Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imependekeza sheria kali ya kupambana na vitendo vya rushwa

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
Written by amini

rushwa.jpg
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imependekeza sheria kali ya kupambana na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi na watendaji wenye tabia ya kuomba ngono kabla ya kutoa ajira au kumpandisha cheo mfanyakazi.
Sheria hizo zimo katika mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar, inayotarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa umma na Utawala bora Haji Omar Kheir, Januari 18, mwaka huu.

Muswada huo umesema kwamba itakuwa kosa la jinai kwa mwanasiasa yeyote kumpa mtu rushwa kwa nia ya kumshawishi mtu huyo au mwingine yeyote kupiga kura au kuacha kupiga kura wakati wa uchaguzi.

"Mtu yeyote kwa nia ya kuathiri utaratibu wa upigaji wa kura wakati wa uchaguzi wowote, atampa rushwa mtu mwingine yeyote, ama moja kwa moja au vinginevyo atakuwa ametenda kosa." Kimesema Kifungu cha 56 (1) cha muswada huo.

Sheria hiyo imesema kwamba mpiga kura yeyote atakayekubali kushawishiwa kwa kupokea rushwa kwa misingi hiyo atakuwa ametenda kosa la rushwa katika uchaguzi huo.

Aidha, sheria hiyo imeweka adhabu kali kwa viongozi au watendaji ambao wamekuwa wakitumia vibaya mamlaka au madaraka kwa kudai au kuomba ngono kwa mtu yeyote kama sharti la kutoa ajira au kupandishwa cheo kazini.

"Mtu yoyote mwenye madaraka atakuwa amefanya kosa na atakapopatikana na hatia atawajibika kulipa faini isiyopungua Shilingi Milioni tatu au kifungo kisichopungua miaka miwili jela." Imesisitizwa katika kifungu cha 58 cha Muswada huo.

Kwa mujibu wa muswada huo mtu yeyote (Kuwadi) kwa makusudi akibainika alishiriki kutoa ushauri, kutoa ushawishi au kusadia kufanyika kwa makosa ya aina hiyo pia atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria.

Muswada huo wa sheria pia umeweka adhabu kwa watu wenye tabia ya kutoa na kupokea rushwa ili kuhakikisha tatizo hilo linatoweka kwa wananchi Zanzibar.

Aidha, sheria hiyo imesema kwamba mmiliki halali katika mali yoyote iliyopatikana au iliyotokana na vitendo vya kosa la rushwa au kuhujumu uchumi itarejeshwa kwa mmiliki halali wa mali hiyo.

Hata hivyo sheria hiyo imesema katika kesi za rushwa na hujumu uchumi kama kutakosekana mmiliki halali mahakama itakuwa na uwezo wa kukamata mali hiyo na kupelekwa serikalini.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom