SoC 2022 Serikali ya Tanzania iwekeze usafiri kwenye elimu ya msingi na sekondari

Stories of Change - 2022 Competition

DON YRN

Member
Jan 14, 2019
62
112
UTANGULIZI.

Kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa elimu katika jamii hasa kwenye maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja. Kulingana na uchumi wa Nchi yetu, ni vigumu moja kwa moja kujenga mabweni kwa mkupuo katika shule zetu za Msingi na Sekondari ili kuhifadhi wanafunzi hasa wale wanaotoka mbali na maeneo ya shule.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Human Rights Watch(February 14, 2017), wanafunzi wengi wanasafiri umbali mrefu, na wengi katika maeneo wanayoishi hakuna shule za kata. Hali hii si nzuri kwa maendeleo ya mwanafunzi na hata elimu kwa ujumla.

Hivyo, nikiwa kama mwananchi yeyote aliye huru kwenye nchi yake, ningependa kuishauri serikali yetu hasa kupitia wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na wadau na wahisani mbali mbali wa Elimu, iwekeze kwenye usafiri kwa kununua MABASI ya kusafirisha wanafunzi wa shule hasa za msingi na Sekondari.
Inaweza ikatumia mfumo wangu wa kiushauri au hata kuuboresha zaidi panapohitajika km ifuatavyo;-

MOJA: Serikali inunue mabasi kwa kila wilaya kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi kutoka kituo hadi kituo, kutoka shule hadi shule.Ili kurahisisha zaidi, zinaweza kuteuliwa hata baadhi ya Wilaya hasa za mijini kwa ajili ya kufanyia majaribio kabla ya kusimika mfumo kamili wa usafirishaji. Hii itaondolea wanafunzi kero ya kukosa masomo hasa wale wanaotoka mbali na mazingira ya shule zao.

PILI: Serikali iajiri madereva na watumishi wengine wenye taaluma husika kwa ajili usafirishaji wa wanafunzi na usimamizi wa chombo cha usafiri husika(basi) kama ilivyo mifumo mingine ya usafiri km UDART, TRL, n.k. na waandikishwe mikataba maalum ya kazi km ilivyo kwa watumishi wengine rasmi wa serikali.

TATU: Mchango wa Shilingi mia mbili(Sh 200) kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya uendeshaji na matengenezo madogo madogo kwa basi husika(Hapa lazima kuwe na mhasibu wa basi husika). Hii itasaidia pia kupunguza kwa kiasi fulani mzigo kwa serikali kwa matumizi yasiyo ya lazima kutoka serikali kuu.

NNE: Serikali igharamikie matengenezo ya kawaida na yasiyo ya kawaida(kama ajali) kwenye gereji za serikali na kuwe na sheria kali za kulinda mabasi hayo ili kukabiliana na hujuma zinazoweza kufanywa na watumishi wake au Raia wengine. Na pia serikali igharamikie kulipia bima ya mabasi hayo km inavyofanya kwenye magari na mabasi ya taasisi zake.

TANO: Wilaya husika iliyokabidhiwa hayo mabasi ya usafirishaji wa wanafunzi lazima isimamie muongozo na uendeshaji wake ili kuleta tija. Hii ni pamoja na kusimamia maadili ya kazi kwa watumishi wake.

SITA: Serikali iongeze pesa zaidi kwenye wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi na kwenye mfuko wa kuinua Elimu nchini kwenye bajeti yake ya kila mwaka ili kusaidia uboreshaji na ununuzi wa mabasi zaidi kila panapohitajika. Hii pia ni pamoja na kushirikisha wadau na wahisani mbalimbali wa Elimu pamoja na michango mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

SABA: Kuwepo na usimamizi maalum au utungaji maalum wa sera na sheria zinazomlinda au kumuongoza mwanafunzi au mfanyakazi awapo kwenye usafiri.

FAIDA ZA MFUMO.
Kila kitu huwa kina kasoro hata kama kikiwa kizuri zaidi km ilivyo kwenye uumbaji. Lakini pia chenye kasoro/changamoto kikiboreshwa huweza kuleta faida zaidi ya kasoro/changamoto hasa zikitatuliwa mapema au hata zikijitokeza mbeleni. Zifuatazo ni faida za kutumia mfumo huu wa usafiri kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini Tanzania;

MOJA: Kuongeza ufaulu kwa wanafunzi. Hii ni kwa sababu wanafunzi wengi wataweza kuwahi masomo kwa wakati muafaka pasipo kukosa vipindi hasa vya asubuhi tofauti na sasa wanafunzi wanatumia usafiri wa umma ambao hauna ratiba maalum. Kukiwa na mabasi haya yatakuwa yanaenda na ratiba maalum ya kuwahisha wanafunzi kwenye masomo(Mfano basi za shule binafsi huwa zinaenda na ratiba maalum ya kuwahisha wanafunzi kwenye masomo.

MBILI: Kupunguza kero za usafiri kwa wanafunzi hasa inapotokea migomo ya madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma hali inayopelekea wanafunzi kukosa masomo na mitihani hasa wale wanaotoka mbali na mazingira ya shule husika hali inayopelekea baadhi kutojiamini kwenye Elimu na hatimaye msongo wa mawazo.

TATU: Kupunguza viashiria vya unyanyasaji kwa wanafunzi vinavyofanywa na baadhi makondakta na madereva wa vyombo vya usafiri wa umma kulingana na nauli ya Sh 200 kuwa ndogo tofauti na nauli za abiria wa kawaida.

NNE: Kupunguza viashiria vya vishawishi kwa wanafunzi hasa wa kike kujihusisha na mapenzi ili kumudu au kulipia usafiri wa kumpeleka au kumtoa shuleni hasa kwa wanafunzi wa shule za vijiji kulipo na uhaba wa usafiri. Hii pia itasaidia kupunguza ujauzito kwa wanafunzi shuleni na pia kupunguza vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa na watu wasio wema kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

TANO: Mfumo huu utazalisha ajira hasa kwa madereva na wasimamizi wengine wa mfumo huu. Hii itasaidia kupunguza kwa kiasi fulani wimbi la ukosefu wa ajira kwenye nchi yetu Tanzania hasa kwa wasomi na wana taaluma mbalimbali wasio na ajira nchini.

SITA: Kuwezesha Wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya usafiri kwa watoto wao tofauti na ilivyo sasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutumia usafiri wa umma na abiria wa kawaida hali inayopelekea mzazi na mlezi kushindwa kuelewa mwanafunzi alitumia usafiri upi uliomfikisha shuleni. Hii pia itawezesha wazazi na walezi kutokuwa na mashaka na kuendelea kuamini zaidi mfumo huu.

HITIMISHO.
Elimu haina mwisho na pia Elimu ni gharama ili kupata maendeleo sahihi ya jamii husika. Hivyo basi, serikali haina budi kugharamikia usafiri kwa wanafunzi wake kupitia kodi za wazazi wao, ndugu zao, n.k. Na ili kuuboresha zaidi mfumo huu, Serikali ihusishe wataalam kutoka nchi nyingine zilizoendelea ambazo zinatumia mfumo huu.
Nawakaribisha kwenye huu mjadala ndugu wadau wa Jamii forums na Watanzania wenzangu kwa ujumla. Ahsanteni.

MAELEZO YA PICHA;
1) Wanafunzi wakigombea usafiri wa Umma.
gar.jpg

Chanzo: Gazeti la Mwananchi(March 01, 2018).
2)Wanafunzi wakigombea usafiri wa Umma.
Chanzo: IPP Media(Jan 18, 2022).
 
Upvote 5

gachacha

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
2,416
3,568
Ngoja waziri wa elimu aje kusoma haya maoni yako.

Kama Ambulance ni pasua kichwa hadi wagonjwa wanajaza mafuta sembuse basi la kusubilia ruzuku.

Nakumbuka kipindi nasoma shule za secondary zilikuwa na malori, saivi yako juu ya mawe.
 

feyzal

JF-Expert Member
Apr 20, 2016
6,036
10,267
Solution kila mwanafunzi wa day asome katika kata yake,huku serikali ikiziboresha shule zote za kata kwa walimu na mahitaji yote..itapunguza hiyo shida.Wanafunzi ambao wanaufaulu mkubwa hao wakipelekwa hizo shule wanazoziita za vipaji maalumu basi wakae huko huko hadi likizo.

Serikali ikileta magari haitasaidia sana sana itajibebesha mzigo mzito wa uendeshaji usiokua na faida kwa kutoa ruzuku kila mwezi.
 
Jul 19, 2022
49
41
Ngoja waziri wa elimu aje kusoma haya maoni yako.

Kama Ambulance ni pasua kichwa hadi wagonjwa wanajaza mafuta sembuse basi la kusubilia ruzuku.

Nakumbuka kipindi nasoma shule za secondary zilikuwa na malori, saivi yako juu ya mawe.
Ahahaha, wagonjwa tu wanateseka ni kweli lakin usafir kwa WANAFUNZI ni muhimu bhas tu ndo mfumo wa serikali upo hv no way
 

DON YRN

Member
Jan 14, 2019
62
112
Solution kila mwanafunzi wa day asome katika kata yake,huku serikali ikiziboresha shule zote za kata kwa walimu na mahitaji yote..itapunguza hiyo shida.Wanafunzi ambao wanaufaulu mkubwa hao wakipelekwa hizo shule wanazoziita za vipaji maalumu basi wakae huko huko hadi likizo.

Serikali ikileta magari haitasaidia sana sana itajibebesha mzigo mzito wa uendeshaji usiokua na faida kwa kutoa ruzuku kila mwezi.
Kila sehemu lazima kuwe na changamoto na hata kuendesha nchi pia ni changamoto, lakini changamoto ya sasa ni kubwa mno kwa wanafunzi kutumia usafiri wa umma. Kukiwa na mabasi maalumu ya kusafirisha wanafunzi kwenda na kurudi shule itakuwa bora zaidi maana hata zikitokea changamoto itakuwa rahisi kuzitatua maana zitakuwa za moja kwa moja.
 

DON YRN

Member
Jan 14, 2019
62
112
Ngoja waziri wa elimu aje kusoma haya maoni yako.

Kama Ambulance ni pasua kichwa hadi wagonjwa wanajaza mafuta sembuse basi la kusubilia ruzuku.

Nakumbuka kipindi nasoma shule za secondary zilikuwa na malori, saivi yako juu ya mawe.
Wanaweza kuanza na baadhi ya sehemu ili kuangalia changamoto zinazoweza kujitokeza kisha wakazitafutia ufumbuzi.
 

feyzal

JF-Expert Member
Apr 20, 2016
6,036
10,267
Kila sehemu lazima kuwe na changamoto na hata kuendesha nchi pia ni changamoto, lakini changamoto ya sasa ni kubwa mno kwa wanafunzi kutumia usafiri wa umma. Kukiwa na mabasi maalumu ya kusafirisha wanafunzi kwenda na kurudi shule itakuwa bora zaidi maana hata zikitokea changamoto itakuwa rahisi kuzitatua maana zitakuwa za moja kwa moja.
Gharama za uendeshaji ni kubwa mzee,ngumu sana hiyo kutokana na serikali yetu tegemezi inakopa ili kuendesha mambo yake.
 

DON YRN

Member
Jan 14, 2019
62
112
Gharama za uendeshaji ni kubwa mzee,ngumu sana hiyo kutokana na serikali yetu tegemezi inakopa ili kuendesha mambo yake.
Siyo vibaya ikikopa na kuendesha mambo yake km haya ya usafiri kwa wanafunzi. Nadhani kinachokwamisha maendeleo Tanzania yetu ni rushwa, TAKUKURU wakisimama nafasi yao kiuweledi hakuna kitakachoshindikana.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

2 Reactions
Reply
Top Bottom