Serikali ya Awamu ya Sita, inaunga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili

JUMA JUMA

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
664
829
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tannzania inathamini mchango wa vyombo vya habari katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani na kuifanya lugha hiyo kuwa yenye hadhi.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani Machi 14, 2022, Katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.

“Serikali ya Awamu ya Sita, inaunga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili. Itakumbukwa kuwa toka tulipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwezi Machi 2021, kumekuwa na viashirio vingi vinavyoonyesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hasaan inavyounga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili” amesema Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa lugha ya Kiswahili imekuwa bidhaa adhimu, watanzania, waandishi wa habari, watangazaji wanawajibu wa kuifanya lugha hiyo kuwa ya kwanza duniani ambayo inawazungumzaji wengi ikizingatiwa penye nia pana njia.

Aidha, katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaendelea kukua duniani, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali itaendelea kufundisha lugha ya Kiswahili kupitia Balozi mbalimbali za Tanzania duniani.

Zaidi ya hayo, Makamu wa Rais ametoa wito na kuwahimiza vijana kusoma na kuandika vitabu na majarida ya Kiswahili ambavyo vitawafikia watu wote ambayo yatasomwa na vizazi na vizazi na kuwafaa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Katika hotuba yake, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango ametumia fursa hiyo kuwapongeza Viongozi wa kiaifa kuanzia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kmbarage Nyerere, Rais Mstaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Hayati Rais Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi walizofanya katika juhudi ya kuikuza lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema lugha ya Kiswahili inaenea na kuenezwa haraka hususan kimataifa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na utashi wa watu wa mataifa mbalimbali wa kutaka kujifunza Kiswahili.

“Leo Kiswahili si mali ya Tanzania tu, bali Kiswahili kimepiga hodi kwenye mataifa mengi ya nje ambayo kwa sasa nayo yanatamani kutangaza, kufundisha na kuzungumza Kiswahili” amesema Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la vyombo vya habari ambavyo vinatumia lugha ya Kiswahili hapa nchini ambavyo idadi yake ni 172 na duniani idadi yake ni 36 ambapo baahi yao wamefika kwenye Kongamano hilo kwa kuwa ni jambo jema wanahabari kukutana, kupata elimu kuhusu lugha na kujadili kwa pamoja mambo yanayowahusu na kufahamishana fursa mbalimbali zinazopatikana duniani kwa kupitia tasnia ya habari na Kiswahili.

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa Wizara yake itahakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wataalamu wa Kiswahili kwa kushirikiana na Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuzitafuta na kuzifuata fursa kwa ubunifu zaidi ili kukamatia fursa zote zitakazojitokeza huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa "Kila jambo linawezekana, kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo.”

Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Dunia linaongozwa na kaulimbiu inayosema “Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani” likitanguliwa na kongamano la kwanza lilifanyika Novemba 12-15, 2007 likiongozwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu la kukieneza Kiswahili duniani kwa kukitumia na kutangaza katika vituo vyao vya habari.
 
Back
Top Bottom