Naipendatz

JF-Expert Member
Jul 27, 2011
5,080
8,217
Waziri wa Elimu Prof. Ndalichako amesema Wanafunzi wa Shule za Msingi/Sekondari watakaokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na changamoto za kifamilia watapewa nafasi ya kurejea Shuleni katika mfumo rasmi “leo leo natoa waraka zege halilali"

Mimba.jpg

======

Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako amesema Wanafunzi waliokatisha Masomo kutokana na sababu mbalimbali watapewa fursa za kurejea Shule. Ameeleza, Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa fursa za elimu

Amefafanua, "Fursa hizo zitajumuisha Wasichana ambao wanapata Ujauzito wakiwa Shule za Msingi na Sekondari. Wataruhusiwa kuendelea na Masomo yao katika Mfumo rasmi baada ya kujifungua"

====

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
TAARIFA YA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
MHE. PROF. JOYCE LAZARO NDALICHAKO (MB) KATIKA MKUTANO NA
VYOMBO VYA HABARI TAREHE 24 NOVEMBA, 2021 KUHUSU MAFANIKIO
YA WIZARA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA - TAREHE 24 NOVEMBA, 2021

Ndugu Wanahabari;
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Leo tupo hapa tukiendelea na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku hii salama tukiwa na afya njema. Aidha, Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha katika mkutano huu ambao unalenga kuelezea mafanikio ya Sekta ya Elimu wakati tunaadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Ninawashukuru kwa namna ambavyo ninyi waandishi mmekuwa mkiibua mijadala mbalimbali inayolenga kuboresha elimu yetu. Sisi kama Wizara tunaendelea kupokea michango yenu pamoja na ya wananchi wengine kwa ujumla ambao wanatoa maoni yao kuhusu masuala ya Elimu, sayansi na Teknolojia.

Ndugu Wanahabari;
Mara tu baada ya Tanganyika kujipatia Uhuru wake, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitangaza vita dhidi ya maadui watatu ambao ni Ujinga, Umasikini na Maradhi. Katika kupambana na adui hawa, hasa ujinga, Watanzania tumeendelea kushuhudia mafanikio na mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambayo ina mchango mkubwa katika kumkomboa Mtanzania dhidi ya adui ujinga. Ni dhahiri kuwa mapambano dhidi ya adui Ujinga ndiyo msingi wa mapambano dhidi ya Maradhi na Umaskini. Bila shaka yeyote ukiondoa Ujinga utakuwa pia umepunguza Maradhi pamoja na Umaskini.

Katika miaka 60 ya Uhuru, tumeshuhudia ongezeko kubwa la fursa za upatikanaji wa elimu katika ngazi zote za elimu. Hii imetokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya elimu na uimarishwaji wa mifumo ya uthibiti na ithibati ya elimu. Tunaendelea kushuhudia maendeleo katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Aidha, ushiriki wa sekta binafsi katika kutoa huduma za elimu nchini katika ngazi zote unaendelea kuimarika.

Ndugu Wanahabari;
Tunaposherehekea miaka 60 baada ya Uhuru wa nchi yetu, ni vizuri tujikumbushe tulikotoka, tulipo sasa na matarajio yetu ya baadaye.

Kumbukumbu za mapambano dhidi ya ujinga zinaturudisha hadi wakati wa Utawala wa Kijerumani na Kiingereza, ambapo kwa kiasi kikubwa elimu ilitolewa na Wamisionari. Elimu hiyo ilitolewa kufuatana na imani yao na historia ya nchi walikotoka ambapo walisisitiza zaidi uenezi wa dini.

Kulikuwa na shule chache za serikali za kikoloni. Shule ya kwanza nchini, Tanga School, ilijengwa na Wajerumani mwaka 1892. Aidha Waingereza walianzisha Tabora School mwaka 1922. Shule nyingine zilizokuwapo zilikuwa ni za madhehebu ya dini na waliosoma walikuwa ni wanafunzi wa dhehebu husika.

Kwa ujumla mifumo ya elimu kabla ya Uhuru ilikuwa na misingi ya ubaguzi wa rangi. Nafasi bora zaidi za elimu zilitolewa kwa watoto wa Kizungu na Kiasia kuliko watoto wa Kiafrika. Lengo kubwa la elimu lilikuwa ni kupata watumishi Waafrika ambao wangetumika katika kutetea matakwa Na maslahi ya wakoloni, pamoja na kufanya kazi za ofisini kama wahudumu na makarani.

(a) Elimu baada ya Azimio la Arusha
Katika historia ya Elimu Tanzania Bara, Azimio la Arusha ni tukio muhimu lililotoa mweleko mahsusi wa elimu na harakati za ujenzi wa Taifa kwa ujumla. Azimio hili lilitangazwa mwaka 1967 mjini Arusha na lengo lake lilikuwa ni kurekebisha kasoro zilizojitokeza baada ya Uhuru ili kujenga taifa linalofuata ‘Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea’. Siasa hiyo ilizaa Falsafa ya ‘Elimu ya Kujitegemea’, yenye lengo la kumkomboa Mtanzania kutokana na utegemezi.

Elimu ilitakiwa kuzingatia ujenzi wa maarifa, ujuzi, stadi na mwelekeo ya kupenda na kuthamini kazi kwa lengo la kumwezesha mhitimu kutumia rasilimali zilizo katika mazingira yake kwa maendelo yake binafsi, jamii na Taifa lake kwa ujumla. Sheria ya Elimu ya mwaka 1969 (Education ACT, 1969) ilitolewa ili kuwezesha utekelezaji wa mabadiliko ya elimu kulingana na tamko la Elimu ya Kujitegemea.

• Matumizi ya Lugha ya Kiswahili
Kufuatia Azimio la Arusha, mwaka 1968 ulitolewa mwongozo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kufundishia kwenye shule za msingi na katika kuendeshea mikutano ya walimu na wanafunzi katika shule za sekondari.

Sote ni mashahidi kwamba, matumizi ya Lugha ya Kiswahili yamewezesha kuleta umoja wa Kitaifa. Aidha, Kiswahili kimeendelea kutumika kikanda na hata katika ngazi ya kimataifa. Kwa sasa Kiswahili kinatambulika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).

• Mabadiliko ya Mitaala
Ubora wa mitaala ni jambo la msingi katika kuhakikisha kuwa nchi inatoa elimu stahiki. Tangu tulipopata Uhuru mwaka 1961, mitaala yetu imebadilishwa mara tano kama ifuatavyo:

Mabadiliko ya Kwanza ya mitaala yalifanyika Mwaka 1967 yakilenga kuondokana na mitaala ya kibaguzi iliyokuwa ikitolewa na wakoloni. Mitaala iliyoandaliwa ililenga kujenga uzalendo kwa kuzingatia Falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea. Mwelekeo wa mabadilliko ya mitaala hii ulikuwa ni kupambana na maadui watatu - Ujinga, Umaskini na Maradhi.

Mabadiliko ya pili yalifanyika Mwaka 1979 yakiwa na msisitizo kwenye elimu ya nadharia na vitendo ambapo masomo ya michepuo yalianzishwa rasmi. Hatua hiyo iliwezesha kuwa na shule za Ufundi, Kilimo, Biashara na Sayansi-Kimu. Lengo ilikuwa kuongeza stadi zitakazowawezesha wahitimu wa ngazi za Sekondari kujikwamua kiuchumi na kujengewa uwezo wa kujitegemea.

Mabadiliko ya tatu yalifanyika Mwaka 1997. Mabadiliko haya yalizingatia matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 1995 na mapendekezo ya Tume ya Makweta ya Mwaka 1982. Pamoja na mambo mengine, msisitizo uliwekwa katika kuboresha utoaji wa elimu kwa vitendo ili kujenga uwezo zaidi wa vijana katika kujikwamua kiuchumi huku wakijengewa ari na moyo wa uzalendo kwa nchi yao.

Mabadiliko ya nne yalifanyika Mwaka 2005 ambayo yalilenga kuingiza ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia ujenzi wa umahiri, yaani Competence-Based Curriculum. Mtaala huu pia uliweka msisitizo wa somo la TEHAMA pamoja na uchopekaji wa masuala mtambuka kama vile Elimu ya UKIMWI, Afya ya Uzazi, Stadi za Maisha, pamoja na utunzaji wa Mazingira.

Mabadiliko ya Tano yalifanyika mwaka 2014 kwa lengo la kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika Ngazi ya Elimu ya Awali, Darasa la 1 na la Pili.

Mapitio yanayoendelea Sasa ya Mitaala
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha elimu kwa kuhakikisha mitaala inayotumika inakidhi mahitaji sasa. Hivyo, Mheshimiwa Rais ameilekeza Wizara ya Elimu kufanya mapitio ya mitaala katika ngazi zote.

Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inajenga ujuzi na stadi zinazoendana na mahitaji ya sasa. Kazi hiyo ya maboresho ya mitaala inaendelea kufanyika. Wadau wa Elimu wanashirikishwa ili kupata maoni yatakayowezesha kupata mitaala yenye msisitizo katika kujenga ujuzi. Marekebisho hayo yatakapokamilika, yatakuwa ni marekebisho ya sita ya Mitaala tangu nchi yetu ilipopata Uhuru.

• Sera ya Elimu ya Watu Wazima ya Mwaka 1970
Moja kati ya mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ilikuwa ni kampeni ya kufuta ujinga kwa watu wazima. Kampeni hii ilitokana na Sera ya Elimu ya Watu Wazima ya mwaka 1970 ambayo ilitaka kila mtu mzima aweze kusoma, kuandika na kuhesabu. Mkakati uliwekwa wa kutimiza lengo hilo ifikapo Desemba 1975. Utekelezaji wa mpango huo wa kitaifa wa kufuta ujinga ulishika kasi na ulipata mafanikio makubwa sana kutokana na msukumo wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Kwanza wa Tanzania.

Mwalimu Nyerere alisisitiza juu ya umuhimu wa kufuta ujinga kwa ajili ya maendeleo na pia kumkomboa Mtanzania kifikra.
Ndugu Wanahabari;

Katika kupiga vita adui ujinga, hatua mbalimbali zilichukuliwa ili kupunguza idadi ya Watanzania wasiojua kusoma na kuandika. Hatua hizo ni pamoja na uanzishaji wa Programu za Kisomo Chenye Manufaa, Kisomo cha Kujiendeleza na Elimu ya
Wafanyakazi. Jitihada hizo zilizaa matunda na kuwezesha idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kupungua kutoka asilimia 48 mwaka 1970 hadi asilimia 22 mwaka 2012 (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012).

Elimu ya Watu Wazima ilitumika kuratibu Kampeni za Kitaifa za kuelimisha umma kuhusu masuala mtambuka ya maendeleo. Kampeni hizo ni pamoja na:

1. Kupanga ni Kuchagua (1969): Ililenga kushirikisha wananchi katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano;

2. Siasa ni Kilimo (1973): Ililenga kudumisha Kilimo cha Kisasa ili kuleta maendeleo;

3. Mtu ni Afya (1974): Ililenga kuelimisha Jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu;

4. Chakula ni Uhai (1975): Ililenga kuelimisha jamii kuhusu uzalishaji wa mazao ya chakula na umuhimu wa lishe bora;

5. Misitu ni Mali (1980): Ililenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza misitu ili kuzuia kuenea kwa jangwa nchini;

6. Elimu kwa Wapiga Kura (1995): ililenga kuelimisha jamii kuhusu demokrasia na namna ya kushiriki kugombea na kupiga kura katika uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi vya siasa; na

7. Tubadili Tabia Tushinde UKIMWI (2001): Ililenga kujenga uelewa kwa makundi yote ya jamii ya Watanzania juu ya janga la UKIMWI na athari zake.

• Tume ya Rais ya Elimu ya Mwaka 1982
Pamoja na mafanikio ambayo yalikuwa yamefikiwa katika sekta ya elimu, bado kulikuwa na haja ya kufanya tathmini ya kina na kupata maoni ya kuiwezesha elimu yetu kuwa bora zaidi. Hivyo mwaka 1982 iliundwa Tume Maalum ya Rais ya kufanya tathmini hiyo. Tume hiyo iliongozwa na Hayati Jackson Makweta na ilijulikana zaidi kama “Tume ya Makweta”. Majukumu makubwa ya Tume ilikuwa ni kufanya tathmini ya mfumo wa elimu uliokuwepo na kupendekeza mfumo unaozingatia hali halisi katika nchi kwa wakati huo.
Malengo mahsusi yalikuwa ni:

(i) kupata mambo yanayothaminiwa kitaifa, kijamii, kitamaduni na kimaadili ili yaweze kuzingatiwa katika utoaji wa elimu;

(ii) kubainisha malengo ya Elimu katika ngazi mbalimbali ili kila mmoja awe ameandaliwa vya kutosha kujitegemea kimaisha na kuliendeleza Taifa; na

(iii) kubainisha maandalizi yaliyotakiwa ili madhumuni na malengo ya elimu yaweze kufikiwa.

Moja ya mapendekezo ya Tume hiyo ilikuwa ni kuingizwa kwa Elimu ya Awali katika mfumo rasmi Hatimaye, Elimu ya Awali iliingizwa kwenye mfumo rasmi mwaka 1993. Pia Tume hiyo iliweka msisitizo katika kuongeza shule za sekondari.

Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha mfumo wa utoaji elimu ikiwa ni pamoja na kuanzisha Vyombo vya kuthibiti Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaani Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) 1994 na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo (NACTE) 1999. Kufuatia kuanzishwa kwa Vyombo hivyo, kumekuwa na uthibiti wa ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.

• Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (Universal Primary Education – UPE)
Mwaka 1977 Serikali ilianzisha “Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote” yaani Universal Primary Education – (UPE). Mpango huu ulikuwa na lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto wote. Kupitia mpango huu shule nyingi za msingi zilifunguliwa na kuandikisha watoto wengi zaidi. Aidha, ili kuleta ufanisi katika utekelezaji, wahitimu wa Darasa la Saba walipata Mafunzo ya Ualimu ili wafundishe Darasa la Tatu na Nne kwa kusaidiwa na walimu wakuu, ambapo baadae waliendelea na mafunzo na kuwa walimu kamili.

• Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)
Baada ya mafanikio makubwa ya Mpango wa UPE, serikali ilikuja na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM). Huu ulikuwa ni mpango wa kwanza katika Sekta ya Elimu na utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA). Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulianza mwaka 2002 ukiwa na malengo yafuatayo:
(i) Kuongeza uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya Msingi;
(ii) Kuinua ubora wa Elimu itolewayo;
(iii) Kujenga uwezo wa watendaji wa MMEM katika ngazi zote za usimamizi wa elimu;
(iv) Kuimarisha taratibu za Kitaasisi; na
(v) Kuimarisha elimu ya masuala mtambuka.

• Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES)
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) ulikuwa ni mpango wa pili katika Sekta ya Elimu wa utekelezaji Mkakati wa Serikali wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) baada ya ule wa Elimu ya Msingi (MMEM).

MMES ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka 2004 kwa Lengo Mahsusi la kuongeza idadi ya vijana wa Tanzania wanaosoma na kuhitimu Elimu ya Sekondari iliyo bora wakiwa na matokeo mazuri.

Ili kufikia lengo hili, MMES ulijikita katika maeneo makuu yafuatayo:
(i) Kuongeza upatikanaji wa Elimu ya Sekondari (access);
(ii) Kutoa elimu kwa uwiano sawa (equity);
(iii) Kuongeza ubora wa Elimu ya Sekondari (quality);
(iv) Kuboresha usimamizi na uendeshaji wa shule
(strengtherning Institutional arrangement); na
(v) Kuzingatia masuala mtambuka katika mitaala ya Elimu (cross-cutting issues).

Utekelezaji wa MMES ulikuwa na mafanikio makubwa katika kuongeza fursa za Elimu ya Sekondari. Tulishuhudia mpango wa ujenzi wa Sekondari za kata ukitekelezwa kwa kasi na kufanya idadi ya Shule za Sekondari kuongezeka kutoka 828 mwaka 2004 hadi 3,039 mwaka 2009. Hatua hiyo ililenga kuongeza shule mahali wanafunzi kuwapunguzia umbali mrefu waliokuwa wanatembea kufuata shule. Serikali imeendelea kuongeza Shule za Sekondari ambapo baadhi ya Kata zina shule zaidi ya moja.

Mafanikio Katika Sekta ya Elimu
Ndugu Wanahabari;
Sasa naomba nijielekeze katika mafanikio ya Sekta ya Elimu tangu nchi yetu ilipopata Uhuru. Mafanikio haya yametokana na kazi iliyotukuka iliyofanywa na serikali kwa awamu zote sita. Wadau mbalimbali wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii nzima ya Kitanzania imetoa mchango mkubwa katika mafanikio hayo. Hivyo, kwa niaba ya Serikali napenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote wa elimu hapa nchini ambao kwa pamoja tunajivunia mafanikio yalipatikana kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu.

• Elimu ya msingi na Sekondari Ndugu Wanahabari;
Katika Elimu ya msingi na sekondari, baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na:
• Kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi zilizosajiliwa kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 18,546 mwaka 2021. Kati ya shule 18,546, shule 16,656 ni za Serikali na 1,890 za Binafsi;

• Shule za sekondari zimeongezeka kutoka 41 mwaka 1961 ambapo shule 2 zilikuwa za Binafsi, hadi kufikia 5,460 mwaka 2021 ambapo shule 3,983 ni za Serikali na shule 1,287 ni za binafsi. Takwimu hizi zinaonesha wazi namna ambavyo baada ya kupata Uhuru, Serikali imetoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi kushiriki katika elimu.

Hali hii imewezesha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya sekondari kuongezeka kutoka wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 4,432 mwaka 1961 hadi wanafunzi 803,085 mwaka 2021. Ongezeko hilo limechangiwa na mikakati mbalimbali ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo ulioanza kutekelezwa 2016 chini ya Serikali ya Awamu ya Tano na unaendelea kutekelezwa. Pia ujenzi wa shule za sekondari za Kata uliofanyika kuanzia mwaka 2005 na unaendelea kufanyika hadi sasa umewezesha elimu ya sekondari kutolewa karibu na wanaposhi wanafunzi.

Serikali ya Awamu Sita Chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendeleza kwa vitendo upatikanaji wa fursa za elimu ya sekondari kwa wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi. Katika kipindi cha miezi nane tu tangu aliposhika hatamu ya uongozi wa nchi yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya sekondari 12,000 na KAZI hiyo INAENDELEA. Aidha, Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuongeza idadi ya shule za Kidato cha tano na Sita ili kuongeza fursa zaidi kwa wanafunzi A-level.

• Elimu Maalum Ndugu Wanahabari;
Elimu ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania bila kujali mazingira yake. Sera za Elimu zimekuwa zikisisitiza juu ya umuhimu wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo baadhi ya mafanikio yalipatikana ni pamoja na:

(i) Kuongezeka kwa idadi ya Shule za Msingi zinazochukua wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka shule nne za Wamisionari (Tabora, Buigiri, Irente na Uhuru Mchanganyiko) mwaka 1961 hadi kufikia shule 776 mwaka 2021. Shule za sekondari zimeongezeka kutoka shule moja (Mpwapwa sekondari) mwaka 1960 hadi kufikia shule 74 mwaka 2021.

(ii) Kuongezeka kwa Vyuo Vikuu vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka Chuo Kikuu kimoja cha Dar es Salaam mwaka 1961 hadi Vyuo Vikuu 11 mwaka 2021. Ongezeko hilo limetoa fursa kwa wanafunzi kuchagua vyuo na fani wanazotaka kusomea.

(iii) Kuanzishwa kwa Mafunzo ya Elimu Maalum mwaka 1976 ambapo Wizara ya Elimu ilianza kuandaa walimu kwa wanafunzi Wasioona na Viziwi katika Chuo cha Ualimu Tabora. Aidha, Mwaka 1983 Chuo cha Ualimu Tabora kilianza kuandaa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye Ulemavu wa Akili. Vilevile Mwaka 1996 Chuo cha Ualimu wa Elimu Maalumu Patandi kilianza kutoa kozi mbalimbali za Elimu Maalumu.

(iv) Ufundishaji wa lugha ya alama umeimarishwa ili kuwawezesha watoto viziwi kujifunza. Aidha, lugha ya alama inawawezesha pia kupata habari ambapo baadhi ya vyombo vya habari huvitumia.

Ndugu Wanahabari

• Elimu ya Juu
Elimu ya Juu imekuwa ikitolewa kwa lengo la kuwezesha wanufaika kupata maarifa na umahiri katika fani stahiki.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianza kama Chuo Kikuu Kishiriki cha London mnamo tarehe 25 Oktoba, 1961 siku chache kabla ya Uhuru wa Tanganyika. Chuo hiki kilipoanzishwa kilikuwa na Kitivo kimoja tu cha Sheria, wahadhiri 6 na wanafunzi 14 ambapo mwanamke alikuwa mmoja tu aliyeitwa Julie Manning. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipata hadhi ya kuwa Chuo Kikuu kamili mwaka 1970 kupitia Sheria Na. 12 ya mwaka 1970.

Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeendelea kukua Kitaaluma, Kitafiti na Kimiundombinu ambapo idadi ya wanafunzi imefikia 43,307 katika mwaka wa masomo 2020/21 ambapo wanawake ni 19,785 sawa na asilimia 45.7. Chuo hiki kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha rasilimaliwatu yenye umahiri katika nchi yetu.

Aidha, tumeshuhudia uanzishwaji wa Vyuo Vikuu vingine vya kimkakati ikiwa ni pamoja na: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na Chuo Kikuu Huria ambacho kinatoa fursa kwa elimu ya juu kwa njia ya masafa. Hadi kufikia mwaka 2021 kuna jumla ya Taasisi za Elimu ya Juu 78 zikiwemo za Umma 48 na binafsi 30.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kilianzishwa rasmi tarehe 01 Julai, 1984 kwa Sheria ya Bunge Na.6 ya mwaka 1984. Chuo kilipewa jina hilo kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Mhe. Edward Moringe Sokoine aliyefariki dunia mwaka 1984.

Chuo hiki kilianzishwa ili kuandaa wataalam wa kilimo katika nyanja mbalimbali. Chuo kilianza na program 3 za masomo mwaka 1984; ambapo zimeongezeka na kufikia 116 mwaka 2021. Aidha, Chuo kimeendelea kujiimarisha kwa kutoa mafunzo kwa vitendo na kufanya tafiti zenye lengo la kuongeza tija katika kilimo na kuongeza thamani ya mazao.

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)
Mradi huu uliidhinishwa na Bodi ya Benki ya Dunia mnamo tarehe
27/05/2021. Makubaliano kati ya Benki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu utekelezaji wa mradi huu yaliyosainiwa tarehe 19/8/2021 chini ya uongozi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Mradi huu utatekelezwa ndani ya miaka mitano una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 425 sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 972. Mradi unatarajia kufanya mambo yafuatayo;
(i) Utajenga mabweni 34, vyumba vya mihadhara na madarasa 130, kumbi za mikutano ya kisayansi 23, maabara/karakana 108, na vituo atamizi 10; na kuboresha mitaala zaidi ya 290;

(ii) kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za sayansi, teknolojia, uhandishi na hisabati (STEM) kutoka wanafunzi 40,000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026;

(iii) Utasomesha Wahadhiri 623 (wanawake 268, wanaume 355) katika shahada ya Uzamivu (PhD) na Wahadhiri 477 (wanawake 197, wanaume 280) katika shahada ya Umahiri

(MSc);
(iv) kujenga Chuo Kikuu kipya cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Butiama; na
(v) kujenga Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi katika eneo la Mloganzila.

Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi huu muhimu ambao kwa hakika utaleta mageuzi makubwa katika Elimu ya Juu nchini.
Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu yamekuwa yakitiliwa mkazo na kupewa kipaumbele tangu miaka ya 1960. Sera ya kwanza ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Utafiti ilianzishwa mwaka 1985. Sera hii ilikuwa na malengo ya kutoa mwongozo wa jinsi ya kusimamia masuala ya sayansi, teknolojia na utafiti nchini, ikiwa ni pamoja na kuchagua, kutathmini na kuhawilisha teknolojia; na kupunguza utegemezi katika teknolojia kutoka nje ya nchi. Mwaka 1996, sera hiyo ilifanyiwa mapitio na kuwa Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 (National Science and Technology Policy, 1996). Mafanikio yaliyofikiwa kwenye Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni pamoja na:

• Kuanzishwa kwa vyuo vya sayansi na teknolojia nchini ambavyo ni: Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam (1962) ambacho sasa kinajulikana kama Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Ufundi cha Mbeya (mwaka 1986) ambacho kwa sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya; na Chuo cha Ufundi Arusha. Vyuo hivi vilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kuzalisha mafundi sanifu katika fani mbalimbali za uhandisi;

• Kuanzishwa kwa Chuo cha Ufundi Dodoma ambacho ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 17.3 ikiwa ni hatua muhimu kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuhakikisha kuwa elimu inaweka msisitizo katika kujenda ujuzi. Ujenzi ulianza Mwezi Agosti 2021 na unatarajiwa kukamilika Februari 2023;

• Kuanzishwa kwa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela, iliyoanza kutoa mafunzo rasmi mwaka 2011. Taasisi hii ilianzishwa ili Kuchochea Sayansi na Teknolojia katika viwango vya kimataifa Barani Afrika. Chuo hiki kinatoa program zinazolenga kujenga uwezo wa nchi ili kuendana na mahitaji ya mapinduzi ya nne ya viwanda;

• Kuanzishwa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission - TAEC) kwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano Tanzania Na. 7 ya mwaka 2003 ili kusimamia, kudhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini;

• Kuanzishwa kwa kumbi za atamizi na ubunifu ambapo kumbi ya kwanza iitwayo Buni Hub ilianzishwa Mwaka 2011, ikijikita kwenye ubunifu katika masuala ya TEHAMA. Hadi kufikia mwaka 2021 kuwa jumla kumbi na atamizi za ubunifu 41 ambazo zimewezesha kuanzishwa kwa makampuni machanga 94. Makampuni hayo yamezalisha ajira za moja kwa moja kwa wananchi takribani 600 na ajira zisizo za moja kwa moja kwa wananchi takribani 15,000;

• Kupitia mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi wa Elimu ya Juu Serikali ya awamu ya sita itaongeza kumbi za atamizi na ubunifu 10 ili kukidhi lengo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha wabunifu wanaendelezwa ili bunifu zao zifikie kiwango cha kuingia kwenye kiwango cha biashara; na

• Kuanzishwa kwa vituo vya umahiri katika fani za: Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Teknolojia ya ngozi, Teknolojia katika usafiri wa anga, pamoja na Maji na Nishati Jadidifu. Vituo hivi vya umahiri vinajengwa kupitia mradi wa ESTRIP wenye thamani ya shilingi bilioni 174 ambao unatekelezwa katika Chuo Cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.

Mweleko wa Sekta ya Elimu
Ndugu Wanahabari;
Mwelekeo wa Sekta ya Elimu baada ya Miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu ni kuendelea kutoa elimu bora itakayoipatia jamii maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Serikali itachukua hatua zifuatazo ili kuimarisha elimu na kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa Elimu:

1. Serikali itahakikisha kwamba inaboresha mitaala ya elimu katika ngazi zote na kuweka msisitizo zaidi katika masuala ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Ujasiliamali, Stadi za kazi na masuala mtambuka. Aidha, fani za kimkakati kama vile uhandisi, kilimo, udaktari zitendelea kupewa kipaumbele;

2. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuendelea kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume. Kazi hii inafanyika kwa kasi zaidi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sambamba na ujenzi wa madarasa 15,000 unaoendelea nchini Serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari za kutwa na shule za sekondari 26 za wasichana katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji umeanza kwa shule 274 za kutwa na shule 10 za Wasichana ambapo serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 1,405 mnamo tarehe Novemba, 2021.

3. Elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi stati itaendelea kuimarishwa. Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya ufundi stadi katika Wiaya 29 na Mikoa. Lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kwa msingi huo, mafunzo kwa vitendo yatapewa uzito stahiki sambamba na kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira;.

4. Serikali itaendelea kuimarisha elimu maalum kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Aidha, Serikali itaendelea kununua vifaa visaidizi ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza kwa ufanisi zaidi;

5. Serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu. Wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni. Fursa hizo zitajumuisha wasichana ambao wanapata ujauzito wakiwa katika shule za msingi au sekondari. Wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi baada ya kujifungua; na

6. Wanafunzi wanaobainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi, ambao matokeo yao hufutwa, pamoja na wanafunzi wanaoshindwa kufaulu mtihani au wanaopata matatizo yoyote wakati wa mitihani watapewa fursa ya kurudia Mtihani mwaka unaofuata. Baraza la Mitihani la Tanzania litatoa utaratibu wa kurudia mitihani. Aidha, wanafunzi ambao na watakaofaulu mitihani ya marudio watapata fursa ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule za serikali.

Hatua hiyo imezingatia kuwa, watahiniwa wa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita wanaofutiwa matokeo yao, wanashindwa kufaulu na wanaopata matatizo hupewa fursa ya kurudia mtihani. Hivyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwapa nafasi ya pili wanafunzi wanaomaliza Elimu ya Msingi kama inavyofanyika kwa wanafunzi wa Sekondari. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya watumishi wote watakaobainika kuhusika na udanganyifu katika mitihani yote ya Taifa.

7. Serikali itaendelea kutoa elimu bila malipo ili kuhakikisha kuwa watoto wote wakitanzania wanapata elimu bila vikwazo. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti iliyoongezeka kutoka bilion 464 hadi 570.

Ndugu wanahabari;
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba Serikali ya Awamu Sita itaendelea kuboresha elimu, sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kuinua sekta ya elimu. Tumeshuhudia mambo makubwa ambayo yamefanyika katika sekta ya elimu ndani ya kipindi cha miezi nane tu ya uongozi wake. Hivyo, ninawaomba na kuwasihi saana watanzania wenzangu tuendelee kumuunga mkono Rais wetu ili dhamira yake njema ya kuleta maendeleo katika nchi yetu na ustawi wa watanzania iweze kufikiwa.

Mwisho nichukue nafasi hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kusherehekea Miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu na KAZI IENDELEE.

Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Wabariki Watanzania Wote
Asanteni kwa Kunisikiliza.
 
Waziri wa Elimu Prof. Ndalichako amesema Wanafunzi wa Shule za Msingi/Sekondari watakaokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na changamoto za kifamilia watapewa nafasi ya kurejea Shuleni katika mfumo rasmi “leo leo natoa waraka zege halilali"

Millard Ayo
Three different stances on one issue by one government
  • Ilisemwa mwanzoni mwanafunzi akishapata ujauzito basi akae nyumbani alee mtoto
  • WB wakabana tukasema wataendelea lakini si kwa mfumo maalum watasoma kwa utaratibu maalum ambao mpaka leo haujaelezwa
  • Leo tena nasikia watasoma kwa utaratibu wakawaida
  • kesho watasemaje?
 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari watakaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na changamoto mbalimbali za kifamilia watapewa fursa ya kurejea Shuleni katika mfumo rasmi.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hii leo akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 "leo natoa waraka wa elimu ambao utaelezea ni lini Wanafunzi watakaokatisha masomo kwa sababu ya mimba na changamoto nyingine watapaswa kurejea Shuleni, leoleo natoa waraka hakuna kupoa, zege halilali"

Wizara ya Elimu inaelezea mafaniko yake ndani ya miaka 60 ya Uhuru kwa kutumia hashtag ya "Tunaboresha Elimu yetu"

My Take
Kama mnakumbuka tuliishauri sana serikali na maamuzi haya ya hovyo,ikakaza shingo. Waziri Ndalichako alikuwepo, mama Samia alikuwepo. Kwa mantiki hii Waziri anatakiwa ajiuzuru kwa kutokuwa na msaada wowte katika nchi ukizingatia kuna wanafunzi wameshaadhirika.
 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari watakaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na changamoto mbalimbali za kifamilia watapewa fursa ya kurejea Shuleni katika mfumo rasmi.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hii leo akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 "leo natoa waraka wa elimu ambao utaelezea ni lini Wanafunzi watakaokatisha masomo kwa sababu ya mimba na changamoto nyingine watapaswa kurejea Shuleni, leoleo natoa waraka hakuna kupoa, zege halilali"

Wizara ya Elimu inaelezea mafaniko yake ndani ya miaka 60 ya Uhuru kwa kutumia hashtag ya "Tunaboresha Elimu yetu"

My Take
Kama mnakumbuka tuliishauri sana serikali na maamuzi haya ya hovyo,ikakaza shingo. Waziri Ndalichako alikuwepo, mama Samia alikuwepo. Kwa mantiki hii Waziri anatakiwa ajiuzuru kwa kutokuwa na msaada wowte katika nchi ukizingatia kuna wanafunzi wameshaadhirika.
Hawa hawaaminniki, usiwaamini. Ushungi usimuamini katu
 
17 Reactions
Reply
Back
Top Bottom