Serikali ya Tanganyika ipo kisheria

Gavana

JF-Expert Member
Jul 19, 2008
33,233
8,779
Serikali ya Tanganyika ipo kisheria

Mwaka 1964 Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika walikubaliana kuanzisha ushirika wao unaoitwa Serikali ya Muungano.

Katika kulinda heshima ya mataifa yao viongozi hao waliweka saini Mkataba wa Makubaliano yao.Mkataba huo wa kimataifa kati ya nchi mbili hizi ndio unaitwa Mkataba wa Makubaliano wa 1964 na kwa kila sifa ni mkataba wa kimataifa unaostahiki kuheshimiwa.Kwa hivyo haiwezekani na ni upotoshaji wa makusudi kwa hivi sasa mjadala wa nchi mbili hizi zilizoungana kutekwa nyara na vyombo visivyohusika.Kwa lugha nyepesi,mjadala wa Muungano na matatizo yake ni mjadala wa wale waliounda Muungano huo,yaani,Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.Au tuseme hivi: Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa pamoja ndiwo waumbaji (creators) wa Muungano;Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kiumbe(creature) kinachotokana na uumbaji wao.Kama panahitajika mazungumzo yoyote juu ya umbo la kiumbe hicho itakuwa baina ya waumbaji wawili hao,sio baina ya kile kiumbe na mmoja wa waumbaji.

Wale wanaojaribu kukwepa mjadala wa kina juu ya muundo wa Muungano siku zote hutumia hoja kwamba eti hakuna Serikali ya Tanganyika na hivyo isingewezekana kufanya mazungumzo kati ya serikali hiyo na ile ya Zanzibar.Hoja hii ni dhaifu,maana yoyote yule atakayeulizwa muungano huu ni wa nani na nani atajibu ni wa Serikali ya Tanganyika na Seikali ya Zanzibar.Hawa ndiwo waliofanya Mkataba.Sasa kama kweli Serikali ya Tanganyika haipo,nani kaifuta na vipi ? Zaidi,Waswahili wanasema, “Yaliyopita sindwele,tugange lijalo”.Kama kweli kuna nia ya kuuenzi,kuulinda na kuuimarisha Muungano,basi tuangalie namna ya kuirejesha Tanganyika katika nafasi yake ili mjadala wa muungano huu upate wenyewe wa kuujadili.

Haikufutwa

Katika makubaliano ya kimataifa yaliyounda Muungano,ambayo hata hivyo katika muda wote wa uhai wa Muungano yamekuwa hayafuatwi,hakuna kifungu hata kimoja kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya Tanganyika ifutwe kwa mujibu wa makubaliano hayo.Serikali ya Tanganyika,kama ilivyo ile ya Zanzibar,imelindwa na kifungu Na. (V) pale kinaposomeka kwamba: The existing law of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their existing territories. Kinachosemwa hapa ni kwamba “Sheria ziliyopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kufanya kazi katika maeneo yao.”

Wataalamu wa katiba na sheria wanafahamu kwamba katiba ndio sheria mama ya sheria zote za nchin.Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali yake iwepo,pamoja na viongozi wake kuwapo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano.Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye Muungano.Hiyo ndio tafsiri ya ‘maeneo yao’.

Wazanzibari wanafahamu kwamba Serikali ya Tanganyika imefutwa kwa makusudi na Bunge la Tanganyika kinyume na Makubaliano ya Muungano ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano,kama kamba ndio Serikali ya Tanganhika.Lengo ni hatimaye kuiuwa Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya,yaani,kuwa nchi moja yenye Serikali Moja.Hiyo ndio ghilba iliyofanywa na viongozi wa Tanganyika mara baada ya kuwekwa saini makubaliano.Kwa kusaidia kufichuwa ukweli wa hadaa hii,msomaji anashauriwa asome Sheria Na. 22 ya mwaka 1964 inayoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar,1964”.Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Tanganyika Aprili 25,1964,siku moja kabla Muungano kuanza kufanya kazi.Ilikusudiwa kuthibisha kukubalika muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar upande wa Tanganyika (ratification).Kifungu cha (viii) cha Makubaliano ya Muungano kinaagiza ifanyike hivyo kwa pande zote mbili za Muungano.Inasikitisha kusoma katika kifungu Na. 2 cha sheria hiyo kwamba, “Sheria iliyopo maana yake sheria iliyoandikwa kama ilivyo muda tu kabla siku ya Muungano lakini haiingizi Katiba ya Tanganyika kwa mintaraf ya Serikali ya Jamhuri Tanganyika au tamko lolote au sheria au kifungu ambacho kinafutika kwa kuanza kufanya kazi Katiba ya Muda.” (Existing law means the written and unwritten law as it exists immediately before Union Day but does not include the Constitution of Tanganyika in so far as it provides for the Government of the Republic of Tanganyika or any declaration or law or any provision which expires with effect from commencement of the Interim Constitution”) Kwa hivyo,wakati Bunge la Tanganyika linapitisha sheria ya kukubali kuwepo kwa Muungano kwa upande wa Tanganyika,sheria hiyo ilianza kupinga vifungu vya makubaliano hayo.Mfano mwengine ni kifungu Na. 7 cha sheria hiyo kinachosema: “Itapoanza kufanya kazi Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar,Katiba ya Tanganyika itasita kuwa na maana kwa Serikali ya Tanganyika kama sehemu moja ya Jamhui ya Muungano.” (On the commencement of the Interim Consitution of the United Republic of Tanganyika and Zanzibar,the Constitution of Tanganyika will cease will cease to have effect for the Government Tanganyika as a separate part of the United Republic”). Kwa maneno mengine,sheria ambazo zilitakiwa zitumike kwa Tanganyika kwa mambo ambayo si ya Muungano eti zisijumuishe Katiba ya Tanganyika.

Kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu vya sheria hii hakukubadilisha makubaliano yaliyokwisha kuwekwa saini kati ya Serikali mbili zilizounda Muungano,yaliyosema kwamba sheria za nchi mbili hizi zitaendelea kutumika katika maeneo yao.Bunge la Tanganyika,na hata lile la Muungano,halikuwa na mamlaka kutafsiri vifungu vya Mkataba wa Muungano.Kama Mkataba ulitakiwa kutafsiriwa basi ni walioandika rasimu ya mkataba huo ndiwo walipaswa kutoa tafsiri ya vifungu vyake,tafsiri ambayo ingepaswa iwe sehemu ya Mkataba huo.Na wala makubaliano yale hayakufuta wadhifa wa Rais wa Tanganyika.Si hivyo tu,bali pia Katiba ya Muungano ambayo ilitakiwa iwe ya mwaka mmoja (interim)ilikuwa ni ile ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho kwa ajili ya kutumika kwa Serikali ya Muungano.Haikuruhusiwa kutumika kuiongoza Tanganyika kwa sababu Tanganyika ilikuwa na Katiba yake na Rais wake.Mwalimu Nyerere alikuwa na vyeo viwili,Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu Katiba ya Muungano na Rais wa Tanganyika kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika,kama alivyokuwa Mzee Karume, ambaye aliendelea kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kubaki Rais wa Zanzibar.Hivyo ndivo makubaliano yalivyo hadi hii leo.Waliobadilika ni watu.Kufanya vinginevyo ni kinyume na makubaliano yale na ndio sababu ya migogoro ya Muungano.Yaliyofanyika ni ujanja uliokuwa hauna nia njema kwa Zanzibar kama alivyosema Profesa Issa Shivji,mtaalamu wa Katiba wa Chuo Kikuu cha Dar er Salaam.

“Lakini yote ya kuepusha Serikali ya Tanganyika kuwepo yalifanywa kwa makusudi kabisa,ili itumike Serikali ya Muungano kama ndio Tanganyika.Katika Sheria lie Na. 22 ya 1964,Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga na kutoa maagizo yanayohusu Muungano kwa kutumia amri(decrees) za sheria ya Tanganyika.Siku ile inapopitishwa sheria ile zilipitishwa pia Decrees mbili zilizotokana na vifungu Na.6 (3),cha 8 na cha 5 cha sheria hiyo Na.22 1964,yaani,The Provisional Transitional Decree 1964,na ile ya Interim Constitution Decree 1964 ambazo zote hazikuwa halali maana ni Decrees zilizopitishwa na Bunge la Tanganyika zilizotokana na Sheria Na.22 ya 1964 ya Tanganyika.”

Miongoni mwa vilivyodhirisha kuwa hakukwa na nia njema ni pale wafanya kazi wa Serikali ya Tanganyika wote walipopandishwa vyeo kwa pamoja na kuwa wafanyakazi wa Muungano kama kifungu cha 3 (1) cha Provisional Transitional Decree kinavyosema: “Every person who holds office in the service of the Republic of Tanganyika immediately before the Union Day, shall on Union Day be deemed to have been elected,appointed or otherwise selected to the corresponding office in the service of the United Republic.” Yaani kila mfanya kazi aliyekuwa wa Serikali ya Tanganyika kufumba na kufumbuwa anakuwa mfanya kazi wa Serikali ya Muungano kwa uchawi wa kifimbo cha Mwalimu Nyereer.Huu ni ujambazi wa kikatiba (constitutional banditry).Vivyo hivyo kifungu cha 6 cha (i) cha Decree kinasema mara tu baada kuanza Muungano,Mahkama ya Tanganyika na Majaji wake wote nao watakuwa ndiwo majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano.Mpaka leo Katiba zote mbili hazitambuwi kuwepo kwa mahkama tatu.Nembo ya Tanganyika inatumika kama nembo ya Serikali ya Muungano na Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika inachukliwa kama Idara ya Mwanasheria Mkuu Tanzania.

Haya yote hayamo na ni kinyume na Makubaliano ya 1964.Yote haya na kile kifungu cha 7 cha Sheria Na. 22 ya 1964 kinachofuta kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika hayakubadilisha na wala hayana mahusiano na Makubaliano ya Muungano ya 1964.Yote haya yalifanywa na Bunge la Tanganyika kwa maslahi ya Tanganyika nje ya Makubaliano.Kwa mujibu wa Makubaliano hayo,yafuatayo lazima yaheshimiwe:-

  • Katiba ya Zanzibar itumike Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano.
  • Katiba ya Tanganyika (ile iliyokuwepo kabla kurekebishwa kuingiza mambo ya muungano)itumike Tanganyika kwa mambo yasiyo ya muungano.
  • Iwepo Serikali ya Tanganyika inayoshughulika na mambo yasiyo ya muungano,kama Serikali ya Zanzibar inavyoshughulikia mambo yake ambayo si ya muungano.
  • Wafanya kazi wa Tanganyika wasihusike na mambo ya muungano,wawe katika ‘civil service’ (mfumo wa wafanya kazi)ya Tanganyika,kama walivyo wa Zanzibar kwa Zanzibar (wasio wa Muungano kama Uhamiaji na wengine)
  • Iundwe Tume ya kutayarisha rasimu ya Katiba ya Muungano ambayo itajadiliwa na Bunge la Katiba.

Haya yalibidi yafanyike mwaka mmoja tu baada ya kuanza Muungano.Hata hivyo,Waingereza wanasema, “Better late than never’(chelewa ufike)Wakati ndiwo huu ikiwa tunataka Muungano wa kweli,Muungano wa haki kwa pande zote mbili.Vinginevyo Wazanzibari wasije wakalaumiwa wakifika mahali wakasema “Enough is enough” (“Tumechoka na maonevu”).Pa kuanzia ni kutambuwa kuwa kuna Serikali ya Tanganyika na ndio inayoweza kuzungumza na Serikali ya Zanzibar kama wawakilishi wa Dola mbili zilizounda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama ulivyojulikana (Tanzania ni usanifu tu uliobuniwa kufupisha jina).
 
Back
Top Bottom