kaisa079
Member
- Nov 16, 2007
- 20
- 0
Bajaj sasa kuwa 'ambulance'
SERIKALI itatoa pikipiki za magurudumu matatu (bajaj) kwa vituo vyote vya afya na zahanati nchini, ili kukabiliana na tatizo la usafiri kwa wagonjwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema wizara yake tayari imetenga fedha kwa ajili ya kununua pikipiki hizo, ambapo kwa kuanzia, zitanunuliwa 350 na kusambazwa katika vituo vya afya 481 katika wilaya zote.
Alisema pikipiki hizo zitafungwa vitanda na wagonjwa kusafirishwa kutoka vituo vya afya kwenda katika hospitali za wilaya.
"Tunaamini tutakaposambaza bajaj hizo tutakuwa tumefanikiwa kwa kiasi fulani kupunguza vifo vya wagonjwa ambavyo vingine vinatokana na kukosekana kwa usafiri wa wagonjwa," alisema Profesa Mwakyusa.
Alisema kwa kuwa mpango huo utaanza na pikipiki chache, ikilinganishwa na idadi ya vituo vya afya, ambavyo ni ya 481, wizara itaangalia wilaya ambazo zitaonekana kuwa na tatizo kubwa la usafiri, ambapo wataanza na Muleba mkoani Kagera, ambapo pia mgao huo utaangalia wilaya nyingine 26 ambazo kasi ya malaria iko juu.
Kuhusu mapambano dhidi ya malaria, Profesa Mwakyusa alisema Serikali inahimiza wananchi kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kuwataka wafukie madimbwi ya maji machafu, ambamo mbu hufanya mazalio na makazi yao.
Alisema wakati wananchi wakiendelea na mapambano dhidi ya malaria, kuna mtu amejitokeza kwa ajili ya kuisaidia Tanzania vyandarua milioni 12, ili viweze kusambazwa katika vituo vya afya kwa ajili ya wananchi.
Alisema mtu huyo anaishi Marekani na amekuwa rafiki mkubwa wa Serikali ya Tanzania, lakini hakutaka kuliweka jina mtu huyo hadharani.
"Nimekuwa na mawasiliano mazuri na mtu huyo na kuzungumza naye kuhusu vyandarua hivyo, lakini awali alishakutana na Rais Jakaya kikwete, Marekani, na kuelezea nia yake ya kutusaidia baada ya Rais kumweleza mikakati na sera za afya nchini, katika mapambano dhidi ya malaria," alisema.
Pia aliwataka wananchi kutumia dawa za ALU kutibu malaria, kwani uwezo wake ni mkubwa ikilinganishwa na SP na klorokwini, ambazo uwezo wake ni mdogo kutokana na kutumika muda mrefu na kuwa sugu.
Kuhusu upatikanaji wa vifaa na dawa katika vituo vya afya, alisema kwa sasa umeandaliwa mpango maalumu ambao utasaidia kuondoa kero iliyopo kwa baadhi ya maeneo ambapo wananchi wamekuwa wakilalamika kukosa dawa na vifaa kwa wakati.
Kuhusu maambukizi ya UKIMWI, Profesa Mwakyusa alisema kutokana na kampeni ya upimaji kwa hiyari iliyoanza Julai 14 mwaka huu, mafanikio yapo kwani watu wamejitokeza kwa wingi na kupima afya zao.
Alisema hali hiyo imeleta mtazamo mpya, kwani siku zote Serikali imekuwa ikitangaza kuwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ni asilimia 7 wakati hali iliyopo sasa inaonesha kasi imepungua na kufikia asilimia 4.9.
Hata hivyo, wakati kasi ikionekana kupungua, mkoa wa Iringa unaongoza kwa kasi ya maambukizi mapya ya UKIMWI kwa asilimia 12.6 ukifuatiwa na Mbeya ambao una asilimia 12.1.
Wakati mikoa hiyo ikiwa juu, mkoa wa Kigoma ni wa mwisho kasi ya maambukizi ambayo ni asilimia 1.2, ukifutiwa na Manyara asilimia 1.6 na Kilimanjaro asilimia 1.7.
Pia alisema Mkoa wa Dar es Salaam umeonekana kupungua kasi ya maambukizi ikilinganishwa na miaka iliyopita kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kasi ya maambukizi kwa mkoa huo ni asilimia 5.9.
Kuhusu ebola, Profesa Mwakyusa alisema Serikali inaendelea kujipanga vyema katika kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini kwa kupeleka wataalamu katika mikoa ya mipakani, ili waweze kufuatilia kwa makini dalili za ugonjwa huo.
Kuhusu Mfuko wa Bima ya Afya, alisema nchi karibu zote zilizoendelea zinatumia utaratibu huo wa kutumia huduma za bima ya afya, hivyo aliwataka wananchi kuunga mkono mpango huo.
Profesa Mwakyusa akizungumzia suala la kuboresha huduma za afya Mkoa wa Dar es Salaam alisema tayari mpango wa kujenga Hospitali ya Mkoa umekamilika na itajengwa Msasani eneo la TIRDO.
Alisema CCBRT ilijitolea kujenga hospitali hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa ambapo Wizara ya Afya imetenga sh. milioni 600 katika kusaidia ujenzi huo.
Kuhusu Ripoti ya Sakata la upasuaji kimakosa, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) ripoti itatangazwa baadaye kutokana na kushindikana kutangazwa jana, kwa kuwa Profesa Mwakyusa anaratajiwa kwenda kijiji cha Partimbo, Kiteto kwa ajili ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kiteto, marehemu Benedict Losurutia anayetarajiwa kuzikwa leo