SERIKALI imeanza mchakato wa kutafuta mwekezaji mpya kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo baada ya mazungumzo na mwekezaji wa awali kutokufikiwa mwafaka na hatimaye kujitoa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema hayo jana alipoulizwa swali na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ambayo serikali imefikia katika mpango wake wa kuanza ujenzi wa bandari hiyo.
“Bandari ya Bangamoyo ni kweli muda mrefu tumeizungumza na tulikuwa tunaenda vizuri na baadhi ya watu lakini sasa hivi inaonekana yale mazungumzo hayakwenda vizuri. Mwenyewe ameamua hatoendelea kuwekeza huko,” alisema Prof. Mbarawa.
Pia alisema hata baada ya mazungumzo na mwekezaji wa awali kuvunjika, nia ya serikali ya kujenga bandari hiyo iko pale pale.
“Nia ya serikali iko pale pale kwa sababu tunajua bandari hii ya Dar es Salaam inaanza kufika mahali inashindwa uwezo wake na bandari itakayotuokoa ni hii ya Bagamoyo. Kwa hiyo hilo la serikali tunalijua na tutahakikisha tunalisimamia ili tuijenge haraka iwezekanavyo.
“Katika mpango huu, naamini tutapata wawekezaji wengine wazuri na wenye uwezo wa kujenga bandari hii ya Bagamoyo,” alisema Mbarawa.
Wakati wa Bunge la Bajeti lililomalizika Juni 30, mwaka huu, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2022/23, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22, serikali ilifufua majadiliano ya mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Bagamoyo (BSEZ) uliosimama tangu mwaka 2018.
Alisem wizara yake ndiyo ilikuwa inaratibu uendelezaji wa BSEZ unaolenga kuendana na ushindani wa biashara za usafiri wa majini pamoja na kuunganisha shughuli zingine za kiuchumi ikiwamo viwanda na utalii.
Dk. Kijaji alisema wizara hiyo ilifufua majadiliano na wawekezaji ambao ni Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) ya China na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) ambayo awali ilikuwa inaitwa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF).
Kwa mujibu wa Kijaji, majadiliano hayo yalihusu eneo dogo la mradi wa BSEZ kwa kuendeleza eneo la hekta 3,087 kati ya hekta 9,887 ambapo unahusisha ujenzi wa bandari.
Pia alisema mpango huo ulihusisha ujenzi wa kituo cha usafirishaji kwenye eneo la hekta 887 na uendelezaji wa eneo maalum la viwanda kwenye eneo la hekta 2,200.
Chanzo: IPP MEDIA