Serikali ya Zanzibar yatangaza bei ya Sukari kwa Kilo kuwa Tsh. 2,000

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279
SERIKALI ya Zanzibar imetoa bei elekezi ya sukari baada ya kuwapo kwa viashiria vya baadhi ya wafanyabishara kutaka kupandisha bei ya bidhaa hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaban, alibainisha kuwa kilo moja ya sukari itaendelea kuwa Sh. 2,000.

Waziri huyo alisema uamuzi huo umelenga kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kuhimili wimbi la kupanda kwa bei za bidhaa hasa zile muhimu katika kipindi hiki ambacho imebaki miezi miwili kuingia kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema serikali imepokea maombi kutoka kwa wafanyabishara waingizaji wa sukari, wakishauri serikali kufanya mapitio ya tangazo lake la bei elekezi kwa bidhaa ya sukari kutoka Sh. 2,000 kwa kilo hadi Sh. 2,300 kutokana na gharama za uagizishaji wa bidhaa hiyo kupanda katika soko duniani.

Shaban alisema serikali baada ya kutafakari maombi hayo imeona ni vyema bei elekezi ikaendelea kubaki kama awali lakini kwa kuwa hoja iliyotolewa na wafanyabishara ya kutaka kuongeza bei ni ya msingi, serikali imeamua kupunguza ushuru wa uingizaji wa sukari kwa asilimia 50 ili kupunguza gharama ya kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

"Serikali imeamua kujinyima mapato yanayotokana na ushuru wa kuagiza bidhaa hiyo ili wananchi waendelee kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu na haitakubali kuona wananchi hawanufaiki na punguzo hilo la ushuru na badala yake wafanyabishara wanafaidika zaidi," alionya.

Alisema wizara itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya sukari duniani kwa lengo la kusimamia ipasavyo bei elekezi ambazo imekuwa ikitoa mara kwa mara.

Waziri huyo alitoa miezi mitatu kwa wafanyabishara ambao wamepewa kibali cha kuingiza sukari na hawajaingiza sukari karibu mwaka mzima, kuwanyang'anya vibali hivyo endapo watashindwa kuingiza sukari.

IPPMedia
 
Back
Top Bottom