uwezekano wa kuwasikiliza washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi ambao wako tayari kuomba radhi ya kurejesha fedha wanazotuhumiwa kupoteza.

Kutokana na maelekezo hayo, Oktoba Mosi 2020, DPP Biswalo Mganga alitoa taarifa kwa Rais kuwa hadi kufikia siku hiyo washakiwa 467 walikuwa wameshaandika barua za kuomba msamaha na kuwa walikuwa tayari kurejesha fedha zinazofikia Sh107 bilioni.

Wakati huo, Bunge lilikuwa limepitisha marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa kuingiza kifungu kinachoruhusu washtakiwa kuingia majadiliano na DPP ili kumaliza kesi zao.

Majadiliano hayo ambayo mwisho husajiliwa mahakamani, yanamwezesha mshtakiwa kukiri kosa na kutoa taarifa zinazoweza kuwezesha kuzuia makosa mengine ili kuharakisha kesi; na kuamua kumshtaki mshtakiwa kwa kosa lenye adhabu ndogo na kumtaka m kulipa fidia, kurejesha au kufilisiwa mali zote zitokanazo na uhalifu.

Waliokubaliana na DPP
Miongoni mwa washtakiwa waliofikia makubaliano na DPP na kumaliza kesi zao kwa njia hiyo kwa mwaka 2020 ni pamoja na mwanahabari Erick Kabendera ambaye alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Agosti 5, 2019 kwa mashtaka ya kupanga na kushirikiana na mtandao wa kiuhalifu, ukwepaji kodi zaidi ya Sh173 milioni na utakatishaji fedha haramu Sh173 milioni.

Februari 24, 2020 alitiwa hatiani na kutakiwa kulipa faini ya Sh100.25 milioni na fidia Sh173 milioni.

Kesi nyingine iliwahusisha washtakiwa Harry Kitilya, Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana ambao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58, lakini Agosti 25, 2020 walifikia makubaliano na DPP ambapo pamoja na mambo mengine aliwafutia mashtaka 57 na kuwabakishia shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 6 milioni.

Walihukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi sita jela na kila mmoja kulipa fidia ya Sh1.5 bilioni waliyoisababisha Serikali.

Mbali na kesi hiyo, ipo ya mwaka 2018 iliyowahusu Rais wa Migodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu, Deodatus Mwanyika na wenzake wawili waliokuwa wanakabiliwa na shtaka moja la kukwepa kodi ya TRA dola za Marekani 9.3 milioni, baada ya kufutiwa mengine 38.

Baada ya kutiwa hatiani, walihukumiwa kulipa fidia ya Sh1.5 bilioni, pia kulipa faini ya Sh1.5 milioni kila mmoja au kifungo cha miezi minne jela, kila mmoja.

Mr Kuku
Tariq Machibya (29) maarufu Mr Kuku alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Agosti 10, 2020 akikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kufanya biashara haramu ya upatu na kukusanya fedha za wananchi zaidi ya Sh17 bilioni.

Baada ya makubaliano na DPP alifutiwa mashtaka matano na kubakiwa na mawili ya kushiriki biashara ya upatu na kukubali kupokea miamala ya fedha.

Desemba 16, 2020 mahakama ya Kisutu ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitano na kulipa fidia ya Sh5.4 bilioni.

Vigogo wa Halotel
Hawa ni wakurugenzi na watendaji wa kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Halotel waliopandishwa kizimbani Machi 27, 2020 wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo kuongoza genge la uhalifu, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh75 bilioni.

Baada ya makubaliano na DPP waliondolewa mashtaka sita wakabakiwa na manne. Desemba 22, 2020 mahakama ya Kisutu iliwatia hatiani na kuwahukumu kulipa faini ya jumla ya Sh24 milioni, fidia ya Sh42 bilioni, kati ya hizo, Sh30 bilioni kulipwa na kampuni.

Wathamini madini
Wa karibuni kabisa ni watumishi wawili kutoka iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, aliyekuwa Mkurugenzi wa Uthaminishaji almasi na vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo na Mthamini wa madini ya almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Septemba 15, 2017, wakikabiliwa na shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 29.5 milioni sawa na Sh61.9 bilioni.

Desemba 18,2020 walikiri mashtaka na mahakama ikawatia hatiani kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja Serikali kutaifisha madini waliyokutwa nayo yenye thamani ya Sh61.9 bilioni.

Wauza madini
Desemba 23, 2020, wafanyabiashara Haji Hassan na Jamal Mohamed walihukumiwa kulipa fidia ya Sh40 milioni baada ya kukiri mashtaka ya kufanya biashara ya madini bila kuwa na leseni.

Pia mahakama ilitaifisha madini waliyokamatwa yakiwemo ya fedha na dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh543 milioni.

Vigogo Best Ocean Air Limited
Machi 26, 2020, mahakama iliwahukumu raia wawili wa India, Manish Khattar (38) na Rajesh Velram(38) kulipa faini ya Sh230 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na makontena 18 ya magogo aina ya mpingo yenye thamani ya Sh500 milioni bila kibali.

Mahakama ilitaifisha magogo hayo kuwa mali ya Serikali na kuwahukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja, kwa kutokujihusisha na kosa lolote la jinai katika kipindi cha muda huo.

Salsabili Investiment
Mkurugenzi wa Kampuni ya Salsabil Investment Ltd, Abdulrahman Omary (55) alikuwa akikabiliwa na kosa la kusafirisha ya makontena 17 yenye shehena ya magogo aina ya mpingo yenye thamani ya Sh452 milioni bila kibali cha TFS.

Aprili 22, 2020 alikumiwa kulipa fidia ya Sh207 milioni na kutaifisha magogo 5,754 na kuwa mali ya Serikali.

Mhandisi wa Mawasiliano
Novemba 24, 2020 mahakama hiyo ilimhukumu, Mhandisi wa Mawasiliano, Baraka Mtunga na mfanyabiashara Rajabu Katunda kulipa fidia ya Sh267 milioni, kwa kosa la kusambaza huduma ya mawasiliano ya intaneti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani bila kulipa kodi na bila kuwa na kibali kutoka TCRA.

Pia, walitakiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni kila mmoja au kutumika kifungo cha miaka miwili jela na kutaifisha vifaa vilivyohusika katika kesi hiyo.

Mfanyakazi CRDB na wenzake
Machi 30, 2020 mahakama hiyo imemuhukumu, Ofisa wa Benki ya CRDB, Andrew Babu na wenzake watatu, kulipa fidia ya Sh106 milioni, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi wa Sh106 milioni kwa kutumia kadi ya Viza Gold mali ya Profesa Charles Kihamia, baada ya kukiri mashtaka na makubaliano na DPP.

Chanzo: Mwananchi
 

Hamatan

JF-Expert Member
Nov 10, 2020
867
1,000
Serikali kwa kiasi kikubwa imeingiza fedha kwa njia ya dhulma.

Iliwaweka mahabusu kwa muda mrefu. Ikashindwa kupata ushahidi wa kuwatia hatiani. Ikawalazimisha wakiri makosa, la sivyo waendelee kusota mahabusu.

Watuhumiwa wakaamua kununua uhuru wao ili wajumuike na familia zao.

Jambo hili wala siyo la kujivunia. Ni sawa ujenge jumba la kifahari la ghorofa kwa pesa uliyoipata kwa njia ya ujambazi.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

tindo

JF-Expert Member
Sep 28, 2011
38,246
2,000
Haya makosa kwakweli kuna watu wengine walizidi aisee. Walitunyanyasa sana na hela chafu hadi wengine tukawa tunaonekana hatujui kupambana. Wacha wazikusanye tu

Kwahiyo serekali nayo imeamua kuwanyanyasa ili iwapore hizo hela?
 

nkese

JF-Expert Member
Mar 8, 2017
2,886
2,000
Dar es Salaam. Serikali imeingiza zaidi ya Sh123.6 bilioni kutoka kwa washtakiwa mbalimbali wa kesi za makosa ya uhujumu uchumi katika mwaka huu wa 2020...
Huo ni ubunifu wenye manufaa/wenye kujenga au kubomoa? (constrctive or destructive)?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom