Serikali ya Tanzania isikilize kilio cha huyu mama mjane

peno hasegawa

JF-Expert Member
Feb 24, 2016
12,809
21,410
Kwa miaka minane mjane Zubeda Mhina amekuwa akiingia na kutoka katika ofisi za kampuni ya bima ya Mwananchi Insurance Company Limited na Mamlaka ya Udhibiti wa Shuguli za Bima (Tira) kudai fidia ya Sh4 milioni bila mafanikio.

Zubeda anadai fidia hiyo baada ya mume wake kufariki katika ajali ya gari mwaka 2014.

Baada ya kuzunguka kwa muda mrefu, mama huyu wa watoto sita amepoteza imani na watendaji wa bima na sasa anaamini mtu pekee anayeweza kumsaidia ni Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nimehangaika hadi nimekamilisha kila nyaraka inayotakiwa ili nilipwe fidia, lakini kulipwa imekuwa taabu sana. Mume wangu ameniacha na watoto wa kusomesha, napata taabu sana, naomba msaada kwa mama Samia mimi nilipwe, nimechoka na hili suala,” anasema Zubeda kwa uchungu.

Machi 6, 2014 akiwa anaendelea na shughuli za kila siku nyumbani kwake Tabata Kisiwani, Zubeda alipokea taarifa kuwa mumewe, Ally Salum Ngoma, alikuwa amepata ajali mbaya eneo la Bwawani katika Barabara kuu ya Dar es Salaam - Morogoro.

Lori la mafuta alilokuwa akiendesha liligongana uso kwa uso na basi la abiria na kusababisha afariki pale pale.

“Nilipata taarifa mume wangu amepata ajali mbaya na nilipotaka kuchukua usafiri niende niliambiwa ‘rudi tu nyumbani, ajali ni mbaya sana.’ Baadaye taarifa ikaja kuwa mume wangu amefariki. Yeye alifia mule mule ndani ya gari. Wenzake wawili walitoka wazima,” anasema Zubeda.

Anasema marehemu alikuwa akiendesha lori lililomilikiwa na kampuni ya mafuta ya Oil Com.

Anafafanua baada ya kukamilisha taratibu zote za kuchukua mwili, Zubeda alishirikiana na ndugu zake kumzika mume wake na baada ya mazishi alielekezwa kufuatilia faili la ajali katika Kituo cha Polisi Chalinze.

“Nilitaka nijue namna ya kupata haki za mume wangu ili nifanye madai. Polisi Chalinze wakatuambia tusubiri faili litaletwa Kibaha. Tulisubiri miezi minne. Kila tukienda wanasema ‘mpaka hukumu isomwe ndio mpate faili.’

Baada ya safari nyingi kati ya Dar es Salaam na Chalinze, hatimaye Zubeda alifanikiwa kupata nakala ya hukumu ya kesi aliyoshtakiwa dereva wa basi ambaye naye alifariki akipatiwa matibabu.

Baada ya kukusanya nyaraka zote zinazohusiana na ajali hiyo, mwaka 2015 Zubeda alikwenda katika ofisi za kampuni ya bima ya Mwananchi Insurance Company Limited (MIC) zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam kuwasilisha madai.

“Baada ya kuzungumza nao wakaniambia tukakae kikao na tuorodheshe mali za marehemu. Tuliorodhesha na kupata Sh25 milioni. Nikapeleka ile orodha na madai, wakaniambia nije siku nyingine.

“Walinipa fomu ya kujaza ambayo walipunguza madai yetu hadi kufikia Sh4.5. Wakaniambia turudi nayo nyumbani tukajadili tena na tukikubaliana na hicho kiasi twende ofisi ya Serikali ya Mtaa tukatie saini makubaliano yetu. Mimi sikuwa na haja ya kwenda mahakamani kushtaki. Nikafanya kama walivyotaka.

“Niliporudi siku nyingine MIC na nyaraka zilizosainiwa, ofisa wao akauliza ‘mmeafiki hili fungu?’ Nikamjibu ndio. Akanipa tarehe ya kurudi tena. Tarehe ilipofika nikaenda, nilimkuta mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la John, akaniambia madai yangu bado yanashughulikiwa. Akanipa tarehe nyingine.

“Siku nilipokwenda nilimkuta mtu mwingine, naye akanipangia tarehe. Siku nilipokwenda nikakuta ofisi imefungwa. Nikaamua kwenda Tira (Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima) wakaniambia hii kampuni (MIC) ina kesi tangu mwaka 2012.

“Nikahoji kama walikuwa na kesi mbona wamenipa karatasi ya malipo?” Analalamika mjane huyo.

Anasema baada ya kubisha hodi Tira, mamlaka hiyo ilimtaka aandike barua ya maombi ya kulipwa haraka ambayo nakala yake Mwananchi imeiona.

Anasema Februari 16, 2016, Tira walijibu barua ya Zubeda wakimjulisha kuwa mamlaka hiyo isingeweza kushughulikia madai yake wakati huo, kwa kuwa kulikuwa na kesi iliyokuwa ikihusisha kampuni ya MIC iliyokuwa ikiendelea katika Mahakama Kuu (Divisheni ya Biashara).

Sehemu ya barua hiyo inasomeka: “Kwa sasa Mamlaka ya Bima haiwezi kushughulikia madai yako, kwani kampni hiyo bado ina kesi inayoendelea katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

“Hivyo tunakushauri usubiri uamuzi wa Mahakama au ufungue shauri la madai mahakamani dhidi ya kampuni hiyo, lakini mamlaka haiwezi kushughulikia madai dhidi ya kampuni iliyoko mahakamani,” ilisema sehemu ya barua hiyo, iliyosainiwa na P.J Ngwembe na M. Robert, kwa niaba ya Kamishna wa Bima nchini.

Tangu wakati huo, madai ya Zubeda yamekwama. Amekuwa akiingia katika ofisi mbalimbali kuomba asaidiwe kupata haki yake bila mafanikio.

Mwaka 2019 alirudi tena Tira kufuatilia hatima ya malipo yake na kujibiwa kuwa kesi iliyokuwa imezuia malipo yake ilikwisha na Tira ilishinda.

“Nikapelekwa kwa mwanasheria wa Tira mwanamke. Akashangaa sana, akauliza kwa nini sijaingizwa kwenye orodha wa walipwaji,” anasema.

Kwa mujibu wa Zibeda aliingizwa kwenye orodha ya watu wanaotakiwa kulipwa na MIC na kupewa tarehe ambayo angelipwa.

“Niliporudi mtu aliyeniingiza kwenye orodha malipo akaniambia MIC wamekata rufaa, kwa hiyo sitaweza kulipwa hadi rufaa hiyo isikilizwe,” anasema Zubeda huku akitokwa machozi.

Mwananchi imeelezwa kuwa hivi sasa wamiliki wa MIC wamekata rufaa Mahakama ya Rufaa baada ya kushindwa kesi katika Mahakama Kuu (Divisheni ya Biashara).

Kampuni hiyo ambayo ni muflisi inaelezwa kudaiwa mamilioni ya fedha na wateja baada ya kushindwa kulipa bima.

“Ni suala complex (gumu) kidogo. Barua zote za nama hii (kama iliyoandikwa na Zubeda kwenda Tira) bado hazijafanyiwa kazi. Itabidi zisubiri hadi uamuzi wa Mahakama utoke,” alisema Meneja uhusiano wa Tira, Oyuke Phostine.

Kwa mujibu wa Sheri ya Bima, kampuni ya bima hairuhusiwi kufanya biashara nchini bila mtaji wa kutosha. Pia hutakiwa kuwa na dhamana ambayo hushikiliwa na Benki Kuu (BoT).

Fedha hizo haziwezi kutolewa BoT bila idhini ya Kamishna wa Bima Tanzania. “Hizi ndizo zinaweza kutumika kulipa watu wanaoidai,” alisema Phostine.

Zubeda amewahi kupeleka malalamiko yake kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo Paul Makonda ambayo ilimwandikia barua aende MIC.

“Nilipoenda MIC wakasema hawaitambui hospitali iliyothibitisha kuwa mume wangu amekufa. Nikarudi hadi Hospitali ya Bwawani walikohifadhi mwili wa marehemu mume wangu baada ya ajali, wakanipa cheti cha uthibitisho wa kifo.

“Kila kitu kimekamilika lakini taabu inakuja kwenye kulipa. Mume ameniachia watoto wa kusomesha. Napata taabu sana. Naomba msaada hata kwa mama Samia ili mimi mjane nilipwe. Naadhirika na watoto hawa.

“Nimelazimika kuridhia malipo ya Sh4 milioni badala ya Sh25 milioni alizostahili kukwepa kwenda mahakamani, kumbe ningejua ningepeleka kesi mahakamani tangu mwanzo labda ingekuwa imekwisha,” analalamika Zubeda.

Chanzo: Mwananchi
 
nashukuru Mungu huku aliponiweka maana angeniweka kuwa ktika sheria walahi hawa wanaonea watu wangeenda jela kbsaaa
halafu hizi kampuni za Bima zimekuwa janja janja sana
 
Back
Top Bottom