Serikali yaagiza wanaodaiwa na TTCL kukatiwa huduma baada ya Januari 31 endapo hawatalipa madeni

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,495
9,275
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile ameliagiza shirika la mawasiliano Tanzania TTCL kufuatilia madeni ya malimbikizo yote inayoyadai mashirika mengine ya Umma na yakishindwa kulipa hadi januari 31 yakatiwe huduma.

Huduma hizo ni simu na intaneti ambapo hadi sasa mashirika hayo yanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 30 na shilika la TTCL.

Dkt Ndugulile ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akifunga kikao kazi cha watendaji wa shirika hilo amesema taasisi hizo 20 zinadaiwa zaidi ya Sh.Bilioni 30 na kutoa ufuatiliaji ufanyike haraka na fedha hizo zilipwe.

“Kuna taasisi zinazodaiwa huduma ya data na simu walipe hayo madeni ifikapo Januari 31, mwaka huu wale ambao hawajalipa wakatiwe huduma, maana kila taasisi kwenye bajeti yake imetenga fedha kwa ajili hiyo lakini hawalipi" amesema Dkt Ndugulile.

Amesema haiwezekani mashirika hayo wakawa wanapata sifa ya kukusanya mapato kwa kutumia huduma hizo lakini hawalipi hawawezi kuwa na mapenzi ya mshumaa kwa wao kuungua tunawamulikia wengine.

Aidha amelitaka shirika hilo kufanya mapitio ya mikataba yake ambayo si rafiki kwa Shirika na kutoa mapendekezo serikalini ifikapo mwishoni Machi, mwaka huu ili hatua zichukuliwe zitakazoongeza mapato.

Ameongeza kuwa “Kuna taarifa kwamba washindani wenu kibiashara ndio wanaohujumu miundombinu tuleteeni tuwashughulikie, nilishasema hili na nasisitiza Mkurugenzi ulishasema hili kwamba miundombinu hasa Dar es salaam inahujumiwa,”amesema.

Ameendelea kusisitiza kuboreshwa kwa kitengo cha huduma kwa wateja kutokana na kulalamikiwa ya wateja pindi wanapotaka huduma katika kitengo hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Waziri Kindamba amesema katika kikao hicho wamekubaliana kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), inayotaka TTCL kuongeza matumizi ya mkongo wa taifa na matumizi ya data kutoka asilimia 40 hadi 80 na maagizo yote aliyoyatoa Rais John Magufuli.

Aidha amesema wamekubaliana kuongeza idadi ya wateja kutoka asilimia mbili hadi sita kwa mwaka, kuongeza mawakala wa vocha na T-pesa ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

“Kuboresha huduma kwa wateja ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa na kuimarisha biashara na mahusiano ya taasisi za umma na binafsi,” amesema.
 
Back
Top Bottom